Walia kupoteza fedha mradi wa kuku

Dar es Salaam. Sikio la kufa halisikii dawa, ni msemo unaoakisi yaliyowafika wanachama wa Taasisi ya Tanzania Community Empowerment Association (Tancea) takribani 50,000 kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Taasisi hiyo ilianzishwa Julai 2021 kwa lengo la kuwasaidia wafugaji wa kuku kupata mitaji, mabanda, vyakula na dawa za kuku wa nyama (broilers).

Baadhi ya wanachama waliozungumza na Mwananchi wamedai waliahidiwa kujengewa mabanda, kupewa vifaranga 1,000, vyakula na dawa za mifugo, mambo ambayo hayakutekelezwa, wakiishia kuchangishwa fedha.

Hata hivyo, uongozi wa Tancea kupitia mwanasheria wake, Jane Gerald umewataka wanachama kufuata utaratibu kudai fedha zao kuliko kulalamika mitaani.

Kutokana na mvutano huo, pande hizo mbili zimekutana leo Novemba 7, 2024 katika kikao kilichofanyika mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo.

Malalamiko hayo yanatolewa kukiwa na kesi kadhaa zinazofanana na hiyo, ikiwamo ya Development Entrepreneurship Community Initiative (Deci) iliyofungiwa na Serikali baada ya wananchi waliochangishwa kupoteza fedha zao.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni katika Kijiji cha Mwanambaya wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani, Grace Komba aliyekuwa mkuu wa kikundi cha watu 300 cha Tanceat katika eneo hilo, anadai waliaminishwa kuwa watapewa misaada ya ufugaji.

“Awali walitualika wakasema wanaanzisha umoja wa wafuga kuku wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa wilaya zote za mikoa hiyo na tulifikia zaidi ya 50,000,” anasema.

Anadai walikuwa wakikutana Kitunda kwa Bibi Jela kupata maelezo ya mradi utakavyokuwa.

“Mwanzoni walikuwa wanasema hatutatoa chochote kwa sababu Serikali imeshatoa fedha nyingi na watakaonufaika ni wastaafu na vijana waliomaliza vyuo. 

“Walisema kuna wafadhili wametoa fedha nyingi, hivyo sisi hatutatoa hata senti tano. Hivyo wakasema kila mmoja atakuwa na banda la kufugia kuku 1,000 na watafunga kamera itakayokuwa imeunganishwa hadi makao makuu itakayokuwa ikifuatilia,” anadai akieleza waliamini kwa kuwa waliajiriwa madaktari wastaafu na waliotoka vyuoni.

Anadai mkurugenzi ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya Udhamini (mweka hazina), Mathias Fulgence alitoa barua ya Januari 25, 2022 kwa wanachama wote, akitoa mrejesho wa kikao cha wajumbe wa bodi 21.

“Mathias akasema wamesajili umoja wa wafuga kuku, lakini walipokwenda kwa wahisani, wamepata maswali waliyoshindwa kuyajibu; kwamba sisi tutamkabidhi mwanachama banda la mamilioni, halafu hajaonyesha juhudi zozote, hana kitambulisho, hajatoa kiingilio.

Anadai kwenye ubao wa matangazo usajili uliobandikwa ni wa Tancea tofauti na walivyoelezwa awali kuhusu Tanceat, hivyo waliamini ni kosa la uchapaji.

Anadai namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) iliwashitua pia kwa kuwa ilikuwa tofauti na iliyoandikwa kwenye risiti ya malipo.

“Kwamba ile Association waliyosajili ina akaunti kwenye benki nne tofauti, halafu umoja wetu wenye Trust hauna akaunti yoyote,” anasema.

Anadai katika barua hiyo, walitakiwa kutoa Sh10,000 za kiingilio, Sh10,000 za mkataba, Sh3,000 za katiba na Sh3,000 za kanuni, jumla Sh26,000 ili kuwapa imani wafadhili.

“Mpaka leo miaka miwili na miezi minne, hakuna cha banda, wala kitambulisho alichopewa mwanachama yeyote. Wakaja tena wakasema tujaze mikataba ya ile Tanceat ambayo haijasajiliwa, lakini ile michango tunaelekezwa tuweke kwenye akaunti ya Tancea,” anasema. 

Anadai mwisho wa Januari 2022 walipelekewa kibali kutoka Ofisi ya Rais, Tamisemi kwamba wana Tancea wamekubaliwa kufanya mafunzo kwa wafuga kuku na utengenezaji wa chakula cha kuku, hivyo wakaamini na kuanza kuchangia.

Anadai alilipa mchango wake na ndugu zake 42.

“Nililipa Januari 26, 2022 na walikuwa wanataka risiti ya benki uipeleke siku hiyohiyo ofisi za Kitunda, wao wanakuandikia risiti nyingine yenye namba ya TIN tofauti na kule ulikoweka hela,” anadai na kueleza hata baada ya kutoa fedha hakuna kilichofanyika.

“Wakaja na gia nyingine, kwamba wafadhili wamesema lazima watukute tumeanza wenyewe, hivyo kama una nyumba yako unatenga chumba, hata kama ni kuku 100 wa kujifunzia. Wakasema kila mwanachama atoe Sh250,000 kwa ajili ya bima ya biashara wanazofanya. Baada ya hapo hakukuwa na uwekezaji wowote,” anadai.

Baada ya hapo anadai walitakiwa kuchangia Sh100,000 ili kupata mikopo ya pikipiki za magurudumu matatu (toyo) mashine za kutengeneza chakula cha kuku na mahindi ya kuanzia mradi.

“Watu wakatoa, lakini baada ya hapo hakuna cha mashine, toyo wala mahindi,” anadai.

Anadai pia walielezwa kuhusu mradi wa kuuza vyakula vya kuku hivyo wakatakiwa kununua kitabu cha kuweka kumbukumbu Sh10,000, huku wakielekezwa kupeleka mahindi na mihogo kwa ajili ya uzalishaji wa chakula cha kuku.

“Walisema baada ya kuuza kuku tutakuwa tukipata gawio la Sh2 milioni kwa awamu tatu, kwanza asilimia 60 (Sh1.2 milioni), yaani wakishauza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya wiki moja ndipo tunalipwa.

“Halafu asilimia 30 ambayo ni Sh600,000 wanakuwekea kwa miezi sita halafu wanakupa ili ufanye malengo yako,” anadai akieleza uzinduzi wa mradi wa uzalishaji wa chakula cha kuku ulidaiwa kufanyika Desemba 21, 2022 wilayani Mkuranga wakatakiwa kuchanga Sh10,000.

Anadai uzinduzi haukufanyika na malalamiko wameyawasilisha kwa mamlaka mbalimbali za Serikali.

Shukuru Jongo, mkazi wa Kijiji cha Mwanzega wilayani Mkuranga anadai alihamasishwa akaunda kikundi cha watu 450 ambao pia walikuwa wakichangishwa.

“Siaminiki tena, naonekana nimekuwa tapeli. Katika uchaguzi wa serikali za mitaa niligombea uenyekiti wa kijiji, ndio maswali yalikuwa hayohayo. Ooh! Wewe ulitutapeli fedha zetu, leo tukupe kijiji si ndiyo utatuuza kabisa?” anadai.

John Shao, mkazi wa Yombo Buza, wilayani Temeke anadai alikuwa akiuza mayai, lakini aliposhawishiwa kuingia Tancea aliacha akitumaini kupata mtaji mkubwa zaidi, lakini ameambulia patupu.

Alipotafutwa kuzungumzia malalamiko hayo Novemba 5, 2024 saa 12.33 jioni, Fulgence Mathias alimtaka mwandishi kufika ofisini kwao Kitunda.

Mwandishi leo Novemba 7 alipofika katika ofisi hizo hakumkuta Mathias, ambaye alipotafutwa kwa simu alimtaka wawasiliane baadaye ili ampangie siku ya kukutana wiki ijayo. 

Hata hivyo, katika kikao kilichofanyika mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mpogolo, mwanasheria wa taasisi hiyo, Jane Gerald amesema wakati mwingine ni rahisi kwa wadaiwa hao kusema wameshawasilisha madai yao kwa viongozi mbalimbali wa kampuni hiyo akiwemo mkurugenzi, lakini kama mwanasheria anayepaswa kuyashughulikia akawa hana taarifa.

“Ukiniuliza mimi nitakuambia sina taarifa kwa sababu sijapewa barua,” amesema.

Amesema baadhi ya wanachama walifunguliwa kesi mahakamani kwa kuiba bidhaa walizotakiwa wauze ukiwamo unga. 

“Walifilisi wenyewe wanachama, walipewa unga na hawakuleta hela, wengine walitapeli, lakini tuko katika hatua za kujiimarisha,” amesema mwanasheria huyo.

Hata hivyo akijibu hoja hiyo mbele ya mkuu wa wilaya, Grace Komba amesema malipo ya bima ya Sh250,000 yalimwezesha kupewa  viroba vya unga vya hadi Sh300,000 ili akauze mtaani na atakapomaliza awasilishe fedha taslimu ofisini.

“Mimi nimeuza sana unga, karibu kilo 600 hadi nilipoona hakuna faida yoyote ninayoipata, hapo nilikuwa nafanya hivi nikiwa nimeshaacha kufuga kuku ambao nilikuwa nikiwafuga awali na kuuza mayai kwa wachuuzi wangu wa rejareja,” amedai Komba.

DC Mpogolo atoa maelekezo

Katika kushughulikia suala hilo, Mpogolo aliwataka wananchi hao kuandika madai yao kwa maandishi na kuyawasilisha katika ofisi za taasisi hiyo na kumpatia nakala ili kufanya mambo yaende kwa utaratibu unaoeleweka.

Akitoa maelekezo hayo pia aliahidi kutuma timu yake kwenda kufuatilia suala hilo.

Mpogolo aliitaka taasisi hiyo kuhakikisha inashughulikia mifumo yake ya uendeshaji kwenda kuwa chama cha ushirika au kampuni ya watu, kutoka mfumo uliopo sasa ili kuweka urahisi katika usimamizi.

“Mimi hili nitaendelea kulifuatilia ili wengine wasiendelee kutapeliwa. Wao nawaagiza vitu viwili waende kwa mrajisi wa vyama kuwa wanaanzisha ushirika wao na wafuate sheria za mrajisi vyama au wakafloat public share (wakauze hisa)ili wawe kampuni ya watu (PLC), wakati huo mimi nitatuma watu wangu,” amesema.

Related Posts