Dar es Salaam. Serikali imesema inatarajia kuwa na mashahidi 10 katika kesi ya kujipatia Sh661 milioni kwa njia ya udanganyifu inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Samna Investment Ltd, Samuel Nakei (50).
Nakei, ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Kitumbini, anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia fedha kwa njia ya kudanganyifu kwa madai atauza vyuma chakavu, jambo ambalo alijua ni uongo.
Mashahidi hao pamoja na vielelezo, wanatarajia kutoa ushahidi wao, Desemba 5, 2924 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Neema Moshi ameieleza mahakama hiyo leo Alhamisi, Novemba 7, 2024 wakati akimsomea hoja za awali (PH) mshtakiwa huyo.
Mshtakiwa huyo amesomewa maelezo hayo, baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika.
Moshi amemsomea maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga, anayesikiliza shauri hilo.
Kabla ya kusomewa maelezo yake, wakili Moshi alimkumbusha mashitaka yanayomkabili kwa kumsomea upya.
Baada ya hapo, Moshi alimsomea maelezo ya awali, ambapo amedai kati ya Septemba na Oktoba 2021 katika jiji la Dar es Salaam, Nakei akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Samna Investment Ltd, kwa lengo kuwahadaa na kudanganya na alijipatia Sh570 milioni kutoka kwa Abdallah Ngunya kwa kumueleza kuwa atamuuzia vyuma chakavu.
Aliendelea kudai mahakamani hapo katika kipindi hicho ndani ya Jiji la Dar es Salaa, Nakei anadaiwa pia kujipatia kwa njia ya udanganyifu Sh91 milioni kutoka kwa Silvano Lyimo, kwa maelezo kuwa atamuuzia vyuma chakavu, wakati akijua kuwa ni ongo.
Moshi alidai kuwa mshtakiwa huyo alimuelekeza Ngunya na Lyimo waingize fedha hizo katika akaunti yake iliyopo katika Benki ya CRDB.
Wakili Moshi aliendelea kudai kuwa walalamikaji hao baada ya kulipa, Nakei aliwaandalia safari ya kuwapeleka maeneo matatu yaliyokuwa na vyuma hivyo.
Amedai mshtakiwa aliwapeleka eneo la Kizota lililopo Dodoma, Lugoba lililopo Chalinze na Tabata lililopo Dar es Salaam, ambapo aliwaonyesha vyuma hivyo.
“Hata hivyo, vyuma hivyo chakavu vilibainika siyo mali ya Nakei, bali ni mali ya Kampuni Badr East Africa.
Washtakiwa baada ya kugunduua hivyo, waliomtaka mshtakiwa awarudishie fedha zao, lakini hakufanya hivyo.
Baada ya Nakei kushindwa kurudisha fedha hizo, walalamikaji walikwenda kulalamika kituo cha polisi.
“Mshtakiwa alikamatwa na kufikishwa kituo Kikuu cha Polisi (Central) Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano na baada ya upelelezi kukamilika, alifikishwa Mahakamani kujibu mashtaka yake,” amesema.
Baada ya kumaliza kusomewa maelezo yake, mshtakiwa alikubali majina yake na anuani yake, siku alipofikishwa Polisi, siku alipofikishwa mahakamani na pia anakiri kuwafahamu walalamikaji wa kesi hiyo.
Hakimu Kiswaga baada ya kusikiliza hoja hizo, aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 5, 2024 itakapoitwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka.
Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.