Mwanza. Katika kipindi cha Januari hadi Juni, 2024 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika mikoa mbalimbali nchini imetoa taarifa za utekelezaji wa shughuli zake, ikiwemo malalamiko ya rushwa iliyopokea na kuyafanyia kazi.
Katika taarifa hizo, miongoni mwa maeneo mengi yaliyolalamikiwa kuomba na kupokea rushwa ni serikali za mitaa ambazo zipo chini Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Sababu za rushwa kuzagaa eneo hilo ikitajwa kuwa viongozi wengi wa mitaa wanategemea uenyekiti kujipatia kipato.
Mathalani, katika taarifa ya Takukuru kwa kipindi cha Aprili hadi Juni 2024 mkoani Lindi, taasisi hiyo ilipokea malalamiko 61, kati ya hayo 52 yalihusu rushwa huku serikali za mitaa zikiongoza kulalamikiwa kwa kuwa na malalamiko 18.
Katika kipindi hichohicho, Takukuru mkoani Tabora ilipokea malalamiko 114 kati ya hayo 95 yalihusu rushwa na serikali za mitaa zikawa kinara kwa kuwa na malalamiko 83 ya rushwa.
Takukuru Kinondoni pia ilipokea malalamiko 88 ya rushwa kati ya hayo 13 yalihusu serikali za mitaa, Mkoa wa Kilimanjaro malalamiko 109 yalipokewa kwa kipindi hicho, huku 54 yakihusu rushwa na serikali za mitaa ziliongoza kwa kulalamikiwa mara 35.
Mbali ya hayo, Takukuru mkoani Mara ilipokea malalamiko 110 kati yake 68 yalihusu rushwa na serikali za mitaa ziliongoza kwa kulalamikiwa kwa kuwa na malalamiko 25 sawa na asilimia 37 ya malalamiko yote.
Kutokana na serikali za mitaa kulalamikiwa kwa rushwa, wananchi wametakiwa kuwafuatilia wakati wa kampeni zinazoanza Novemba 20 hadi 26, 2024 kisha kuwachagua viongozi wa mitaa wanaojihusisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazowaingizia vipato, kama ambavyo kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wa kamati ya mtaa katika Mamlaka za Miji za Mwaka 2024 zinavyotaka.
Kwa mujibu wa kanuni hiyo, Kamati ya Mtaa itakuwa na wajumbe wasiozidi sita ambao ni mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wengine watano ambao kati yao wajumbe wawili watakuwa wanawake.
Moja ya sifa za mgombea wa nafasi hizo iliyotajwa katika Kanuni ya 15 ya uchaguzi wa serikali za mitaa ni kuwa na shughuli halali ya kumwezesha kuishi.
“Mkazi yeyote wa mtaa anaweza kugombea uenyekiti wa mtaa au ujumbe wa kamati ya mtaa endapo ni raia wa Tanzania, ana umri wa miaka 21 au zaidi, ana uwezo wa kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza, ana shughuli halali ya kumwezesha kuishi, ni mkazi wa eneo la mtaa, ni mwanachama wa chama cha siasa na amedhaminiwa na chama hicho na ana akili timamu,” inaeleza kanuni hiyo.
Mkazi jijini Mwanza, Mayala Damian anasema sababu kubwa ya viongozi wa serikali za mitaa kuongoza kwenye malalamiko ya kuomba rushwa ni kuingia kwenye uongozi wakiwa wana matarajio makubwa ya kunufaika kiuchumi, wakidhani watapata mishahara na posho kitu ambacho siyo uhalisia.
“Wenyeviti hawana marupurupu yanayoeleweka kutoka serikalini kwa hiyo kama hana shughuli nyingine ya kujipatia kipato mara nyingi anategemea vihela vidogovidogo kwa wanaotaka huduma kwenye ofisi zao. Mfano mwananchi anataka muhuri tu anatozwa Sh5,000 kwa hiyo wakati huu ndiyo wa kuwapiga chini viongozi kama hao,” anasema Damian.
“Yaani hata wanafunzi wakipeleka zile barua za kuthibitisha makazi yao nao wanatozwa pesa, mwananchi tu unahitaji labda barua ya mtaa unaambiwa kutoa kopi ni Sh2,000 kweli tangu lini kutoa kopi ikawa bei hiyo? lakini kwa kuwa mtu una shida utafanyaje unaitoa tu. Kwa hiyo wakati huu ndio sahihi wa kuwatoa wanaodhani uenyekiti ni kitega uchumi na kuwaweka watakaotuongoza,” anasema.
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza na Mwenyekiti wa Kamati ya Amani mkoani humo, Hassan Kabeke anasema hata katika vitabu vya dini (Biblia na Quran) rushwa imepigwa marufuku akitaka viongozi wa dini kuwahamasisha waumini wao kujitokeza kupiga kura Novemba 27, 2024 kuwachagua viongozi wanaofaa.
Sheikh wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Abdulwarith Juma anasema hata katika Quran Mtume (S.A.W) amesema amelaaniwa na ametolewa katika rehema za Mwenyezi Mungu yule mwenye kutoa na kupokea rushwa.
Anasema kama viongozi wa dini wana wajibu wa kuwaambia wananchi ukweli kwamba wanaogombea kwa kutoa rushwa hawafai kwa kuwa watakaopata uongozi kwa njia hiyo hawawezi kushughulikia matatizo ya wananchi, bali mamlaka yao waliyoyapata na namna gani watalinda mamlaka hayo.
“Tuna haki na wajibu kuwafahamisha waumini wetu ni aina gani ya viongozi tunaowataka,” anasema.
Askofu David Emmanuel ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la makanisa ya Kipentekoste (CPCT) mkoani Mwanza ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya amani, mkoani humo anasema viongozi wa dini wana jukumu la kwenda kuwahamasisha waumini, kujiepusha na kila aina ya rushwa na vishawishi katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Lakini cha pili tuwahamasishe kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura tarehe hiyo ikifika kwa kuwa kura ni haki ya kila mtu,” anasema.
Askofu wa Kanisa la Charismatic Episcopal Church of Tanzania (CECT), Charles Sekelwa anasema demokrasia siyo haki tu ya kupiga kura bali pia ni nafasi ya wananchi baada ya kusikiliza sera na kuamua nani wamchague kwa kuwa watakuwa tayari wamejua nini atawapatia.
Kazi za serikali za mitaa
Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 145 na 146, kazi za serikali za mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi, kuwashirikisha katika mipango na shughuli za utekelezaji maendeleo.
Katiba inaeleza bila ya kuathiri maelezo ya jumla yaliyomo katika ibara ndogo ya (1) ya ibara hii, hiki chombo cha serikali za mitaa, kwa kuzingatia masharti ya sheria iliyokianzisha, kitahusika na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa shughuli za kutekeleza kazi za serikali za mitaa katika eneo lake, kuhakikisha utekelezaji wa sheria , ulinzi wa wananchi, kuimarisha demokrasi katika eneo lake na kuitumia demokrasi kuharakisha maendeleo ya wananchi.