YANGA kwa mara ya kwanza msimu huu, inashuka uwanjani katika Ligi Kuu Bara bila ya mabeki wawili wa kati, Dickson Job na Ibrahim Bacca, itakapoikabili Tabora United yenye kocha mpya aliyewahi kuwanoa mastaa wa DR Congo akiwamo Maxi Nzengeli, Ellie Mpanzu, huku timu hiyo ikitamba itatonesha kidonda.
Mabeki hao wanatumikia adhabu ya kadi, huku Yanga ikitoka kupoteza mechi iliyopita mbele ya Azam FC, Bacca alilimwa kadi nyekundu katika mchezo huo, wakati Job anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano.
Yanga itakuwa wenyeji wa Tabora kwenye Uwanja wa Azam Complex, itawakosa mabeki hao walioanza kwa pambano katika mechi sita kati ya nane bila kuruhusu bao katika Ligi, lakini ikikutna na timu iliyotoka kushinda michezo miwili mfululizo dhidi ya Pamba Jiji na Mashujaa yote yakifungwa na Morice Chukwu.
AZIZI, NONDO
Kukosekana kwa Job na Bacca, moja kwa moja kunatoa nafasi kwa nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto pamoja na Aziz Andabwile kupewa nafasi kubwa ya kuziba mapengo hayo.
Andabwile aliyejiunga na Yanga msimu huu, kiasili ni kiungo mkabaji, lakini tangu ametua kikosini hapo amekuwa akichezeshwa beki wa kati, ambapo katika mechi tatu za ligi alizocheza dhidi ya KenGold (dakika 3), JKT Tanzania (dakika 90) na Coastal Union (dakika 10), ametumika beki wa kati.
Kabla ya hapo, Gamondi alianza kumtumia Andabwile kama beki wa kati kipindi cha pre season walipocheza dhidi ya TS Galaxy ya Afrika Kusini na Yanga kushinda 1-0, kisha katika Kilele cha Wiki ya Mwananchi kwa Yanga kuifunga Red Arrows ya Zambia mabao 2-1.
Kwa upande wa Mwamnyeto msimu huu ni kama amepoteza namba mbele ya Job na Bacca, wakati Yanga ikicheza mechi tisa za ligi, yeye amecheza nane kati ya hizo mbili akitokea benchi dhidi ya KMC na Simba.
Mbali na kukosekana wachezaji hao wawili wanaotumikia adhabu ya kadi, pia Yanga inatarajiwa kuikosa huduma ya Yao Kouassi aliye majeruhi kama ilivyo kwa Chadrack Boka.
Boka aliumia katika mchezo uliopita dhidi ya Azam akitolewa kipindi cha kwanza kilipomalizika, taarifa zilizopo ni kwamba hali yake kiafya sio nzuri na ilitarajiwa jana jioni aangaliwe kama kuna uwezekano wa kucheza. Kabla ya kuumia dhidi ya Azam, pia Boka alishindwa kumaliza mchezo wa nyuma dhidi ya Singida Black Stars ambao alitolewa mapema zaidi dakika ya 10.
Hata hivyo, Boka ambaye amekuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza msimu huu ndani ya Yanga akicheza beki wa kushoto, akikosekana anatumika Nickson Kibabage.
Boka akiwa amecheza mechi nane, amekuwa akipishana na Kibabage aliyecheza mechi nne na kwa upande wa kulia Yanga pia itamkosa Yao, kwa kawaida Gamondi humtumia Job anayekosekana leo, hivyo huenda Denis Nkane akacheza au Kibwana Shomari.
Nkane ambaye kiasili ni winga, Gamondi amempa jukumu jingine akiwa anamtumia kama beki wa kulia. Katika nafasi hiyo, amemtumia mara mbili msimu huu katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CBE wakati Yanga ikishinda 6-0 na Singida Black Stars.
Mbali na wachezaji hao, nafasi nyingine zipo imara hivyo ni jukumu la Gamondi kukipangilia vizuri kikosi chake ili kurudi kwenye hali ya ushindi.
Gamondi amezungumzia ishu ya kuwakosa wachezaji hao, alisema: “Ukiachana na Ibrahim Bacca mwenye kadi nyekundu, tuna Dickson Job ambaye ana kadi tatu za njano, Yao bado anaumwa hataweza kucheza. Kuna mchezaji ambaye bado tunaangalia hali yake ya afya (Boka) kuona kama anaweza kucheza. Hivyo tuna hao wachezaji wanne ambao ni ngumu kuwa nao kesho (leo).
“Lakini wapo wengine ambao wanaweza kuziba nafasi zao na mambo yakaenda vizuri kabisa.”
Wakati Yanga ikiwa inawakosa wachezaji wake wanne wa kikosi cha kwanza, upande wa Tabora United ipo full mziki, chini ya kocha mpya Anicet Kiazayidi, raia wa DR Congo, aliyewahi kuwanoa Nzengeli wa Yanga na Mpanzu wa Simba, Steven Ebuela (Al Hilal ya Sudan) alipokuwa Maniema Union, jambo linalowapa imani viongozi kuona wamepata mtu sahihi wa kutimiza malengo yao.
CV ya kocha huyo inaonyesha timu alizozifundisha ni AS Vita, As Simba, Les Aigles du Congo na Maniema Union, hivyo ujio wake unakwenda kuziba pengo la Mkenya Francis Kimanzi, lakini ikibebwa zaidi na nyota waliowahi kuitumikia Yanga, Heritier Makambo na Yacouba Songne ambao wote wamewahi kucheza Yanga huku kocha wa makipa wa kikosi hicho, Khalfan Mbonde akisisitiza kwamba: “Katika mchezo wa kesho (leo) wachezaji wetu wote wapo vizuri, hakuna tutakayemkosa.”
Katika kikosi hicho, pia kuna Morice Chukwu ambaye mechi mbili zilizopita ambazo Tabora United imezifunga Pamba Jiji (1-0) na Mashujaa (1-0), ndiye amefunga mabao hayo ya kuamua ushindi jambo ambalo linawatisha walinzi wa Yanga.
Kuhusu kuizuia safu ya ushambuliaji ya Tabora United, beki wa kushoto wa Yanga, Nickson Kibabage, amesema: “Kwa upande wa safu yetu ya ulinzi tunafahamu tunakwenda kukutana na safu ya ushambuliaji ya aina gani, mwalimu wetu tayari anawajua na ameshafanya tathmini namna gani ya kucheza dhidi yao.
“Kazi yetu sisi kama walinzi ni kufuata maelekezo ya walimu. Tunajua kesho (leo) watafanya kazi mara mbili ili kupata alama hivyo lazima tujiandae vyema.”