HUWEZI kuamini, ila ndivyo ukweli ulivyo, Yanga jana imechana mikeka ya wengi baada ya kupoteza mechi ya pili mfululizo katika Ligi Kuu Bara msimu huu ikiwa ni rekodi mbaya kwa klabu hiyo na kwa kocha Miguel Gamondi, baada ya kufumuliwa mabao 3-1 na Tabora United ikiwa kwenye uwanja wa nyumbani, jijini Dar.
Yanga ilikuwa imecheza mechi nane mfululizo bila kupoteza kabla ya Azam Fc wikiendi iliyopita kuwatibulia kwa kuwafunga bao 1-0 na jana tena Tabora kutonesha kipigo, kikiwa ni kikubwa cha kwanza tangu ilipofungwa 3-0 na Kagera Sugar kwenye uwanja wa nyumbani mechi iliyopigwa Januari 15, 2020.
Mabao hayo na ushindi huo kwa Tabora kwa jana yalikuwa ya kwanza kupata mbele ya Yanga tangu timu hiyo ilipopanda daraja msimu uliopita, kwani kabla ya hapo ilishakutana na wababe hao wa soka nchini na mara tatu na zote ilipoteza zikiwamo mbili za mbili za Ligi Kuu na moja ya Kombe la Shirikisho.
Tabora ilifungwa 3-0 katika mechi ya kwanza ya msimu uliopita ikiwa nyumbani kabla ya kulala 1-0 ugenini na katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita ikakumbana tena na kipigo cha 3-0 kabla ya jana Nyuki hao wa Tabora walijivua unyonge kwa kuibutua Yanga kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Katika mchezo wa jana, Yanga ilicheza bila mabeki wake mahiri wa kati, Ibrahim Bacca anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu na Dickson Job anayetumikia adhabu ya kadi tatu za njano na kumlazimisha kocha Gamondi kumchesha nahodha Bakar Mwamnyeto na Aziz Andabwile hata hivyo aliumia na kutolewa.
Andabwile aliumia dakika ya 10 aliporuka na kuanguka vibaya na kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliyechezesha kama kiungo namba sita na Khalid Aucho kurudi kucheza kama beki wa kati, lakini haikusaidia kuiokoa Yanga kuepuka aibu kwenye uwanja wa nyumbani kwa mara ya pili.
Pia iliwakosa mabeki wa pembeni wa kikosi cha kwanza Yao Kouassi na Chadrack Boka walio majeruhi na kuwatumia Denis Nkane na Nickson Kibabage ambao walizidiwa ujanja na nyota wa Tabora wakiongoza na Heritier Makambo, Yacouba Songne, Offen Chikola waliokuwa wakisumbua muda mrefu wa mchezo.
Katika mchezo huo hali ilionekana mapema Yanga haikuwa na siku nzuri kutokana na nyota walioanza kikosini kupoteza nafasi nyingi mbele ya kipa Hussein Masalanga ambaye hata hivyo hakumaliza mchezo huo alipoumia kipindi cha pili akiwa ameokoa penalti iliyopigwa na Stephane Aziz Ki.
Penalti hiyo ilitokana na beki Andy Bikoko kumchzezea vibayan, Pacome Zouzoua na mwamuzi Nassoro Mwinchui kuarumuru tuta na Aziz Ki kupiga mpira uliodakwa na Masalanga.
Kama kuna mchezaji ambaye aliyewaumiza Yanga kwa jana ni nyota wa zamani wa kikosi hicho, Yacouba Songne aliyetengeneza mabao mawili ya kwanza yaliyowekwa kimiani na Offen Chikola dakika ya 19 na sekunde chache kabla ya mapumziko.
Yacouba aliyeichezea Yanga kwa misimu miwili kabla ya kuhamia Ihefu na kisha kucheza Djibouti, aliisumbua ngome ya Yanga na kuhusika kutoa pasi na mabao yote mawili ya Chikola aliyemtungua Diarra Djigui kwa mashuti na kufanya hadi mapumziko Tabora inayonolewa na kocha mpya toka DR Congo Anicet Kiazayidi kuwa mbele kwa mabao 2-0. Mabao hayo yamemfanya Chikola kufikisha mabao matatu msimu huu y ligi.
Kipindi cha pili Yanga ilifanya mabadiliko kadhaa ikiwamo ya kuwaingiza Clement Mzize, Prince Dube na Clatous Chama, lakini mambo yalikuwa magumu hata pale Masalanga alipoumia na nafasi yake kuchukuliwa na Haroun Mandanda, kwani Tabora iliendelee kuisumbua Yanga.
Ilichofanya Tabora ni kurudia historia ya Juni 6,2023 ambapo Mbeya City ilipokuwa timu ya mwisho kwenda mapumziko ikiongoza kwa mabao 2-0 kwa mabao ya George Sangija dakika ya tatu na Richard Ngodya dakika ya 44, kwenye mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Ilichofanya Tabora ni kuwaachia Yanga washinde kwa kumiliki mpira ikimiliki mchezo kwa vipindi vyote viwili, lakini wageni wakipaki basi na wakatumia mashambulizi ya haraka kutengeneza mabao yao.
Dakika ya 77 kipindi cha pili Tabora wakapata bao la tatu kwa shambulizi kama hilo likifungwa kwa shuti na kiungo mkongomani, Nelson Munganga na kuimaliza Yanga.
Baada ya bao hilo la tatu mashabiki wa Yanga wakajikuta wanaondoka uwanjani wakiona hakuna nafasi ya kupindua matokeo hayo licha ya timu yao kumiliki mchezo kwa muda mrefu.
Hata hivyo, wakati mashabiki wakiamini Yanga imetoka mswaki kabisa, Mzize aliipatia Yanga bao la kufutia machozi dakika ya 90+4 kwenye dakika nane za nyongeza na kufanya mchezo huo.
Huo ni ushindi wa tatu mfululizo wa Tabora tangu ilipomtema kocha Mkenya Francis Kimanzi, kwani imetoka kuzifunga Pamba Jiji na Mashujaa na kuifanya sasa ifikishe pointi 17 na kupanda kwa nafasi moja kutoka ya saba hadi ya sita baada ya mechi 11 ikilinganana na Fountain Gate.