Ziara ya Rais Samia Cuba yasogezwa mbele

Dar es Salaam. Ziara ya kitaifa ya siku mbili ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Cuba iliyopangwa kufanyika kuanzia Novemba 6 hadi 8, 2024 imesogezwa mbele kutokana na kuchafuka kwa hali ya hewa iliyosababisha ndege kushindwa kutua.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameeleza hayo leo Alhamisi Novemba 7, 2024 katika taarifa kwa vyombo vya habari.

“Ziara hii imeahirishwa kutokana na taarifa ya awali ya kuchafuka kwa hali ya hewa na dhoruba inayoitwa Rafael kupiga katika visiwa vya Cuba na mji wa Havana na kusababisha viwanja vya ndege vyote kufungwa, kikiwemo kikuu cha cha Jose Mart.

“Kiwanja cha Jose Mart kimefungwa kwa saa zaidi ya 48, lakini napenda kuutarifu umma kwamba kimbunga kimeshapita na shughuli zimeanza kurejea katika hali yake ya kawaida,” amesema.

Kutokana na hilo, Balozi Kombo amesema ziara ya Rais Samia nchini humo itafanyika siku za usoni na itatolewa taarifa maalumu.

Kuhusu tamasha la Kiswahili duniani, Balozi Kombo amesema Rais Samia ameagiza liendelee kama kawaida likiongozwa na mawaziri waliokwenda nchini humo, akiwamo Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro.

Wengine ni Waziri wa Afya, Jenista Mhagama na Nassor Mazrui ambaye ni Waziri wa Afya wa Zanzibar. Pia wapo mawaziri wengine.

Related Posts