AKILI ZA KIJIWENI: Dirisha dogo ni mwenye nguvu mpishe

TUNATAMANI sana kuona dirisha dogo la usajili msimu huu lifike hapo mwezi Desemba kuanzia tarehe 15 ili hicho ambacho timu zinakipigia hesabu tuone kama kitatimia.

Kila timu inakuambia itatumia kipindi cha usajili wa dirisha dogo kuimarisha kikosi chake kwa kupunguza baadhi ya wachezaji na kuongeza kadhaa wapya ambao wataziimarisha katika mechi zitakazobakia za Ligi Kuu na mashindano mengine.

Kuna kitu tumekikumbuka hapa na tukaona tukikumbushe kwa timu kama njia ya kuziandaa kisaikolojia na maisha baada ya hilo dirisha dogo la usajili ambalo kila timu inatamani lifike ikijiaminisha litaleta ukombozi.

Dirisha dogo la usajili ni gumu kwa timu kuliko wengi wanavyofikiria kwa sababu kwanza wachezaji wazuri wengi wanakuwa na mikataba na timu zao na hatudhani kama itakuwa rahisi kwa timu kuwauza wachezaji wao wazuri kirahisi.

Hata wale ambao mikataba yao inaisha kipindi hicho cha dirisha dogo au itabakiza muda wa miezi sita baada ya kipindi hicho cha usajili na kuwepo na urahisi wa kuwapata, watataka hela nyingi ambazo ni timu chache tu ambazo zina mzigo wa kutosha wa kuwanasa wachezaji hao.

Maana yake kuna timu zitajikuta zikisubiria wachezaji ambao hawapati nafasi kwenye timu zao kutokana na viwango vyao kutokuwa vya kuvutia ili ziwachukue na kuwategemea wazinusuru.

Sasa unapomchukua mchezaji ambaye kwenye timu yake hapati nafasi kwa sababu ya kiwango na timu yako ndiyo unamtegemea huyo ili akutimizie malengo kwenye ligi, kinachofuata hapo kwa asilimia kubwa ni maumivu mwishoni mwa msimu.

Halafu kwa timu zilizo chini kwenye msimamo wa ligi tunaona zitateseka sana kwa sababu wachezaji wataogopa kujiunga nazo wakihofia zikishuka daraja nao wataonekana kama wamekuwa miongoni mwa vyanzo vya kuzishusha daraja.

Muda utaongea aiseeh! Lakini tunazikumbusha timu zisiweke matumaini kwa asilimia mia moja kwa dirisha dogo la usajili.

Related Posts