KIJIWENI hapa hatukushangaa kuona Pamba Jiji ikimchukua Felix Minziro kumrithi Goran Kopunovic baada ya kumtimua kama ambavyo Kagera Sugar walifanya kwa Melis Medo baada ya kuachana na Paul Nkata.
Hawa makocha historia yao ndiyo inafanya mimi na washkaji zangu hapa kuona kama timu hizo mbili zilipiga hesabu sahihi kwa kuwachukua makocha hao kwani huenda wana sifa zinazofanana.
Sifa ya kwanza inayofanana ya hao makocha ni mahusiano mazuri ambayo wanajua kuyajenga na wachezaji wao na wanaishi nao kama baba na watoto tofauti na baadhi ya makocha wenzao ambao hawana tabia kama zao.
Kocha kuwa na mahusiano mazuri na wachezaji wake ina faida kubwa kwa vile watakuwa wakicheza kwa kujituma kwa ajili yake ili wasimuangushe na kumlinda asiondolewe kwa vile wanaweza kuletewa kocha ambaye atatengeneza mpaka baina yao.
Jamaa hao wawili wana sifa yao nyingine ambayo ni kuishi kwenye timu kwa kuendana na mazingira yaliyopo pasipo kulazimisha kufanyika kwa marekebisho ya harakaharaka au kuziingiza timu gharama kwa kulazimisha zitimize kwa haraka mahitaji yao.
Mpira wetu unajuliakana na klabu nyingi zinakabiliwa na changanoto mbalimbali hasa za kiuchumi hivyo yako mahitaji ambayo hayawezi kutimizwa kwa haraka sasa hizi mara nyingi kwa makocha wasio na uelewa husababisha mgogoro mkubwa na viongozi wa timu ikiwa yale wanayotaka hayafanyiwi kazi mapema.
Minziro na Medo ni makocha ambao wamekuwa na hulka ya kutengeneza ukaribu na viongozi pamoja na mashabiki jambo ambalo hutengeneza umoja na mshikamano kwenye timu na kusaidia kupatikana kwa matokeo mazuri kwenye mashindano.
Tazama walizikuta timu hizo zikiwa katika nyakati ngumu lakini hawakuonyesha wasiwasi na badala yake wamekuwa wakiwapa imani viongozi, wachezaji na mashabiki inawezekana timu hizo zikafanya vizuri na kusalia kwenye ligi.
Mnaona wenyewe kilichotokea katika raundi za mwisho ambazo timu hizo zimecheza kabla ya ligi kusimama. Pamba imeshinda mabao 3-1 ugenini kwa Fountain Gate na Kagera Sugar imepata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji nyumbani.