WAKATI kiungo Sospeter Bajana amerejea uwanjani baada ya kuwa nje ya kwa muda mrefu kutokana na majeraha, huku akiingia ubaridi kwa kuhofia ubora wa wachezaji wanaocheza nafasi moja naye, kocha wa timu hiyo, Rachid Taoussi amesema mechi ni nyingi kila mmoja atacheza kulingana na ubora atakaoonyesha.
Bajana alikuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi kumi akiuguza jeraha la nyonga amerejea mazoezini na juzi akizungumza na Mwanaspoti alisema sio rahisi kurudi moja kwa moja kikosini kutokana na uwepo wa wachezaji ambao wanafanya vizuri sasa.
“Nilikuwa nje ya uwanja ni mwaka sasa siwezi nikarwejea moja kwa moja kucheza wakati kuna wachezaji wanafanya vizuri na wanaipambania timu kufikia malengo nina kazi ya kufanya kuhakikisha namshawishi kocha aniamini na kunipa nafasi,” alisema Bajana na kuongeza;
“Naheshimu ubora wa Adolf Mtasingwa na James Akaminko ambao wamekuwa wakicheza nafasi ambayo na mimi naicheza kila mmoja anafanya majukumu yake kwa ubora nafikiri ili kuweza kucheza natakiwa kufanya kazi ya ziada.”
Alisema kurudi kwake licha ya wapinzani wake kwenye nafasi kuwa bora kutaongeza chachu ya ushindani wa namba lakini bia ubora kwenye eneo hilo kwani ili mmoja acheze na mwingine akae benchi ni lazima ammoja awe imara zaidi ya mwingine.
Wakati Bajana akifunguka hayo, kwa upande wa Taoussi alisema wachezaji wengi eneo moja na wote wakiwa bora ni chachu ya mafanikio kwake kutokana na wingi wa mechi na ratiba ngumu ya mechi mfululizo itamsaidia kufanya mabadiliko ya mara kwa mara.
“Kuna mechi nyingi nafurahia wachezaji wengi wamerudi na wengine wanarudi kidogo kidogo naamini wote wakiwa kwenye ubora unaotakiwa tutakuwa na timu ambayo inaonyesha ushindani kwa wapinzani bila kuchoka kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara eneo hilo la kiungo,” alisema na kuongeza;
“Bajana bado ajawa fiti lakini tayari ameanza mazoezi ni mchezaji mzuri ataongeza kitu hasa ushindani katika eneo la kiungo mkabaji ambalo tayari wachezaji waliopo wameonyesha uwezo mkubwa.”
Wachezaji wengine wanaocheza eneo hilo ni Ever Meza ambaye hana namba kikosi cha kwanza na Yahya Zayd ambaye bado anaendelea kujiuguza jeraha la goti alilofanyiwa upasuaji.