KIPA wa Namungo FC, Beno Kakolanya ameuzungumzia ujio wa kocha mpya, Juma Mgunda katika kikosi hicho akisema umeongeza mzuka kwa wachezaji kwani nje ya taaluma yake anasimama kama baba na anaamini muda si mrefu timu hiyo itarejesha makali yaliyozoeleka Bara.
Kakolanya alisema amefanya kazi na Mgunda akiwa Simba na sasa amekutana tena Namungo, hivyo anamfahamu ni kocha wa aina gani na anayetaka kitu gani kutoka kwa mchezaji.
“Kocha Mgunda anatoa nafasi kwa kila mchezaji aonyeshe kiwango chake, hivyo inakuwa ni juu yetu kuyafanyia kazi yale tunayokuwa tunaelekezwa mazoezini, ili yalete matunda wakati wa kusaka pointi tatu,” alisema Kakolanya na kuongeza; “Ni kocha mzawa anayefahamu wachezaji vizuri, kuna wakati akiona haupo sawa anakuita na kukuweka sawa, kuhakikisha hauharibu kazi.”
Mbali na hilo, alizungumzia ushindani wa namba, unaofanya wawe bora na kumrahisishia kazi kocha, kufanya uchaguzi sahihi kulingana na mechi husika.
“Hadi sasa nimedaka mechi dhidi ya Fountain Gate, Singida Black Stars na Dodoma Jiji, naendelea kupambana katika mazoezi ili niendelee kupata nafasi ya kucheza,” alisema kipa huyo wa zamani wa Prisons, Yanga, Simba, Singida Fountain Gate na Taifa Stars.