Kwenye hotuba yake aloitoa kwenye bustani ya mawaridi nje ya majengo ya ikulu ya White House, Rais Biden amesema anajiandaa kuhakikisha ubadilishanaji madaraka kwenda kwa Donald Trump unafanyika kwa desturi zilizooleka nchini humo.
Ahadi hiyo ni tofatui kabisa na kile alichokifanya Trump mwaka 2020 ambapo alikataa kuyatambua matokeo yaliyompa ushindi Biden na kususia hata halfa ya kuapishwa kwake Januari 2021.
Matamshi ya Biden kuhusu kubadilishana madaraka kwa njia ya amani yalitolewa pia usiku wa Jumatano na makamu wake na aliyekuwa mgombea wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa rais wa Novemba 5, Kamala Harris, pale alipozungumza na wafuasi wake kukubali kushindwa uchaguzi.
Katika hotuba yake Biden pia amemkaribisha Trump kwa mazungumzo kwenye ikulu ya White House. Upande wa Trump ulikwishasema rais huyo mteule amepokea mwaliko huo na atatafuta siku ya kumtembelea rais Biden.
Hotuba ya Biden ilijikita vilevile kutoa mwito wa umoja wa kitaifa akiwahimiza Wamarekani kuwa na mshikamano bila kujali upande walioupigia kura katika uchaguzi wa siku ya Jumanne.
Biden ajaribu kutuliza hasira za baadhi ya Wademocrat
Ama kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais, Biden ametumia hotuba yake kuwarai wanachama wa chama chake cha Democratic kutokata tamaa baada ya mgombea wao Kamala Harris kupoteza kinyanganyiro cha urais kwa Donald Trump.
Biden amewakumbusha kwamba “kupoteza uchaguzi hakuna maana ya wao kuwa wameshindwa”. Mamtashi yake yumkini yalikuwa na lengo la kutuliza hamkani ndani ya chama chake katikati ya kiwingu cha lawama zinazoelekezwa kwake.
Baadhi ya Wademocrats wanamlaumu Biden kuwa sababu ya kushindwa kwa Harris wakisema alipaswa kuchukua uamuzi wa mapema wa kuachana na mipango ya kuwania kuchaguliwa tena.
Biden alijiondoa kwenye mbio za kuwania tena urais mwezi Julai kutokana na shinikizo baada ya kufanya vibaya katika mdahalo na Trump mnamo mwezi Juni.
Wademocrats kadhaa wanaamini alikawia mno kuchukua uamuzi huo na hilo limekigharimu chama chao kwenye uchaguzi. Ushindi wa Trumo dhidi ya Harris tayari umebadili upepo wa kisiasa ndani ya Marekani na ulimwenguni.
Putin na Xi wamtumia Trump salamu za pongezi kwa ushindi wa uchaguzi
Viongozi wa dunia wameendelea kumtumia Trump salamu za pongezi na hapo jana aliendelea kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na viongozi kadhaa wa mataifa washirika.
Hapo jana pia Rais Vladimir Putin wa Urusi alimtumia Trump salamu za pongezi na kusema yuko tayari kufanya naye mazungumzo.
Hapo jana Trump alikimbia kituo cha habari cha NBC kwamba bado hajazungumza na Putin tangu aliposhinda uchaguzi lakini anatumai atazungumza naye.
Mamtashi yake yanaashiria mabadiliko makubwa mjini Washington kutoka msimamo wa Biden wa kumtenga Putin tangu Moscow ilipotuma vikosi vyake kuingia Ukraine mwaka 2022.
Tangu wakati huo utawala wa Biden umekuwa muungaji mkono mkubwa kijeshi wa Ukraine katika vita vinavyoendelea.
Trump amekuwa mkosoaji mkubwa wa misaada hiyo ya kijeshi kwa Ukraine na amesema atashinikiza kupatikane mkataba wa amani ili kumaliza vita vya Ukraine, pendekezo ambalo watawala mjini Kyiv wamelipokea kwa mashaka.
Mbali ya Putin, Rais Xi Jinping wa China naye alituma salamu zake za pongezi kwa Trump akimrai rais huyo mteule kufanya kazi kwa dhamira ya kuzipatanisha nchi hizo mbili ambazo mahusiano yake yamedorora.
Katika hatua nyingine Trump ameanza kuisuka serikali yake kwa kumteua aliyekuwa meneja wake wa kampeni Susan Wiles kuwa mkuu wa utumishi wa Ikulu.
Trump ataapishwa mnamo Januari mwakani na inatazamiwa ataendelea wiki hii kuteua wale watakaomsaidia kazi atakapochukua hatamu za uongozi.