Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango anatarajia kuondoka nchini leo Novemba 8, 2024 kuelekea Baku nchini Azerbaijan, kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa 29 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29).
Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari leo na Msaidizi wa Makamu wa Rais – Habari, Franco Singaile imesema mkutano huo unatarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 11 -22, 2024 jijini humo.
“Akiwa nchini Azerbaijan, Makamu wa Rais anatarajiwa kuhutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa COP-29, ambapo ataeleza msimamo na jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Vilevile Makamu wa Rais atashiriki mikutano ya pembeni ikiwa ni pamoja na ule utakaojadili hatua zinazopaswa kuchukuliwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, fursa za nishati safi ya kupikia na biashara ya kaboni.
“Pia, atashiriki kwenye mkutano utakaojadili namna ya kuongeza uwekezaji kwenye uchumi wa buluu katika maeneo ya bahari na maziwa makuu, kama hatua ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.”
Sambamba na ushiriki katika mkutano wa COP 29, taarifa hiyo pia imesema kuwa Makamu wa Rais anatarajiwa kufanya mikutano ya uwili na wakuu wa nchi na serikali pamoja na viongozi wa mashirika ya kimataifa wanaoshiriki mkutano huo ili kujadili fursa mbalimbali za maendeleo kwa manufaa ya pande zote mbili.
Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais ameambatana na viongozi pamoja na wataalamu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.