Fadlu aleta kiungo fundi kutoka Morocco

SIMBA imekamilisha jumla ya mechi 10 za Ligi Kuu Bara ikikusanya pointi 25 na mabao 21, huku ikiruhusu mabao matatu tu hadi sasa wakati ligi hiyo ikienda mapumziko ya wiki mbili, lakini kuna kitu ambacho kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids ameamua kukifanya katika kuimarisha kikosi hicho dirisha dogo.

Kwa wanaokumbuka Mwanaspoti liliwahabarisha Fadlu amesema anahitaji mashine tatu za maana, winga ambaye tayari wamemsainisha Ellie Mpanzu kutoka DR Congo, lakini anahitaji pia beki wa kati ya maana na kiungo mshambuliaji ambaye atakuwa na kazi ya kuwalisha wenzake ili timu ifunge mabao zaidi.

Sasa kwa taarifa yako, tayari Fadlu ameshalipeleka mezani jina la kiungo fundi wa mpira kutoka timu aliyokuwa akiinoa ya Raja Casablanca ya Morocco, Abdelhay Forsy aliyeanza mazungumzo ili dirisha dogo litakalofunguliwa mwezi ujao na kufungwa Januari mwakani atue asaidieane na Jean Ahoua.

Kiungo mshambuliaji huyo kwa sasa anakipiga CA Renaissance Zemamra pia ya Morocco iliyomsajili kutoka Raja wakati Fadlu akiinoa kama kocha msaidizi na inaelezwa mazungumzo yapo hatua nzuri na muda wowote ataibukia Msimbazi ili kuuungana na kocha huyo ambaye amegeuka kipenzi cha Wanasimba.

Rekodi zinaonyesha Abdelhay aliyekuwa akiingia na kutoka Raja na Zemamra, amemvutia Fadlu kwa uwezo wake uwanjani na amewaambia mabosi wa Msimbazi, jamaa akitua kila kitu kitakuwa chepesi na Ahoua atakuwa na mtu sahihi wa kusaidiana naye licha ya uwezo pia wa kucheza kama winga.

Katika mechi tano kati ya tisa ilizoichezea timu hiyo katika Ligi Kuu ya Morocco, Botola Pro, ameasisti mara tatu na inaelezwa ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kutoa pasi, kutengeneza mashambulizi na hata kufunga, kitu ambacho Fadlu analia nacho kwa sasa Msimbazi.

MPYA01
MPYA01

Forsy ana uzoefu mkubwa, akiwa amewahi kuichezea klabu kubwa ya Morocco, Raja Casablanca na anajulikana kwa umahiri wake wa kutumia miguu yote miwili.

Mbali na kumudu nafasi ya kiungo mchezeshaji, ana uwezo wa kucheza kama winga wa kushoto au kulia, jambo linaloweza kumfanya kuwa na faida zaidi kwa kocha Fadlu anayetaka kubadilisha safu ya mashambulizi ya Simba iwe yenye kasi na uwezo zaidi wa kufunga.

Baada ya kupoteza dhidi ya Yanga, Oktoba 19, Fadlu alieleza Simba inahitaji maboresho ikiwemo kiungo, mwenye uwezo wa kutoa pasi za mwisho kwa usahihi na anayeweza kuchangia moja kwa moja katika ujenzi wa mashambulizi.

Forsy anatambulika kwa mtazamo wa kiufundi na anaweza kutoa pasi sahihi za mwisho na anajua jinsi ya kuingiza mipira kwenye eneo hatari kwa wapinzani.

Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani ya Simba, jina la Abdelhay Forsy limekuwa katika orodha ya wachezaji wanaowindwa na klabu hiyo tangu enzi za kocha Abdelhak Benchikha na kurejeshwa tena kwa mazungumzo kwa hitaji la Fadlu ni kuonyesha wanamfuatilia tangu kipindi hicho.

“Simba wako siriazi na mchezaji huyo. Anaonekana kuwa chaguo sahihi la kuongeza nguvu kwenye kikosi. Forsy ni kiungo mwenye jicho la pasi za mwisho na uwezo wa kiufundi wa kuongoza mashambulizi,” kilisema chanzo hicho cha ndani.

Ingawa Simba bado haijathibitisha rasmi mazungumzo na mchezaji huyo, lakini chanzo makini kutoka klabuni hapo kimesema uongozi umeanza kufanya mazungumzo ya kina na kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26 ili kupata saini ya kiungo huyo.

MP
MP

Katika hatua nyingine, mara baada ya Simba kumalizana na mechi za Ligi Kuu juzi kwa kuifumua KMC mabao 4-0, benchi la ufundi chini ya Fadlu Davids, limehamishia nguvu na akili kwenye mechi za CAF ikijiandaa kukabiliana na Bravos d Maquis ya Angola katika mechi ya Kundi A ya Kombe la Shirikisho.

Mbali na Bravos, kikosi cha Simba pia kimepangwa na CS Sfaxien ya Tunisia na CS Constantine ya Algeris na Fadlu tayari amejifungia ndani na wasaidizi wa benchi la ufundi la timu hiyo ili kuanza hesabu mpya na namna gani wataingia kwenye mechi za hatua ya makundi.

Simba haitakuwa na mchezo wowote wa ligi sasa hadi itakapoanza mechi ya kwanza ya makundi ya shirikisho itakapoanzia nyumbani Novemba 27..

Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu amechekelea mapumziko ya mechi za kalenda ya Fifa kwa timu za taifa huku Wekundu hao wakiondolewa mchezo dhidi ya Pamba Jiji uliokuwa upigwe Novemba 21.

Fadlu alisema muda huo wao kama makocha watautumia vizuri kujipanga sawasawa dhidi ya Bravos Maquis kwa kutafuta kila taarifa za ubora wao.

Kocha huyo alisema mapumziko hayo pia yatawasaidia wachezaji wake kujiandaa kwa utulivu huku pia mastaa wake watakaokwenda timu za taifa kupata muda mzuri wa kurejea na wao kujiandaa wakiwa kama timu.

“Tulilazimika kufanya mzunguko wa wachezaji ili kila mmoja apate muda wa kupumzika sawasawa ratiba ilikuwa ngumu sana lakini nimeona kuna mechi imeondolewa ya ligi hii itatupa nafasi nzuri kujaindaa na mechi ya kwanza ya makundi,” alisema Fadlu na kuongeza;.

“Akili yetu sasa itajikita huko kwenye Shirikisho, kwetu sisi makocha tutakuwa na muda wa kujua kila taarifa za wapinzani wetu juu ya ubora wao lakini huku tukiendelea na maandalizi taratibu.

Aidha Fadlu aliongeza kuwa katika maandalizi yao hayo watahakikisha wanaongeza kasi ya kutumia nafasi kwani mechi hizo za CAF hazizalishi nafasi nyingi za kufunga.

“Tunatakiwa kuanza vizuri, ikiwezekana kwa ushindi mkubwa na bila kuruhusu bao, kitu muhimu hapa ni sisi kutumia nafasi tutakazotengeneza kwa wingi hizi ni mechi ambazo hazina nafasi nyingi.

“Angalia mechi iliyopita (dhidi ya KMC) sawa, tulishinda vizuri lakini kipindi cha kwanza tulistahili kupata mabao hata matatu lakini hatukuwa kwenye utulivu mkubwa hili ni lazima tulifanyie kazi ndani ya huu muda.”

Related Posts