Kisukari kinaweza kuathiri si tu afya ya mwili, bali pia afya ya akili. Utafiti mbalimbali umeonesha kwamba kuna uhusiano mkubwa kati ya kisukari na matatizo ya afya ya akili kama vile upweke, wasiwasi na kupoteza kumbukumbu.
Utafiti uliochapishwa katika jarida la Diabetes Care linalochapishwa na Chama cha Kitaifa cha Kisukari la Marekani, umeonesha watu wenye kisukari wana uwezekano mkubwa wa kuwa na matatizo ya utambuzi, kama vile ugumu wa kukumbuka mambo au kufikiri kwa uwazi.
Kisukari huchangia matatizo ya afya ya akili kwa njia kadhaa, ikiwamo mabadiliko katika viwango vya sukari ambayo huathiri ubongo kwenye ufanyaji wake wa kazi.
Kiwango cha juu au cha chini cha sukari kinaweza kusababisha hali ya kuchanganyikiwa, uchovu na hata shida za kumbukumbu, kuwa na hali ya wasiwasi na hali ya kuwa mnyonge, kisukari kinaweza kuathiri mfumo wa neva.
Utafiti umeonesha watu wenye kisukari wana uwezekano mkubwa wa kupata matatizo ya neva, yanayoweza kuathiri uwezo wa ubongo kufanya kazi vizuri.
Hali hii inachangia matatizo kama vile uwezo hafifu katika kuzingatia, kudhibiti hisia na matatizo katika utendaji wa kila siku.
Ugonjwa wa kisukari unaleta changamoto kubwa za kisaikolojia. Watu wengi wenye kisukari wanakabiliwa na hisia za huzuni, upweke, wasiwasi na mfadhaiko, hivyo kuathiri uwezo wa mtu kujiendesha na kuishi maisha ya kawaida.
Athari ya kisukari katika afya ya akili huweza kumfanya mgonjwa kushindwa kufuata mpango mzuri wa lishe au kutumia dawa kama inavyopaswa.
Hali hii inaweza kuleta athari mbaya zaidi kwenye udhibiti wa sukari na hivyo kuanzisha mzunguko mbaya wa matatizo ya mwili na akili.
Ili kukabiliana na athari za kisukari katika afya ya akili, ni muhimu kwa watu wenye kisukari kuchukua hatua za kuimarisha afya zao za akili. Mosi, kujifunza kuhusu ugonjwa wenyewe wa kisukari, elimu juu ya kisukari inaweza kusaidia kuelewa hali halisi ya kuishi na kisukari.
Kujua dalili za kisukari na jinsi ya kudhibiti viwango vya sukari kunaweza kupunguza hofu na wasiwasi.
Pili, mafunzo ya usimamizi wa msongo wa mawazo kama vile kufanya zoezi la yoga, kunaweza kusaidia katika kupunguza viwango vya mfadhaiko na msongo wa mawazo.
Tatu, kuwasiliana na wataalamu wa afya, ni muhimu kuwa na uhusiano mzuri na madaktari na wataalamu wa afya ya akili.
Msaada wa kitaaluma unaweza kusaidia kujiandaa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na kisukari.