LEKASHINGO ATAKA USHIRIKIANO TUME YA MADINI

MWENYEKITI Mpya wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo ameahidi kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na ushirikiano mkubwa na watumishi na wadau wote wa Sekta ya Madini.

Lekashingo ametoa ahadi hiyo leo Novemba 8, 2024 akiripoti ofisi za Tume ya Madini zilizopo Kikuyu, jijini Dodoma tayari kuanza majukumu yake mapya baada ya kuteuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Oktoba 31, 2024 kuwa Mwenyekiti mpya wa Kamisheni ya Tume ya Madini akichukua nafasi ya Profesa Indris Kikula ambaye muda wake umemalizika.

Amesema, Sekta ya Madini ina nafasi kubwa ya kubadili mtazamo wa nchi, kubadili maisha ya watanzania pia kubadili uchumi wa nchi.

“Hivyo ni muhimu sisi watumishi wa Tume ya Madini kuhakikisha kwamba tunaangalia mifumo yetu kama inastahili, kuhakikisha mazingira maeneo ya migodini yanatuzwa, kuhakikisha jamii inashirikishwa, nimefurahi kusikia wachimbaji wadogo wanapewa umuhimu unaostahili,”amesema Lekashingo.

Aidha, amesema amefarijika kurudi Tume ya Madini kama Mwenyekiti wa Kamisheni na kumshukuru Rais Dkt. Samia kwa kumuamini na kumpa jukumu hilo muhimu la kuongoza Tume ya Madini.

“Pia nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Madini Anthony Mavunde, Katibu Mkuu Mhandisi Yahya Samamba na viongozi wote kwa kuwa nami katika safari hii,”amesema Lekashingo na kuongeza

“Wengi mnafahamu nimepata bahati ya kutumika kama Kamishna wa Tume ya Madini na ninaelewa madini yana umuhimu mkubwa katika uchumi wetu hivyo ni jukumu letu kupitia Tume kuhakikisha Wizara inafanya vizuri kutunza mazingira na madini yananufaisha watanzania na uchumi wa nchi yetu,”amesisitiza.

Awali, akitoa taarifa ya Tume ya Madini Kaimu Mkurugenzi wa Leseni na Tehama, Mhandisi Aziza Swedi kwa niaba ya Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo, amesema Tume ya Madini imeendelea kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na madini ambapo kiwango cha makusanyo ya maduhuli ya Serikali kilipanda kutoka Shilingi Bilioni 346.275 zilizokusanywa Mwaka 2018/2019 na kufikia Shilingi Bilioni 753.18 Mwaka 2023/2024.

Aidha, amesema katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, Tume ya Madini imepangiwa kukusanya jumla ya Shilingi Bilioni 999. 998, ambapo hadi kufikia Oktoba 31, 2024 Tume imefanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi Bilioni 354. 613 sawa na asilimia 35.46 ya lengo la mwaka. Makusanyo ya mwezi Oktoba ni Shilingi Bilioni 96.724 sawa na asilimia 116.07 ya lengo la mwezi Oktoba 2024.

Mhandisi Swedi amesema, mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeimarika na kufikia asilimia 9.0 Mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 5.1 kwa mwaka 2018. Aidha, ukuaji wa Sekta ya Madini uliimarika na kufikia asilimia 11.3 kwa Mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 5.1 Mwaka 2018.

 

Related Posts