Ligi ya Championship imenoga | Mwanaspoti

UHONDO wa Ligi ya Championship unaendelea kushika kasi ambapo baada ya jana kupigwa michezo mitatu, kesho itapigwa mingine mitatu kwenye viwanja mbalimbali, ili kuzisaka pointi tatu muhimu za kusaka tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Mchezo wa mapema saa 8:00 mchana utapigwa Uwanja wa Jamhuri Morogoro ambapo wenyeji African Sports ambayo haijashinda hadi sasa kati ya michezo saba iliyocheza, itaikaribisha Biashara United iliyochapwa mabao 2-0, dhidi ya Stand United.

Saa 10:00 jioni itapigwa michezo miwili ambapo Bigman FC iliyotoka suluhu na Mbeya Kwanza itakuwa kwenye Uwanja wa Ilulu Lindi kucheza na Maafande wa Polisi Tanzania wenye kumbukumbu mbaya ya kuchapwa mechi ya mwisho mabao 2-1 na Geita Gold.

TMA iliyochapwa na majirani zao wa Mbuni mchezo uliopita kwa bao 1-0, itakuwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha kucheza dhidi ya Maafande wa Green Warriors watakaoingia na morali baada ya kuichapa Cosmopolitan mechi iliyopita bao 1-0.

Uhondo wa Ligi hiyo utaendelea tena kesho Jumapili kwa michezo miwili kupigwa ambapo Transit Camp iliyotoka sare ya 2-2 na Kiluvya United itakuwa Uwanja wa Meja Isamuhyo Mbweni kucheza na Songea United iliyofungana 1-1, dhidi ya Mbeya City.

Mchezo wa kumalizia wikiendi utapigwa kwenye Uwanja wa Mabatini Pwani ambapo wenyeji Kiluvya United ambayo haijaonja ladha ya ushindi katika michezo saba iliyocheza, itaikaribisha Mbeya City iliyotoka sare na Songea United ya bao 1-1.

Akizungumzia mwenendo wa Ligi hiyo Kocha Mkuu wa African Sports, Kessy Abdallah alisema licha ya kuanza vibaya msimu huu ila wao kama benchi la ufundi na wachezaji bado hawajakata tamaa, wakiamini ni kipindi cha mpito ambacho wanapitia kwa sasa.

Related Posts