Dodoma. “Kwenye biashara yangu debe moja la mkaa naweza kutumia siku tatu nikitumia majiko haya lakini yake ya zamani (majiko ya bati, chuma) nilikuwa natumia debe kwa siku moja tu,” anasema Dosa Manaa mamalishe wa Kijiji cha Kolo wilayani Kondoa mkoani Dodoma.
Dosa anasema ameamua kuacha kutumia majiko ya bati na kuamia majiko ya banifu yanayotengenezwa kwa udongo.
“Yale mengine (ya bati) yanatumia mkaa mwingi sana kwa sababu yakishawaka yamewaka lakini haya ukishaweka mkaa baadaye unaweza kuweka pembeni na kisha kuendelea kupika bila mkaa kwa sababu lina udongo,” anasema.
Anatoa mfano anapopika wali, akibandika jikoni na kuchemka tu, anatoa moto wote na wali unaiva kabla ya kupoa kwa jiko.
Huku akionyesha majiko yake makubwa matatu yaliyotengenezwa kwa udongo, anasema ubunifu huo umemsaidia kupunguza matumizi ya mkaa aliyokuwa yakitumia Sh2, 000 kwa siku hadi Sh700 anayotumia sasa.
Dosa hakupata majiko haya mbali, yanapatikana huko huko kwenye kijiji chao cha Kolo na kwa wabunifu wa Asili Group.
Mwenyekiti wa Asili Group, Hawa Chora anasema kikundi hicho kilichoanzishwa mwaka 2012 na kukisajili mwaka 2019 kikiwa na wanachama sita.
“Tulilenga katika kuwasaidia wanawake kupata majiko ambayo yatapunguza matumizi ya mkaa na kupunguza gharama za nishati hiyo na ukataji wa miti,” anasema.
Anasema alipopata wazo la kuanzisha kikundi alikwenda kwa Aisha Bwitu (Katibu wa Kikundi) na kumshauri kuhusu kuanzisha kikundi kwa kuwa Serikali husaidia watu kupitia vikundi vya uzalishaji mali.
Anasema baada ya ushawishi huo waliongezeka wanawake na mwanamume mmoja hadi kufikia 19.
“Tulianza na mradi wa uoteshaji wa miche lakini baadaye tuliona tuongeze ubunifu na kuja na wazo la majiko haya yatakayopunguza matumizi ya mkaa,” anasema.
Anasema walianza kwenda kuchukua udongo wa mfinyanzi katika kijiji jirani cha Mnenia kwa ajili ya kuanza kutengeneza majiko hayo banifu na mwanamume alikuwa akiwasaidia katika kuchimba udongo huo kisha kuleta kwenye eneo hilo kwa kutumia punda.
Hawa anasema bei ya majiko inaanzia Sh2,000 hadi Sh5, 000 000 na kwa mwezi mmoja wanatengeneza wastani wa majiko 20 kulingana na mahitaji ya soko.
Mwanakikundi Jaha Imeda anasema wakishaleta udongo husaga kwa kutumia jiwe kisha kuloweka kwenye maji.
Anasema baada ya kukoroga na kulainika vizuri huuchukua mkononi na kuunda jiko banifu na kisha kulitoboa katikati ili liweze kupitisha hewa.
“Tunayaweka kwanza ili yakauke kabla ya kuyachoma moto ili kuyaweka uimara. Bado tunatumia moto wa kuni kwa ajili ya kuyachoma. Na yakiwa tayari yanabadilika rangi,” anasema.
Anasema kwa siku wanaweza kutengeneza majiko hata 20 kama wakiianza kazi hiyo asubuhi, lakini utengezaji hutegemea zaidi uhitaji.
Mjumbe wa Asili Group, Salama Sachu anasema licha ya mafanikio ya kujenga ofisi yao, wanakabiliwa na changamoto ya usafiri wa kuchukua udongo umbali wa kilomita nane, wakitumia punda.
Pia, wanakosa vifaa vya kisasa kutengeneza majiko, hivyo hutumia mikono, jambo linalochelewesha uzalishaji na kupunguza ufanisi.
“Tunaiomba Serikali itusaidie vifaa ambavyo vitatusaidia kutengeneza majiko haya ili tuweze kutengeneza mengi zaidi kwa muda mchache,” anasema Salama.
Aisha Bwitu anasema lengo la ubunifu huo ni kuhakikisha jamii inatumia majiko banifu yanayopunguza gharama za maisha na athari kwa mazingira.
“Majiko hayo yanatumia mkaa mdogo, hivyo kusaidia kuokoa pesa na kupunguza uharibifu wa mazingira kwa kutokata miti. Ubunifu huu unasaidia pia kuokoa muda wa kupika,”anasema Aisha.
Kuhusu uimara wa majiko, mamalishe Dosa Manaa anasema inategemea matunzo yake, lakini kwa yeye pamoja na hekaheka za biashara yanatumia angalau miaka mitatu.
Dosa anawashauri watu kutumia majiko hayo kwa kuwa yatawasaidia katika kupunguza gharama za ununuzi wa mkaa huku wakitunza mazingira.
Mmoja wa mafundi wa majiko banifu katika kikundi kingine cha Tumaini kilichopo Kondoa Mjini, Shabani Mazige anasema jiko banifu linatofauti kubwa na yale majiko ya mabati na vyuma.
“Majiko banifu yanachukua asilimia 50 tu ya mkaa unaotumika kwenye majiko yanayotengenezwa na mabati na vyuma na ni kwa sababu ya udongo unaoweka katika majiko banifu unasaidia kuhifadhi moto,” anasema Mazige.
Anasema bei kubwa ya majiko hayo ambayo yanauzwa kati ya Sh7, 000 na Sh20, 000 inatokana na mlolongo wa utengenezaji wake ambao ni mrefu ukilinganisha na yale ya bati na vyuma.
Hata hivyo, majiko hayo banifu yanayotengenezwa na kikundi hicho chenye watu wanne ni tofauti na yale ya Asili Group kwa kuwa huongezwa bati kwa kuzungushiwa juu ya udongo.
“Majiko bunifu yana bei kubwa lakini hiyo ni kutokana na utengenezaji wake una mlolongo mkubwa kwa kuwa inatakiwa kuchukua udongo kabla ya kuufinyanga na kisha kuuchoma katika tanuru tofauti na majiko ya bati ambayo kazi yake huishia katika bati,” anasema.
Anasema kwa wastani wanatengeneza majiko 50 kwa mwezi ambayo hayakidhi mahitaji ya soko ambalo linahitaji majiko hayo mengi wasiyoweza kuyatengeneza.
Anasema soko la majiko yao liko jijini Dar es Salaam, Dodoma na nchi jirani ya Kenya na wapo wafanyabiashara wanaoyanunua kwa ajili ya kuyasafirisha.
“Lengo ni kukuza matumizi ya majiko banifu na kuongeza uzalishaji ili kupunguza matumizi ya misitu. Angalau kila kona ya nchi kuwe na wazalishaji wa majiko haya,” anasema.
Anawashauri Watanzania kuendelea kutumia majiko hayo ili kuepusha matumizi makubwa ya miti katika kutengeneza mkaa.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu teknolojia za nishati, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule anasema Serikali itaendelea kuweka vivutio kwa wazalishaji na wasambazaji wa teknolojia za nishati safi na salama ya kupikia ili kupunguza utegemezi wa mkaa na kuni, hasa maeneo ya vijijini.
“Mpango huu unalenga kupunguza athari za mazingira na afya, huku Serikali ikiongeza wigo wa upatikanaji wa majiko hayo kwa gharama nafuu,”anasema Rosemary.
Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) Advera Mwijage anasema majiko hayo yanapunguza gharama kwa watumiaji na kusaidia kuhifadhi mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti ovyo.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.