KIPA wa Tabora United, Hussein Masalanga amefichua siri iliyompa mafanikio ya kuidaka penalti iliyopigwa na kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki wakati Yanga ikifa 3-1 aliyoitaja ni kujua anapiga upande gani, baada ya kumfuatilia baadhi ya mechi za Ligi Kuu na michuano ya CAF.
Alisema baada ya kumuona Aziz Ki ndiye anajiandaa kupiga mpira alijipa asilimia kubwa ya kuudaka, kwani penalti zake nyingi anazipiga upande wa kulia.
“Asilimia kubwa ya penalti anazopiga Aziz Ki ni upande wa kulia, nikajiandaa kudaka kwenda upande huo na kweli nikafanikiwa, nadhani makipa wengi nitakuwa nimewafumbua macho kuliona hilo, sio kwa Aziz Ki pekee hata kwa wengine, lazima tujiongeze kuwasoma, ingawa najua watabadilika na kuanza kupiga tofauti,” alisema Masalanga na kuongeza; “Kwa nafasi yangu ya kipa, nalazimika kufuatilia washambuliaji aina ya mikimbio yao, mipira wanayopiga ni ya aina gani, nje na hapo unaweza ukafungwa mabao mengi.”
Alizungumzia mechi hiyo, aliyodaka dakika 45 za kipindi cha kwanza baada ya kuumia akaingia Haroun Mandanda, alisema mashambulizi ya Yanga ni hatari wakianzia pembeni.
“Yanga ilikuwa inashambulia kuanzia pembeni, kisha wanaingia ndani, safu yao yote ya mbele ilikuwa ni hatari, lakini dakika 90 zikaamua tushinde mchezo huo,” alisema.
Mbali na hayo, Masalanga alisema atakaa nje wiki mbili, ili kuuguza majeraha ya goti, aliyoumia katika mchezo huo.
“Baada ya kwenda hospital waliniambia goti lilisogea pembeni, ikabidi walirudishe sehemu yake, kisha wakanipa dawa ya maumivu na nimeambiwa nikae nje wiki mbili. Kuumia kwangu kulitokana na kuwania mpira wa juu na Kennedy Musonda ambapo akatua juu ya goti langu, lakini baadaye akaja kunipa pole maana ilikuwa ni presha ya mchezo.”