KIUNGO mshambuliaji mkongwe wa Namungo, Jacob Massawe amemvulia kofia kiungo wa Coastal Union, Charles Semfuko, akisema ni mmoja ya wachezaji chipukizi wenye uwezo mkubwa na kama akiendelea na moto huo atafika mbali katika maisha ya soka kwani boli analijua.
Massawe alisema msimu uliopita viliibuka vipaji vya chipukizi wengi, ila kwa bahati mbaya hakuwaona walioendeleza moto wakimentaini viwango vyao, hivyo anamsisitiza Semfuko kukaza buti ili awe tunu kwa taifa.
“Naumia kuona chipukizi wanakosa mwendelezo, wao ndio wanaotegemewa kwa kikosi cha Stars, hivyo lazima wawekewe mikakati ya kuona wanafanya vizuri, wakati mwingine najiuliza shida ni wasimamizi wanakuwa wanajali maslahi pekee, ama kuna changamoto nyingine inayowakwamisha,” alisema Massawe na kuongeza;
“Wachezaji chipukizi wanapaswa kutambua, wanapoingia katika soka,inahitaji nidhamu, kujituma kwa bidii na kulinda viwango vyao, kujitenga na vitu nje ya uwanja, ndipo wanaweza wakafika mbali.
Semfuko msimu uliopita alimaliza na mabao manne, ambapo msimu huu tayari anamiliki bao moja alilofunga dhidi ya Kagera Sugar, hivyo ameshauriwa kuzingatia miiko ya soka, ili aje afaidi matunda ya kipaji chake.
Mbali na hilo, Massawe kazungumzia ugumu wa msimu huu, kuuona ni wa tofauti na mingine ambayo ameiona tangu aanze kucheza Ligi Kuu.
“Ugumu unaibua ubora wa viwango vya wachezaji, kwangu mimi naona tunapiga hatua kubwa sana katika soka, ligi iliopita nilimaliza na mabao manne na asisti nne, kwa sasa nina mabao mawili na asisti moja, naamini nitafanya vizuri zaidi,” alisema mkongwe huyo aliyewahi kukipiga Stand United, Ndanda, Toto Africans, Gwambina na African Lyon.