Takukuru Arusha yazungumzia ilivyotimuliwa na Chadema

Arusha. Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema kuwatimua maofisa watatu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), taasisi hiyo imetoa taarifa ikisema hatua ya chama hicho imekipogtezea fursa ya kupata elimu ya kuzuia rushwa.

Lema aliwatimua maofisa hao katika semina ya wagombea wa uenyekiti wa mitaa wa Chadema iliyofanyika Novemba 7, 2024, jijini Arusha, akieleza kuwa maofisa hao hawakuwa wajumbe halali wa mkutano huo.

Akizungumzia tukio hilo leo, Novemba 8, 2024, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo amesema maofisa hao walihudhuria mkutano huo baada ya kupokea mwaliko wa maandishi kutoka kwa uongozi wa Chadema Wilaya ya Arusha Mjini.

“Moja ya majukumu ya Takukuru ni kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa. Tulipopata mwaliko, tuliona uhitaji na tukajiratibu kutuma maofisa wetu kwenye mkutano huo wa ndani,” amesema Ngailo.

Ngailo ameongeza kuwa hadi sasa bado hawajafahamu sababu za kufukuzwa, lakini amesisitiza kuwa hatua hiyo haitakatisha tamaa taasisi hiyo kuendelea kutimiza wajibu wake.

“Chadema wamejikosesha fursa ya kupata elimu ya rushwa, hasa kuelekea kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa. Wamepoteza nafasi ya kupata ufafanuzi kuhusu madai yao ya majina hewa kwenye daftari la wapiga kura. Hata hivyo, elimu itaendelea kutolewa kwa watu wengine na wakati mwingine kupitia vyombo vya habari,” amesema.

Kwa upande wake, Lema ambaye aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, amesema aliwaondoa maofisa hao kwa sababu hawakuwa na mwaliko rasmi, na hakuwa na taarifa kuhusu uwepo wao kabla ya mkutano huo.

“Mkutano ulikuwa wangu, uliandaliwa kwa ajili ya kuwapa mwongozo wajumbe wangu wanaojiandaa kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa. Kukutana na sura mpya pale kulifanya nifanye uamuzi wa kuwatimua,” amesema Lema.

Kuhusu barua inayoelezwa kuwa iliwaalika maofisa wa Takukuru, Lema amesema hana taarifa ya barua hiyo na wameanzisha uchunguzi wa kuthibitisha madai hayo.

“Hakuna barua, ni taarifa zisizo na ukweli. Takukuru ndio waliomba kuja, na nimewaonya watendaji wangu kanda nzima kwamba ni marufuku kuzialika taasisi za serikali kwenye mikutano yangu bila mimi kufahamishwa,” amesema.

Katibu wa Chadema Wilaya ya Arusha Mjini, Francia Chuma, ambaye anadaiwa kuandika barua hiyo, amesema kwa sasa hawezi kuzungumzia sakata hilo na ameomba muda wa kutulia kabla ya kutoa taarifa zaidi.

“Naomba muda, nitazungumza nitakapotulia,” amesema.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Arusha Mjini, Rick Moiro amesema hana taarifa ya ofisi yake kuandika barua hiyo ya mwaliko. Ameeleza kuwa mkutano huo ulikuwa wa ndani na ulipaswa kuhudhuriwa na wajumbe pekee.

“Sikuwa na taarifa kuwa kuna maofisa wa Takukuru kwenye mkutano, ila najua katibu wetu aliwasilisha malalamiko Takukuru jana kuhusu madai ya baadhi ya wagombea kutoka chama kingine kuwashawishi wajumbe wetu kujiondoa kwenye kinyang’anyiro,” amesema Moiro.

Related Posts