Takukuru kuikabili rushwa uchaguzi serikali za mitaa

Dar es Salaam. Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kinondoni imepanga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari za rushwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa kama sehemu ya mikakati yake ya kuanzia Oktoba hadi Desemba 2024.

Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024, ambapo wananchi wameshaanza kujiandikisha, na kwa sasa hatua ya uteuzi wa wagombea inaendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa, Novemba 8, 2024, Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kinondoni, Christian Nyakizee amesema miongoni mwa mikakati yao ni kuwahusisha vijana katika mapambano dhidi ya rushwa kabla na baada ya uchaguzi.

Nyakizee ameeleza kuwa rushwa katika uchaguzi hupelekea kuchaguliwa viongozi wasio waadilifu, ambao mara nyingi hutumia muda wao kulipia gharama za kampeni badala ya kuleta maendeleo kwa wananchi.

Nyakizee amesema Takukuru kupitia programu yake ya Takukuru Rafiki inawafikia wananchi kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na semina, mijadala ya wazi, mikutano ya hadhara, uandishi wa makala, maonesho, na vipindi vya redio na televisheni. Aidha, wameimarisha klabu za wapinga rushwa katika jamii.

Kulingana na ripoti ya utendaji wa Takukuru Kinondoni kwa kipindi cha Aprili hadi Juni 2024, jumla ya malalamiko 72 ya rushwa yalipokelewa, ambapo saba yalitolewa maamuzi na Serikali kushinda mashauri matatu, huku mengine 24 yakiendelea kusikilizwa.

 Nyakizee aliongeza kuwa Takukuru imefuatilia utekelezaji wa miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh15.9 bilioni, ikigundua kasoro ambazo waliosimamia miradi hiyo wameshauriwa kuzirekebisha.

“Tutafuatilia kwa ukaribu kasoro tulizobaini mpaka miradi hiyo itakapokamilika, ili kuhakikisha ubora na thamani ya fedha zilizotengwa,” amesema Nyakizee.

Related Posts