Vijana 5,744 waandikishwa JWTZ | Mwananchi

Dodoma. Vijana 5,744 waliokuwa na sifa ikiwa ni pamoja na walioshiriki katika ujenzi wa ukuta wa Mererani na Ikulu waliandikishwa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), katika kipindi cha kuanzia mwaka 2019 hadi 2022.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amesema hayo leo Ijumaa Novemba 8, 2024 wakati akijibu swali la la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu Asia Halamga.

“Je, kuna Mpango gani wa kuajiri vijana wa JKT walioshiriki katika ujenzi wa Ukuta wa Mererani, Ikulu na maeneo mengine,” amesema.

Akijibu swali hilo, Dk Tax amesema Jeshi la Kujenga Taifa lilianzishwa mwaka 1963 kwa lengo la kutoa mafunzo ya uzalendo, ulinzi na malezi kwa vijana wa kitanzania.

Amesema mafunzo hayo, yanalenga kuwafundisha umoja na mshikamano, ukakamavu na kuwa tayari kulitumikia Taifa lao wakati wote.

“Katika mafunzo hayo, vijana hufundishwa pia stadi mbalimbali za kazi na maisha. Lengo ni kuwawezesha vijana hao kuwa na uwezo wa kujitegemea baada ya mafunzo,” amesema.

Aidha, amesema JWTZ huandikisha askari wapya kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo yanayotolewa mara kwa mara, kama ilivyofafanuliwa katika Kanuni ya 5 ya Kanuni za Majeshi ya Ulinzi, Juzuu ya Kwanza (Utawala).

Hivyo, amesema vijana wote wanaojiunga na JKT huandikishwa kwa kufuata utaratibu huo.

Katika swali la nyongeza, Asia amehoji kuwa Serikali haioni haja ya kuwachukua pia vijana waliojenga Chuo Kikuu cha Mzumbe (Morogoro), bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, nyumba za wakazi wa Msomera (Handeni- Tanga) na nyumba za Ukonga (Dar es Salaam) kwa kuwa zote ni kazi za operesheni kwa kuwa ni kazi za msimu.

“Kwa kuwa JWTZ haiwezi kuwa na nafasi zinazojitosheleza watu wote, haioni kuungana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuwa na data base ya vijana waliofanya kazi maalumu wakaweza kuwekwa katika majeshi mengine?” amehoji.

Akijibu swali hilo, Dk Tax amesema utaratibu wa kuwachukua vijana ni kama alivyoeleza katika majibu ya swali la msingi lakini vijana wote wanaokwenda JKT hushiriki katika operesheni mbalimbali.

Hata hivyo, amesema kwa kadri ya mahitaji ya wakati huo yalivyo na jinsi nafasi zinavyopatikana vijana mbalimbali huandikishwa.

Kuhusu database, Dk Tax amesema ipo na wanashirikiana na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama katika kuainisha vijana wakwenda kwao na wenye sifa kulingana na mahitaji yao.

“Lakini ikumbukwe pia katika Bunge hili liliondoa kigezo hicho, pengine tukalishauri kuangalia upya kigezo hicho ambacho kiliondolewa,”amesema.

Februari 16, 2024, Bunge lilipitisha azimio la kuondoa kigezo cha kupitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) kwa vijana wanaomba kuandikishwa JWTZ na ajira katika vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

Azimio hilo lilitokana na mjadala mkali wa wabunge na mawaziri uliotokana na mwongozo wa Spika uliombwa na Mbunge wa Mbozi (CCM), George Mwanisongole kutokana na mafunzo ya JKT kutochukuwa wahitimu  wote wa kidato cha nne na cha sita.

Related Posts