Vilio wagombea kuenguliwa uchaguzi serikali za mitaa

Dar/Dodoma. Wakati vyama vya siasa vya upinzani vikilalama wagombea wake kuenguliwa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa serikali za mitaa, Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa amevitaka kuacha kulalamika pembeni badala yake vitumie siku mbili zilizowekwa kuwasilisha malalamiko.

Kwa mujibu wa vyama hivyo, wagombea wake wameenguliwa kwa sababu mbalimbali zikiwamo za mihuri kukosewa, uraia, kukosa vigezo na umri kuwa tofauti na uliojazwa kwenye daftari la wakazi.

Wakati vyama vya upinzani vikipaza sauti kuilalamikia Tamisemi kuhusu mwenendo wa uteuzi wa wagombea, Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeitaka ofisi hiyo kutenda haki kwa vyama vyote vilivyosimamisha wagombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.

Akizungumza na wanahabari jijini Dodoma leo Novemba 8, 2024 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, Mchengerwa amesema kuna siku mbili za kupokea changamoto na malalamiko (pingamizi za uteuzi) mbalimbali kupitia taratibu ambazo wagombea wanatakiwa kuzifuata endapo hawajaridhika.

“Uchaguzi wa serikali za mitaa unaongozwa na sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali iliyotolewa. Nawakumbusha uchaguzi huu ni wa kisheria, hivyo mtu yeyote mwenye malalamiko afuate sheria na kanuni.

“Sheria na kanuni zetu hazijaacha ombwe kama kuna jambo lolote linaloweza kuibuka kutokana na uchaguzi huu. Nitoe wito kwa wagombea wasioridhika na uamuzi utakaotolewa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kuhakikisha wanawasilisha pingamizi zao kwa njia sahihi,” amesema Mchengerwa.

Amesema hawategemei mtu yeyote kuonewa katika uchaguzi huo kwa sababu misingi yake ni Katiba na kanuni za uchaguzi ambazo zimeeleza nini cha kufanya kwa wagombea wasioridhika na wale walioridhika na uteuzi. Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi huo, siku ya uteuzi ni leo Novemba 8.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mrema akizungumza na wanahabari leo Novemba 8, jijini Dar es Salaam amesema wagombea wa chama hicho wameenguliwa pasipo sababu za msingi.

Hata hivyo, Mrema amesema hawataka tamaa bali watafuata utaratibu uliowekwa ili kukataa rufaa.

“Bukoba Vijiji wa kata (wagombea) 11 wameenguliwa wote na sababu zilizowekwa ni kwamba wamekosa vigezo, vivyo hivyo Wilaya ya Serengeti katika kata nane wagombea wetu walioenguliwa hapa sababu yao muhuri haukamilika,” amedai Mrema.

Amedai wilayani Kilosa wagombea wa Chadema wameenguliwa baada ya fomu zao kuchezewa na wasimamizi wa uchaguzi akidai waliongeza herufi katika majina na kuwakosesha sifa za kuwania nafasi hiyo.

“Haya mambo yalifanyika mwaka 2019, lakini safari hii wasimamizi wasaidizi wamesahau kwamba kuna fomu mbili ambazo moja mgombea anaondoka nayo baada ya kukidhi matakwa ya taratibu za mchakato huu.

“Hapa Dar es Salaam, Kibamba wagombea wetu wameenguliwa na sababu iliyowekwa eti hana kazi ya kumpatia kipato halali, ukiandika mjasiriamali unaambiwa hiyo siyo kazi, sasa sijui walitaka watu wadanganye au,” amehoji Mrema.

Kwa mujibu wa kanuni ya 15 ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji za mwaka 2024 miongoni mwa sifa za mgombea ni awe raia Tanzania, awe na umri wa miaka 21 kuendelea, uwezo wa kusoma au kuandika Kiswahili au Kiingereza.

Pia awe na shughuli halali ya kumwezesha kuishi na awe mkazi wa eneo husika au kitongoji, kijiji na mwanachama wa chama siasa, awe na akili timamu.

Mrema amesema mwaka 2019 Chadema ilijitoa katika hatua ya uteuzi, lakini safari hii hawatajitoa katika mchakato kwa masharti ya kwamba hawapo tayari kuonewa.

Kutokana na hilo, Mrema amewataka waliongeuliwa kinyume cha utaratibu kukata rufaa kwa mujibu wa kanuni ya 21, akiwataka wanachama wao kutokata tamaa kutokana na mazingira yaliyopo.

Hata hivyo, ameeleza Chadema kitaketi kwa siku za usoni kutoa msimamo kuhusu uchaguzi huo.

“Katika uchaguzi huu tunataka tufuate hatua kwa hatua, maana nchi kila siku wanajaribu kusema Chadema wakorofi na wana matatizo, lakini kwenye mchakato tutafuata hatua kwa hatua ili dunia ione,” amesema.

Kilio cha wagombea kuenguliwa kipo pia katika vyama vya Ada Tadea, CUF, ACT-Wazalendo na AAFP.

Viongozi wa vyama hivyo waliozungumza na Mwananchi wamesema asilimia kubwa ya watu waliosimamishwa hasa katika maeneo ambayo ndiyo ngome zao wameenguliwa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi.

“Tunaendelea kukusanya takwimu kwa kweli hali inasikitisha na hakuna sababu za msingi wanazozisema, eti muhuri wa chama hakuna, wakati uhalisia muhuri uliwekwa na walichukua nakala za fomu zao baada ya kuzikabidhi kwa wasimamizi,” amesema Mohamed Ngulangwa ambaye ni Mkurungenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib amesema kwa nyakati tofauti amekuwa akipigiwa simu na viongozi wa vyama hivyo wanaomlalamikia kuhusu wagombea wao kukatwa.

Khatib ambaye ni Mwenyekiti wa Ada Tadea amesema suala la wagombea kuenguliwa limekuwa kilio kwa kila chama cha upinzani.

“Mchakato haupo sawa, mgombea wetu ameenguliwa kisa yeye ni mjasiriamali. Huu ni mtihani mkubwa, inasikitisha sisi hatuna uwezo wa kusimamisha wagombea maeneo yote, basi hata yale tulipowaweka wamewaengua,” amesema.

Msemaji wa Kisekta wa Tamisemi ACT-Wazalendo, Rahma Mwita amesema: “Hali ni mbaya, wagombea asilimia kubwa wameenguliwa. Tumehangaika kuwekeza na kusimamisha wagombea nchi nzima, kilichotokea wameenguliwa hasa katika maeneo ambayo chama kina ushawishi.

“Tanga Mjini, Newala, Bukoba Vijijini wameenguliwa wote, sababu zinazotajawa hazina mashiko eti ameshindwa kuthibitisha uraia wake, sasa alipewaje fomu,” amehoji.

Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe amesema bado anaendelea kukusanya taarifa, lakini suala la wagombea kukatwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa ‘ndiyo habari ya mjini’ hasa kwa vyama vya upinzani.

“Watu wanalalamika sana wanaokatwa ni vyama vya upinzani, siyo CCM. Tunashinda kuelewa hawa watu (wasimamizi wa uchaguzi) wamesomea kukata upinzani tu, inashangaza, chama tawala wagombea wake hawakatwi,” amesema.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla akizungumza na viongozi, wanachama na wagombea wa uchaguzi wa serikali za mitaa wilayani Temeke ameitaka Tamisemi kutenda haki katika mchakato huo.

“Nitumie nafasi hii kuwaomba Tamisemi waitendee haki kwa CCM na vyama vingine vyote vitendewe haki. Tunaamini uchaguzi utakuwa huru na haki na atakayeshinda kwa haki, atangazwe.

“CCM hatuhitaji upendeleo, hatuhitaji kubebwa, tuko tayari kwani tulishajipanga. Hatuhitaji mbelekeo na Tamisemi itende haki kwa vyama vyote vya siasa vilivyoweka wagombea na sisi tupo tayari kushindana na tutashinda kwa haki,” amesema Makalla katika taarifa ya chama hicho kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Novemba 8.

Katika mkutano na wanahabari, Mchengerwa amesema wote wanaopeleka rufaa katika ngazi hiyo ya chini, wasikilizwe na uamuzi wa haki utolewe.

“Niwaelekeze wasimamizi wasaidizi katika maeneo yote kuhakikisha wanatenda haki na kuzingatia misingi ya 4R kama ambavyo kanuni zetu, taratibu zetu zilivyotoa miongozo sahihi kabisa nini cha kufanya,” ameagiza.

Related Posts