Viongozi wa EU wakutana Budapest – DW – 08.11.2024

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wako Budapest wanakokutana kwenye mkutano wa kilele usio rasmi, kutafuta njia za kuimarisha mikakati yao ya ushindani mbele ya Marekani na China.

Mkutano wa viongozi wa Ulaya mjini Budapest
Mkutano wa kilele wa UlayaPicha: Marton Monus/REUTERS

Waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban ambaye nchi yake ndiyo mwenyekiti wa sasa wa  Umoja wa Ulaya ametabiri kwamba yatashuhudiwa mabadiliko makubwa ulimwenguni, tena ya haraka kuliko inavyofikiriwa, baada ya Donald Trump kushinda uchaguzi wa rais nchini  Marekani na hivyo amesisitiza kwamba Ulaya inabidi iutazame ukweli huu na kuchukuwa hatua.

“Kuna makubaliano kwamba Ulaya inapaswa kuchukuwa dhima kubwa katika suala linalohusu amani yake  na mustakabali wa usalama wake yenyewe, na hata kujihusisha yenyewe moja kwa moja na hatupaswi kuwategemea Wamarekani  kutulinda sisi.”

Orban aliyazungumza hayo jana akiwa na waziri mkuu wa Albania baada ya mkutano wa jumuiya ya kisiasa ya Ulaya, ambako takriban viongozi 50 wa Ulaya walikutana.

Hii leo Ijumaa  kabla ya mkutano wa kilele usiokuwa rasmi wa viongozi wa Umoja wa Ulaya,Orban alikiambia kituo cha redio cha serikali nchini Hungary kwamba Marekani chini ya Donal Trump itaachana na vita vya Ukraine na hapana shaka Ulaya haiwezi kufadhili pekeyake vita hivyo.

Viongozi wa Ulaya katika mkutano wa Budapest
Viongozi wa Ulaya katika mkutano wa BudapestPicha: Mehmet Ali Ozcan/Anadolu/picture alliance

Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani, baada ya kuzungumza na viongozi wengine katika Umoja wa Ulaya kwenye mkutano huo wa kilele usio rasmi amesema viongozi wa Ulaya wataendelea kufanya kazi vizuri na rais wa Marekani huku pia akiongeza kwamba Umoja wa Ulaya unapaswa  kubakia thabiti kuhusiana na vita vinavyoshuhudiwa Ulaya na Mashariki ya Kati.

Washirika wa Umoja wa Ulaya katika Jumuiya ya NATO wanatarajia kumshawishi Trump kwamba ikiwa atasaidia kusimamia hatua yoyote ya kufikiwa amani basi itapaswa kufanyika kwa kuzingatia msimamo wa kuonesha nguvu za pande zote mbili  Ukraine na Marekani.

Mkutano huo wa Budapest wa leo Ijumaa unataka pia kutafuta njia ya kuimarisha ushindani wa jumuiya hiyo mbele ya macho ya Marekani na China.Soma pia: Viongozi wa Ulaya wakutana Budapest kufuatia ushindi wa Trump

Umoja huo wa Ulaya kwa muda mrefu umekuwa ukihangaika na suala la ukuaji uchumi tangu liliposhuhudiwa janga la Uviko-19 na athari za kupanda kwa gharama ya nishati kulikotokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani
Kansela Olaf ScholzPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Kurudi tena madarakani wa Donald Trump kumeibuwa upya dharura ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Tayari Trump ameshasema kwamba atapanisha ushuru wa hadi asilimia 10 na 20 kwa bidhaa kutoka nje. Trump anasema kwamba Marekani imekuwa ikiangaliwa sio kwa jicho la usawa na Umoja wa Ulaya pamoja na washirika wengine wa kibiashara.

Kadhalika mkutano huo unaofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Puskas mjini Budapest, utajadili uchaguzi wa hivi karibuni huko Georgia na uamuzi wa Israel wa kulipiga marufuku shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wakipalestina UNRWA.

 

Related Posts