WACHEZAJI WA MSD WATAKAOSHIRIKI SHIMUTA WAAGWA KUANZA SAFARI KUELEKEA KWENYE MASHINDANO TANGA

Wachezaji wa Bohari ya Dawa (MSD) watakaoshiriki kwenye mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma,Taasisi na Makampuni Binafsi (SHIMUTA) mwaka 2024 jijiniTanga, leo Ijumaa tarehe 8 Novemba 2024 wameagwa na Menejimenti ya MSD na kuanza safari ya kuelekea kwenye mashindano hayo.

Akizungumza wakati wa kuwaaga wachezaji hao Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Elisamehe Macha amewakumbusha watumishi hao kuwa michezo ni sehemu ya kazi hivyo wanapaswa kuhakikisha wanaenzi tunu za MSD ikiwemo uhodari na nidhamu kama wanapokuwa sehemu zao za kazi.
“Tunategemea kuona mnajituma ikibidi kupata ushindi, MSD inathamini na kuwekeza kwenye michezo kwa kuwa michezo ni afya kwa watumishi wetu na inapelekea kuleta tija kwenye utendaji wa watumishi wa MSD. Mnapokuwa michezoni msisahau kuzingatia nidhamu kwa kuwa mnabeba taswira ya taasisi.

Macha, amewaeleza kuwa Menejimenti ya MSD inapenda michezo ifanyike kwa umahiri kwani MSD tumeanza kushiriki mashindano haya ya SHIMUTA, tujipange vizuri ili kuhakikisha MSD inashiriki vizuri zaidi kwenye michezo hii pamoja na mingine ijayo kwa kufanya maandalizi ya mapema na kuweka mfumo mzuri wa kutambua vipaji vya watumishi.

MSD imepeleka wachezaji hamsini na tisa (59) kushiriki michezo mbalimbali katika mashindano ya mwaka huu ya SHIMUTA

Related Posts