Tarime. Askari wanyamapori amefariki dunia, huku mtu mmoja akijeruhiwa baada ya tembo kuvamia Kijiji cha Murito wilayani Tarime, mkoani Mara wakitokea katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Askari huyo, Arafat Miyimba (27) amefariki dunia wakati yeye na wenzake wakiwa katika harakati za kuwarudisha tembo hao hifadhini.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele amesema tembo wanne walivamia kijijini hapo leo Novemba 9, 2024 saa 3.30 asubuhi.
Gowele amesema baada ya tembo kufika kijijini hapo, mwanakijiji Idrisa Musa (25) alijeruhiwa mwilini ndipo wananchi walipoomba msaada kutoka mamlaka husika.
“Baada ya kupata taarifa za uvamizi huo wa tembo niliwasiliana na Senapa ili kufika eneo la tukio na kutoa msaada. Walitumwa askari saba wa wanyamapori kwa ajili ya kuwakoa wakazi wa kijiji hicho kutokana na kadhia hiyo,” amesema.
Amesema askari walifika mapema kabla madhara zaidi hayajatokea wakaanza utaratibu wa kuwarejesha tembo hifadhini.
Ameeleza askari wakiwa katika harakati za kuwarejesha hifadhini, tembo waligeuka na kuanza kuwafukuza.
Katika kukimbia Miyimba alianguka na wakati ananyanyuka tembo mmoja alimjeruhi kwa kutumia meno yake.
“Askari wengine walijitahidi kumuokoa mwenzao lakini ilishindikana alifia palepale. Baada ya tukio tembo hao walikimbilia hifadhini,” amesema.
Amesema majeruhi amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara kwa matibabu zaidi.
Gowele amesema Kijiji cha Murito ni kati ya vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na mara kadhaa Serikali imekuwa ikiwasisitiza wananchi kuhama kutoka katika maeneo yaliyo jirani na hifadhi kuepuka madhara yanayoweza kutokea.
“Tumempoteza askari leo akiwa anajaribu kuwaokoa wananchi lakini mara kadhaa tumewasisitiza kutoka maeneo yaliyo jirani na hifadhini, kwani ni hatari kwao na hata ufanyaji wa shughuli za maendeleo katika maeneo hayo ni changamoto,” amesema.
Amesema bado wanaendelea kuwasisitiza wananchi kuhama kutoka katika maeneo hayo kwa maelezo kuwa kwa mujibu wa wataalamu wapo wanyamapori kama tembo, ambao wana utamaduni wa kurejea katika maeneo waliyokuwa wakiishi miaka ya nyuma kama ilivyotokea leo.
Uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, umekiri kutokea kwa tukio hilo, ukisema taratibu za mazishi ya askari huyo zinaendelea.