Dube kimemkuta nini Yanga? Mafaza wafunguka

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Prince Dube bado anajitafuta ndani ya timu hiyo, huku namba zake nazo zinakosa utulivu sahihi ambao aliutarajia na hata uliotarajiwa na mashabiki na viongozi wa timu hiyo.

Dube alitua Yanga msimu huu akitokea Azam FC ambayo aliitumikia kwa miaka minne kuanzia 2020 alipotua nchini kisha kulazimisha dili la kutua Yanga iliyolazimika kumwaga fedha nyingi ili kumsajili.

Wakati Dube anatua Yanga kulikuwa na matarajio makubwa kwamba mshambuliaji huyo anakwenda kuungana na kikosi ambacho namba zake za ufungaji zingekua kwa haraka na kukuza jina na hata klabu yake.

Tofauti na matarajio hayo Dube hakuanza na kasi hiyo, lakini pia haonyeshi utulivu kwamba labda mambo yatakaa sawa.

Kando na hayo hakuna anayejua kitu gani kimemkuta kwani hadi sasa ana asisti moja tu Ligi Kuu Bara, huku akiwa hana bao lolote, kitu ambacho si kawaida kwa muda aliotumika kikosini.

Dube lazima akili yake ikumbane na mabadiliko hayo kwamba, sasa ametua Yanga klabu ambayo ina presha kubwa ya matokeo. Ndani ya Yanga hakuna muda wa kusema unatafuta kujipanga, akili yake inatakiwa kujiongeza haraka na ifanye kazi.

Nyota lazima ajiondoe kwenye unyonge na anachotakiwa ni kuvua vazi la presha na kuvaa lile la ujasiri kisha kupigania nafasi yake ndani ya Yanga kwani timu hiyo ni tofauti na kule alikotoka Azam ambako angeweza kukaa hata mechi 50 bila kufunga na maswali yasiwe mengi  sana.

Ukitazama mechi ambazo Dube ameshacheza mpaka sasa akifunga mabao matatu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali kisha bao moja la mchezo wa fainali ya ngao ya jamii baada ya hapo mambo yakabadilika haraka.

Mzimbabwe huyo hajafunga bao lolote kwenye ligi katika mechi 10, lakini licha ya kupata nafasi ya kutosha ameonekana kuwa  na presha kubwa uwanjani ikimpunguzia utulivu.

Nafasi ambazo Dube amekuwa akizipoteza ameonyesha  kwamba anakosa kujiamini akiikubali presha kuingia  kwake na kujiweka katika wakati mgumu kufanya mambo makubwa uwanjani.

Dube anaweza kujifunza kwa kiungo mpya wa timu hiyo Clatous Chama ambaye alipotua ndani ya Yanga tena akitokea Simba alikaribia kukumbana na presha ya namna hiyo, lakini akaikwepa fasta.

Wakati Chama akianza kuandamwa na kuonekana kama hatapata nafasi ndani ya Yanga alivaa vazi la ujasiri na kubadilika haraka akaanza kufanya mambo yake akiasisti na hata kufunga na sasa anaendeleza makali yake.

Hili la Chama linaweza kuwa elimu kubwa kwa Dube ili kulinda nafasi ndani ya kikosi cha Yanga, vinginevyo akiendeleza unyonge utamuondoa njiani.

Wakati Dube akikumbana na ukame huo wa mwanzo wa ligi washindani wake watatu katika nafasi anayocheza kina Clement Mzize, Kennedy Musonda na hata Jean Baleke ambaye alikosa mechi nyingi za kwanza wameshaanza kufunga, kila mmoja akiwa na bao moja kwenye ligi huku Mzize mabao mawili.

Hii ni presha nyingine kwa Dube ambayo anatakiwa kuikataa na kuamua kupambana kwani nafasi bado anayo kwa benchi la ufunzi kama ambavyo ameendelea kuaminiwa ndani ya kikosi hicho.

Mashabiki wa Yanga wanaumizwa na hali anayokumbana nayo Dube wakiwa bado hawajakata tamaa wakisubiri mabao yake na atakapoanza kufunga tu upepo utabadilika haraka na kuanza kumuimba kwa mazuri na kusahau ya nyuma haraka.

Ikukumbukwe kuwa mbali na kufunga klabuni, lakini Dube pia ni nyota wa kikosi cha timu ya taifa ya Zimbabwe na amekuwa akifunga mabao ya maana tu, isipokuwa ameonekana kuyumba katika ligi wakati kwa mechi za CAF na michuano mingine nje ya ligi ya Bara jamaa amefunga na hapo ndio swali linakuja… kimemkuta nini kwa sasa hadi ashindwe kufunga walau bao moja katika ligi aliyozoea kufunga?

Msimu wa mwisho wa Dube akiwa na Azan kabla ya kuhamia Yanga aliichezea michezo 16 ya mashindano.

Kwenye michezo hiyo alicheza mechi 12 za ligi kati ya 19 akifunga mabao saba na kutoa asisti mbili kabla ya kugoma kuendelea na mkataba wake.

Pia alicheza mechi mbili za Kombe la FA bila kufunga bao wala kutoa asisti, lakini pia akicheza mechi mbili za Kombe la Shirikisho Afrika akifunga bao moja na kuhusika kwenye mabao 10 ndani ya msimu. 

Lakini kwa ujumla hesabu zinaonyesha katika misimu minne ya kuitumikia Azam katika Ligi Kuu, mwamba huyo aliifungia jumla ya mabao 33 na kama sio kuwa majeruhi mara kwa mara huenda hadhithi ingekuwa nyingine katika msimu wa kwanza alipotua akitokea Highlanders ya Zimbambwe alipofunga mabao 14 katika mechi zisizozidi 20.

Msimu wa pili aliumia na kuishia kufunga bao moja wakati ule wa tatu alitupia mabao 11 na wa mwisho akicheza mechi chache alifunga mabao saba mbali na asisti za kumwaga na mabao mengine ya mechi za michuano ya CAF, Kombe la Mapinduzi na mingineyo aliyoitumikia timu hiyo.

Akizungumzia ukame huo wa Dube, mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba ‘Tekelo’ alisema  kinachomtafuna ni namna alivyopoteza umakini kwa kuamua kuikubali presha, lakini bado ana nafasi  ya kubadilisha mambo.

Mziba anasema Dube anatakiwa kurudisha umakini  akiwa uwanjani kwani timu anayoichezea ina viungo bora waliomzunguka.

“Kinachomharibia Dube ni kuikubali presha. Unajua anatoka kwenye timu ambayo haina presha ya matokeo na alianza vizuri, lakini alipoanza kupoteza nafasi za wazi pale ndio kumemtisha,” anasema Tekelo.

“Nadhani bado ana nafasi kubwa. Naona makocha wanamuamini nafasi anapata ya kucheza na anacheza kwenye timu ambayo anazungukwa na viungo bora. Anachotakiwa ni kutuliza akili akishafunga mabao hata mawili ahakikishe anakuwa jasiri kisha aendelee kupambana.”

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Chinga One’ anasema Dube ajitathimini kwa kufanya mambo mawili – kwanza kama anaona kucheza nafasi ya mshambuliaji wa kati inampa shida azungumze na kocha washauriane, lakini kama anataka kucheza  mshambuliaji wa mwisho, basi aongeze utulivu wa kutumia nafasi.

“Unajua Dube ni mshambuliaji mwenye ubora hata wa kushambulia akitokea pembeni na akicheza huko amekuwa akifunga pia. Sasa kama anaona ili awe bora atokee huko aongee na makocha watashauriana,” anasema Chinga

“Kama anataka kuendelea kucheza mshambuliaji wa mwisho basi atulize, akili ashushe presha. Ni kweli Yanga kuna presha lakini ukiwa mtulivu utafunga sana tu. Namuona kama hana utulivu wa kutumia nafasi hii ni timu kubwa anayoichezea sasa watu wake wanataka ushindi tu. Akitulia atafunga mabao mengi tu.”

Related Posts