Dar es Salaam. Asubuhi ya leo ilitokea taarifa iliyoacha simanzi kwa wengi, nayo ni ya kifo cha Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrance Mafuru ambaye amehudumu nafasi hiyo kwa mwaka mmoja na miezi mitatu.
Mafuru aliyekuwa mtaalamu wa fedha na uchumi maarufu hapa nchini akihudumu katika sekta binafsi na sekta ya umma, amefariki dunia leo Novemba 09, 2024 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Apollo nchini India.
Pengine utajiuliza Tume ya Mipango ina kazi gani na kwa nini kuondoka kwa bosi wa ofisi hiyo ni pigo kwa nchi. Kwa mujibu wa tovuti ya tume, taasisi hiyo ina wajibu na majukumu kama ifuatavyo.
Moja ni kutathmini hali ya rasilimali za Taifa na kuishauri Serikali kuhusu matumizi bora ya rasilimali hizo na kuandaa dira ya maendeleo ya Taifa, mpango wa maendeleo wa muda mrefu, mpango wa maendeleo wa muda wa kati na mpango wa maendeleo wa muda mfupi na kusimamia utekelezaji wake.
Kupendekeza maeneo ya miradi endelevu ya kielelezo na mikakati ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuzingatia dira na mikakati ya maendeleo ya taifa na kufanya tathmini na uchambuzi wa mara kwa mara wa viashiria muhimu vya uchumi, ambavyo vinajumuisha urari wa malipo, mtiririko wa fedha na bei, deni la Taifa na kuishauri Serikali ipasavyo.
Pia ofisi hiyo ina wajibu wa kutathmini sera mbalimbali zilizopo kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wake kwa kuzingatia mipango ya maendeleo ya Taifa na kupendekeza sera mpya pale inapoonekana inafaa kwa maslahi ya Taifa na kufuatilia utekelezaji wa maeneo muhimu ya vipaumbele vya Taifa kwa sekta mbalimbali za uchumi, na kuhakikisha kuwa hatua stahiki zinachukuliwa ili kutatua changamoto zozote za uendeshaji zitakazobainika katika sekta hizo.
Ofisi hiyo iliyo chini ya ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, ina kazi ya kutoa mwongozo kuhusu ushirikiano wa kiuchumi kati ya Jamhuri ya Muungano na nchi nyingine na mashirika ya kimataifa na kuhakikisha mipango ya sekta, inafungamanishwa na mipango ya taifa ili kuwa na matumizi yenye tija ya rasilimali za nchi.
Vilevile kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mipango ya kitaifa na miradi ya kielelezo na kuchukua hatua zinazohitajika ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi pamoja na kuishauri Serikali kuhusu mabadiliko yoyote katika mpango wa maendeleo wa Taifa ulioidhinishwa.
Tume ya Mipango pia ina jukumu la kufuatilia utekelezaji wa maamuzi ya baraza la mawaziri kuhusu masuala ya mipango ya maendeleo na usimamizi wa uchumi, kushauri kuhusu mikakati ya kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu nchini na kukuza mbinu za ubunifu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Kazi yake nyingine ni kutambua na kufanya utafiti kuhusu suala lolote ambalo tume inaona ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa na kusimamia na kutoa mwongozo katika uandaaji wa mipango mkakati iliyoandaliwa na wizara, idara zinazojitegemea, wakala za Serikali, sekretarieti za mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na taasisi nyingine za umma.
Vilevile tume ina kazi ya kuratibu na kuendeleza kada za mipango, uchumi na takwimu na taaluma nyingine zinazofanana na hizo, kuratibu makongamano ya wadau mbalimbali kwa ajili ya kujadili masuala ya mipango ya maendeleo na kubainisha rasilimali za nchi kwa matumizi endelevu kwa maendeleo ya taifa.
Pia kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi katika upangaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo na kutekeleza majukumu mengine yanayohusiana na mipango ya maendeleo kadri Rais atakavyoelekeza.