MATOKEO ya kupoteza mechi mbili mfululizo yaliyofuata baada ya Yanga kushinda mechi nyingi kwa taabu tofauti na ubora wa kikosi cha timu hiyo iliyojaa mafundi wa boli, yamezua jambo kwa kocha Miguel Gamondi.
Uongozi wa timu hiyo iliyopoteza uongozi wa ligi kwa watani wao Simba baada ya vipigo viwili mfululizo, bao 1-0 kutoka kwa Azam FC na 3-1 kutoka Tabora United, vimewafanya viongozi wa klabu hiyo kukaa kikao cha dharura usiku na kuamua jambo zito.
Usishtuke. Ndivyo upepo ulivyo kwa sasa huko Jangwani, kwamba kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amekalia kuti kavu na taarifa mbaya kumhusu zinaweza kutangazwa wakati wowote.
Mwanaspoti limepenyezewa taarifa kwamba kuna uamuzi mgumu unatarajiwa kuchukuliwa muda wowote na uongozi wa klabu hiyo ambao umeshajifungia kwa vikao vizito mara baada ya timu hiyo kupoteza mchezo wa pili mfululizo katika Ligi Kuu Bara, baada ya awali timu hiyo kucheza mechi nane mfululizo na kushinda bila kuruhusu bao lolote, huku mambo matano yakitajwa ndio yanayomng’oa Muargentina huyo.
Yanga, ilianza kupoteza mechi ya kwanza msimu huu mbele ya Azam FC kwa bao 1-0 wikiendi iliyopita, kisha juzi ikalala tena kwa mabao 3-1 kutoka kwa Tabora United, mechi zote zikichezwa kwenye uwanja wa nyumbani.
Baada ya matokeo hayo ya juzi, usiku huo huo ukawarudisha ofisini mabosi wa Yanga wanaounda Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo na kujadili mwenendo wa timu yao wakijifungia kwa saa nne wakijadili matokeo hayo.
Wakati mabosi hao wakijifungia kujadili hatua ya timu yao, taarifa za uhakika ni kwamba kocha wao Miguel Gamondi hakuwa sehemu ya mkutano huo akiomba akutane nao jana.
Maombi hayo ya Gamondi yakawatibua mabosi wa Yanga na kuona kama kocha huyo amewadharau akishindwa kufika kwenye kikao kilichobeba mustakabali wa timu yao.
Ingawa jana hadi gazeti hili linakwenda mitamboni ilikuwa haijatangazwa, lakini Mwanaspoti linafahamu kwamba maazimio ya kikao hicho mabosi wa Yanga walikubaliana kwamba Gamondi achomolewe pamoja na msaidizi wake.
Mabosi wa Yanga walikubaliana juu ya uamuzi huo wakijadili mambo matano mazito ambayo wameyaona msimu huu ambao ni wa pili wa kocha huyo aliyewapa mataji matatu ndani ya misimu miwili.
Mabosi wa Yanga licha ya timu yao kushinda mechi zote nane za kwanza za ligi bila ya kuruhusu bao kabla ya kupoteza mbili zilizofuata, vigogo hao hawakuridhishwa na namna timu yao ilivyokuwa ikishinda wakiona ni kama inapata matokeo kwa kubahatisha sana.
Yanga imeshinda mechi tano kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0 ikipata ushindi wa mabao 2-0 kwenye michezo miwili huku ushindi mkubwa ni pale walipoichapa Pamba kwa mabao 4-0, vigogo hao wanaona ni kama sio matokeo mazuri kulingana na uwekezaji wa kikosi chao ulioufanya.
Eneo la pili ambalo mabosi hao wameshindwa kukubaliana na kocha wao huyo ni namna anavyokipanga kikosi chake ikielezwa kulikuwa na mgawanyiko mkubwa kwa wachezaji wake kutokana na kutopenda kuwapa nafasi wengine.
Licha ya kocha huyo kuonekana anafanya mzunguko wa kuwapa nafasi wachezaji wake lakini baadhi ya wachezaji walionekana kutozingatiwa katika mgawanyo huo wa muda wa kucheza huku wengine licha ya kuonekana wanahitaji kupumzishwa lakini bado waliendelea kupata nafasi.
Baada ya mchezo wa juzi, mechi inayofuata kwa Yanga ni dhidi ya Al Hilal ya Sudan, mabingwa hao wa soka wakiwa nyumbani kwenye mechi ya kwanza ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayopigwa Novemba 27, 2024.
Hapo hapo mabosi wa Yanga wakapiga hesabu ndefu kwamba kama kikosi chao kikikutana na Al Hilal kikiwa kwenye kiwango cha sasa, ni wazi timu yao inaweza kupoteza kwa kuwa watakutana na timu mbili zinazofundishwa na makocha wanaojuana na pia marafiki Anicet Kiazayidi ambaye amewahi kuwa msaidizi wa Florent Ibenge wote Wakongomani.
Yanga imeona ni bora Gamondi aondolewe sasa kisha kocha mpya mkubwa aje haraka ili aanze kazi haraka ili kuwashtua wapinzani wao lakini pia itarudisha morali ya ushindani kwa wachezaji wao.
Yanga imewahi kumfukuza kocha Mserbia Zlatko Krmpotic akiwa anaongoza ligi tena akitoka kushinda mechi ya mwisho kwa mabao 3-0 lakini mabosi hawa wa Yanga chini ya Injinia Hersi Said wakati huo akiwa sehemu ya mfadhili wakampa mkono wa kwaheri.
Uamuzi wa kumtimua Gamondi ambaye bado timu yake ina tofauti ya pointi moja dhidi ya vinara Simba, inaelezwa hayajapita kwa ugumu mbele ya mabosi hao wakiona ni wakati mwafaka wa kuachana naye ili kuirudisha timu yao kwenye mstari.
Jana Gamondi alikuwa akutane na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andre Ntine katika kupata hatma yake ambapo Mwanaspoti linafahamu mbali na kocha huyo pia msaidizi wake wa kwanza Mussa Nd’ew naye ataungana naye kwenye fagio hilo.