Madiwani upinzani Mtwara wasusia kikao kisa kuenguliwa wagombea

Mtwara. Madiwani 10 wa vyama vya upinzani katika halmashauri ya Mtwara,  wamesusia kikao cha baraza la madiwani kwa madai kuwa mchakato wa wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa serikali za mitaa umefanyika kihuni, hali iliyosababisha wagombea wa vyama vya upinzani kuondolewa.

Hatua hiyo inatokana na kile wanachoeleza kuwa ni kutokubaliana na uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi katika halmashauri hiyo ambaye amewaengua baadhi ya wagombea wa nafasi ya uenyekiti kwa madai ya kujaza vibaya fomu za uteuzi wa wagombea.

Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika Novemba 8, 2024 diwani wa kata ya Ndumbwe ambaye pia ni mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Mtwara, Abdul Mahupa amesema wamechukua hatua ya kususia kikao hicho,  kutokana na kutoridhishwa na  mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi ya uenyekiti ambayo imegubikwa na sintofahamu.

Ameeleza kwamba wagombea wao wameondolewa kwenye uchaguzi kwa sababu ya kushindwa kutimiza vigezo, ikiwemo kujaza vibaya fomu.

“Mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa haukuwa wa haki, tunaondoka na kuacha kikao hiki, tunaenda kusimama na wananchi wetu.

Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya wialaya ya mtwara wakiondoka  baada ya kususia kikao kwa madai ya kuwa kutoridhishwa na mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa.

Tunakufahamisha mwenyekiti kwa kuwa hatujaridhishwa,  ingawa Serikali ilisema kuwa uchaguzi utakuwa wa haki lakini haijafanyika. Hivyo  tumeamua kususia baraza kwa sababu tunaona matukio ni ya kihuni. Wagombea wetu wameondolewa kisa hawakutimiza masharti, jambo ambalo limezua taharuki.

“Hatuwatendei haki wananchi, uchaguzi huu haukuwa wa haki japo wananchi walijitokeza kujiandikisha lakini haki haijatendeka kwa wagombea wetu ili kujadiliana na kupokea maelekezo ya juu kutoka kwenye vyama vyetu, tumelazimika kuondoka nje ya ujumbi huu,” amesema Mahupa.

Ameongeza kuwa yapo makosa ya kikanuni ambayo mtu anaweza kuenguliwa lakini wao hawakufanya, badala yake wanaambiwa kuwa katibu wa tawi ya CUF haruhusiwi kugombea kwa sababu ambayo haina mashiko kwao.

Naye diwani wa kata ya Nanguruwe (Chadema), Patrick Simwinga amekosoa hatua hiyo, akisema ni vigumu kukubali kuwa sehemu ya kikao hicho.

“Unajua watu waliotumia haki yao ya kidemokrasia na nguvu zao za kuwa sehemu ya uchangiaji wa michango ya kimaendeleo kwenye vijiji vyao ya kuwa wenyeviti na wajumbe lakini wanaenguliwa bila sababu, hii sawa,” amesema Simwinga.

Katibu wa ACT Wazalendo Jimbo la Mtwara Vijijini, Hamisi Likwenda amesema anaunga mkono kitendo cha kususia kikao kilichofanywa na madiwani hao.

“Naunga mkono hoja yaani hapa demokrasia hakuna na mimi narudi kuwaona wagombea wangu na kuona hali ilivyo. Kwa kweli tumefikia pabaya na tutatoa tamko kwa nchi nzima, hii hali sio nzuri, hatuikubali,” amesema Likwenda.

Akizungumzia uamuzi wa madiwani Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mtwara Vijijini, Abdala Saidi Makame, amekosoa kitendo cha madiwani hao kutoshiriki kikao, akisema ni utovu wa nidhamu huku akiwataka warudi kwenye viti vyao.

“Jazba unajua haijengi, inabomoa uchaguzi, uko nje ya kikao hiki, hatujapata taarifa yoyote inahusiana na uchaguzi, ni vema wangetafuta majibu kupitia maswali ya papo kwa hapo, walichofanya ni utovu wa nidhamu,” amesema Makame.

Kwa upande wake, msimamizi mkuu wa uchaguzi wa serikali za mitaa halmashauri ya Mtwara, Abeid Kafunda, ameeleza kuwa hajapokea malalamiko yoyote kutoka kwa wagombea walioenguliwa kutoka katika vijiji 110.

Amesema wapo walioondolewa lakini wapo waliofanya vizuri na wakapitishwa, hivyo amesema kwa ambao wana malalamiko wayafikishe ofisini kwake.

“Niwasihi viongozi wa vyama vya upinzani, wanapokuwa na malalamiko, kuwasiliana na maofisa wa uchaguzi ili kuhakikisha mchakato unafanyika kwa amani na haki,” amesema.

Related Posts