LICHA ya kukiri matokeo kutokuwa mazuri, mastaa wa KenGold wamejishtukia na kusema njia mbadala ya kumaliza presha kikosini ni juhudi binafsi za mchezaji mmoja mmoja bila kukata tamaa.
Timu hiyo inayocheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, haina mwenendo mzuri katika ligi hiyo na imecheza mechi 11 ikivuna pointi tano mkiani na kuwapa presha kubwa kwa mashabiki wao.
KenGold ya wilayani Chunya, Mbeya ilipanda Ligi Kuu kwa rekodi tamu ikitwaa ubingwa wa Championship na kwa sasa inahaha kwa matokeo yasiyoridhisha.
Winga wa timu hiyo, Herbert Lukindo alisema licha ya kutokuwa na matokeo mazuri, haiwezi kuwakatisha tamaa badala yake juhudi binafsi za kila mchezaji kikosini zitaiweka pazuri.
Nyota huyo wa zamani wa Mbao na Biashara United aliongeza watatumia vyema kipindi cha mapumziko kusahihisha makosa yao kuhakikisha ligi inaporejea wanafanya vizuri.
“Mpira ndio kazi yangu, napambania timu lakini kujiweka kwenye soko la ushindani, naamini kwa juhudi za mchezaji mmoja mmoja itatuweka pazuri kwenye msimamo,” alisema nyota huyo mwenye mabao matatu.
Kwa upande wa straika wa timu hiyo, Mishamo David mwenye mawili alisema baada ya kufungua akaunti ya mabao kazi imeanza upya, hawajachelewa na ligi haijasha hivyo lolote linaweza kutokea.
“Ushindani ni mkali lakini lazima tupambane, nashukuru nimeanza kutupia na hii inaongeza nguvu na morali kwangu kuendelea kuipigania timu kujiweka pazuri,” alisema nyota huyo aliyefunga mabao mwili yaliyoipa KenGold sare ya 2-2 nyumbani mbele ya Dodoma Jiji kwemue Uuwanja wa Sokoine, jijiini hapa.