Sh10,000 yamweka bodaboda matatani, adaiwa kumchoma moto mtoto

Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia dereva bodaboda, Juma Afyusisye (38), mkazi wa Iwambi jijini humo kwa kosa la kumjeruhi kwa kumchoma moto mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Iwambi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Novemba 9, 2014 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, kijana huyo alimpatia fedha Sh10,000 mwanafunzi huyo kwa ajili ya kununua maandazi ya Sh5,000 ambapo mwathirika huyo aliitumia pesa yote kwa matumizi binafsi.

Amesema baada ya mwathirika kurejea akionekana hana pesa hiyo, mtuhumiwa alijichukulia sheria mkononi kwa kumwagia mafuta ya petroli kisha kuwasha kiberiti na kumsababishia majeraha sehemu za mwili.

“Mwathirika amelazwa Hospitali ya Ifisi katika mji mdogo wa Mbalizi kwa huduma zaidi, Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wazazi na walezi kutojichukulia sheria mkononi, badala yake watumie njia sahihi kuwaadhibu watoto.

“Lakini hatutaendelea kufumbia macho aina yoyote ya ukatili na unyanyasaji katika jamii, bali itaendelea kuchukua hatua kali kwa watuhumiwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Kuzaga.

Hata hivyo, kwa mujibu wa maelezo ya mtoto huyo, aliyelazwa katika hospitalini hiyo kwa matibabu, amesema jirani huyo alimpa Sh10,000 ili anunue sukari na maandazi ambapo aliporejea Sh200 ilipotea na kujikuta akichomwa moto.

Amesema baada ya kumwagia petroli , alimvisha tairi kisha kumuwashia kiberiti na kumuacha akiwaka moto kabla ya kusaidiwa na majirani wengine waliofika.

“Alinipa Sh10,000 nimnunulie maandazi na sukari, sasa Sh200 ikapotea ndio akanimwagia petroli na kunivisha tairi kisha kuniwashia kiberiti na kuondoka, baadaye nikasaidiwa na watu,” amesema mwanafunzi huyo.

Daktari bingwa wa upasuaji katika hospitali teule ya Ifisi, Dk Amos Mboela amethibitisha kutokea tukio hilo akieleza kuwa mwathirika alifikishwa hospitalini hapo jioni na kupatiwa matibabu.

Amesema kutokana na mazingira ya eneo la tukio hilo kutokuwa mazuri, alipofikishwa hospitalini hapo alipewa huduma ya haraka ikiwamo dawa za tetenasi.

“Mgonjwa anaendelea na huduma na afya yake inaimairika japokuwa ilibainika mazingira aliyopatiwa janga hayakuwa mazuri na alipewa huduma ya haraka pamoja na dawa za tetenasi,” amesema Dk Mboela.

Baba mzazi wa mhanga huyo, Ebloni Mwambigija amesema hakuelewa kiini cha jirani huyo kuchukua uamuzi huo kumchoma mwanawe akieleza kuwa anaona nia kubwa ilikuwa ni kumuua.

Amesema ukatili wa namna hiyo hauwezi kukubalika akiomba mamlaka na vyombo vya dora kuchukua hatua kali ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye roho za hivyo.

Naye mama mzazi wa mtoto huyo, Malta Abiud amesema walipokea taarifa za mwanao kuchomwa moto kutoka kwa wasamaria wema.

“Tunaomba hatua kali zichukuliwe zaidi ili kukomesha vitendo vya kikatili kama hivi,” amesema mzazi huyo.

Related Posts