Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imewaita wananchi wa Cuba na ukanda wa visiwa vya Caribbean kujifunza lugha ya Kiswahili ili kurahisisha mawasiliano katika mtangamano wa biashara, utalii na uwekezaji kwa Bara la Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma leo Jumamosi Novemba 9, 2024 imemkariri Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro akieleza hayo wakati wa kongamano la Kiswahili lililofanyika Havana, nchini Cuba.
Dk Ndumbaro amewaambia wananchi wa Cuba na wale wa ukanda wa Caribbean kwamba Kiswahili kimekuwa lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kikanda, ikiwemo Jumuiya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU).
Amesema wananchi wa ukanda wa Caribbean wana kila sababu ya kutumia Kiswahili kama nyenzo ya mawasiliano, akieleza Afrika itanufaika zaidi na fursa zilizopo katika ukanda huo kwa sababu watatumia lugha ya Kiswahili.
“Moja ya kanuni ya kujifunza lugha ni kuitumia eneo inapozungumzwa zaidi, nitumie fursa hii, kuwaalika ndugu zetu wa Cuba na ukanda wa Caribbean kunoa Kiswahili chenu zaidi Tanzania.
“Mkiwa Tanzania mtapata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii kama Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama ikiwemo ya Serengeti na visiwa vya marashi ya karafuu Zanzibar,” amesema.
Dk Ndumbaro amesema wakifika Zanzibar watajiona kama vile wapo ukanda wa visiwa vya Caribbean kwa sababu hali ya hewa na mazingira ya bahari yanafafana.
“Mtapata fursa kuona shule maarufu za sekondari zilizojengwa kwa msaada wa Cuba chini ya Kamanda Fidel Castro (Kiongozi mwanamapinduzi wa Cuba)” amesema.
Akizungumzia kongamano hilo, Dk Ndumbaro amesema litasaidia kuunganisha lugha ya Kiswahili na Kihispaniola ili kuwaleta watu wengi pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, kiuchumi na utalii.
“Pia itaongeza fursa ya ajira kwa vijana wetu kupitia ukalimani katika mashirika mbalimbali ya kimataifa hata kuandaa machapisho mbalimbali,” amesema.
Amesema kongamano hilo lenye kaulimbiu isemayo ‘Ustawi wa Kiswahili duniani, tulipotoka, tulipo na tunapokwenda’ litakwenda sambamba na uzinduzi wa maandiko kutoka lugha ya Kiswahili kwenda Kihispaniola.
“Kutakuwa na uzinduzi wa kamusi ya Kiswahili na Kihispaniola iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Havana, nyaraka nyingine ni kitabu cha misemo cha Kihispaniola kilichoandaliwa na Bakita-Baraza la Kiswahili Tanzania.
Dk Ndumbaro amesema nyaraka nyingine ni kitabu kilichoandaliwa na nguli wa Kiswahili kutoka Zanzibar, Said Khamis aliyeshikiriana na Shani Khalfan.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameishukuru Serikali ya Cuba kwa ukarimu walioonyesha kwa ujumbe wa Tanzania kwa muda wote waliokuwepo katika Taifa hilo.
“Rais Samia Suluhu Hassan anawashukuru kwa maandalizi yote mliomwandalia, lakini kwa neema hii tunaamini ziara ya mkuu wetu wa nchi hapa Cuba itafanyika siku za usoni,” amesema.
Kongamano hilo lilipangwa kuhudhuriwa na Rais Samia lakini ilishindikana kutokana na kuchafuka kwa hali ya hewa iliyoikumbuka mji wa Havana iliyosababisha ndege kushindwa kutua.