Mwanza. Ikiwa imepita siku moja tangu wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kuteua wagombea uenyekiti kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024, mapokezi ya teuzi hizo yametofautiana baina ya vyama vya siasa, vingine vikifurahia na vingine vikilia kuchezewa rafu katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Baadhi ya vyama ambavyo viongozi wake wamezungumza na Mwananchi leo Jumamosi Novemba 9, 2024, vimeridhishwa na uteuzi huo kwa kuwa wagombea wao wote wameteuliwa, huku vingine vikilia hujuma iliyosababisha wagombea wao kutoteuliwa.
Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF) Mkoa wa Mwanza, Idd Kiula amesema waliweka wagombea katika mitaa 31 na wote wameteuliwa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi mkoani humo.
Amesema hadi sasa kwenye chama hicho hawajapokea malalamiko kutoka kwa wateule wao, ameongeza kuwa wasimamizi wa wakati huu wanafanya kazi nzuri.
Makamu Mwenyekiti wa UPDP Mkoa wa Mwanza, Mwamini Ramadhani amesema wagombea 12 waliojaza fomu kuwania nafasi ya uongozi wa serikali za mitaa, wote wameteuliwa na kuwa mpaka sasa hawajapokea changamoto yoyote.
Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia Makini mkoani humo, Juma Mshana amesema wagombea wake wote zaidi ya 40 kutoka Wilaya ya Nyamagana na Ilemela wameteuliwa kuwania nafasi za uongozi wa Serikali za Mitaa huku Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana bila ya kutaja idadi, akisema wagombea wao wote wameteuliwa kuwania nafasi hizo.
Naye, Katibu wa Chadema Mkoa wa Geita, Sud Mtenyagala amesema mchakato kwa upande wao unaenda vizuri na hadi sasa ni kijiji kimoja pekee ambacho mgombea wao amekataliwa.
“Kule Bukombe, kijiji kimoja cha Nachirukuru ndio wagombea wetu wameenguliwa kwa madai hawajakidhi vigezo, lakini maeneo mengine mchakato unaendelea vizuri,” amesema.
Alipoulizwa idadi ya wagombea walioidhinishwa na chama kugombea, amesema kwa sasa hana idadi kamili.
Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi mkoani Mwanza, Ramadhani Amran amesema zaidi ya wagombea 16 katika Wilaya ya Magu, hawajateuliwa sababu ikitajwa kuwa wamedhaminiwa na ngazi ya chama isiyo sahihi.
“Jimbo la Magu, wagombea karibu 16 hawajateuliwa…wamejaza fomu, wamerudisha na walidhaminiwa na ngazi ya wilaya ya chama lakini sasa hivi tunashangaa wameenguliwa hawakuteuliwa, sababu ya kutowateua wanasema ngazi ya chama iliyowadhamini siyo yenyewe,” amesema.
Ameongeza kuwa wilaya zingine ikiwemo Ilemela, wagombea wao wote sita wameteuliwa na Nyamagana wanne wameteuliwa na walidhaminiwa na ngazi ya wilaya ya chama.
“Kikanuni na kimaelekezo ni kwamba ngazi yoyote ya chama inaweza kudhamini mtu, lakini muhuri huohuo majimbo mengine wameteuliwa…tumechukua hatua ya kujaza mapingamizi,” amesema Amran.
Katibu wa CUF Wilaya ya Geita, Severin Malugu amesema licha ya kuweka wagombea kwenye nafasi za uchaguzi kuanzia mitaa, vijiji na vitongoji, baadhi ya wagombea wameenguliwa kwa madai kuwa hawana sifa.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan, alianzisha falsafa ya 4R kwa lengo la kuweka usawa kwenye vyama, lakini kinachofanywa na wasimamizi wa uchaguzi ni ubabaishaji unaoua demokrasia.
“Msimamizi wa uchaguzi ameondoa majina ya wagombea kwa madai wadhamini wameandika majina mawili badala ya matatu na ukiangalia sababu za pingamizi hii haipo ni uonevu tuu,” amesema.
Malugu amesema tayari wamewasiliana na Mkurugenzi wa Wilaya ya Geita aliyewataka waandike barua za kuweka pingamizi, jambo walilolitekeleza na sasa wanasubiri kuona utekelezaji.
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Shinyanga, Hamis Ngunila amesema majina mengi ya wagombea wao yamekatwa, kitendo ambacho kimewasikitisha kutokana na kunyimwa haki yao ya msingi.
Amesema katika kata ya Mjini na Mwawaza, majina yote ya wagombea yamekatwa na maeneo mengine kwenye baadhi ya mitaa majina yamekatwa ikiwemo mitaa ya kata ya Chibe, Ibadakuli na Kizumbi.
Amesema kutokana na hali hiyo tayari wameshaandika pingamizi kupinga hatua ya majina ya wagombea wao kukatwa, akieleza kuwa mfumo uliotumika hauko sawa kwani hautendi haki.
Akizungumzia mwenendo wa uteuzi mkoani Simiyu, Mwenyekiti wa Chadema mkoani humo, Mussa Onesmo amesema sehemu kubwa ya wagombea wao, wameondolewa kwa njia zisizo za haki ikiwemo mashinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Serikali.
Hata hivyo, amesema wamewataka wagombea wao walioathiriwa na uamuzi huo kukata rufaa ili kulinda haki zao.
Ameongeza kuwa katika Willaya ya Maswa kata za Shishiyu, Sukuma na Badi, wagombea wao wote wameondolewa bila sababu za msingi na baadhi ya fomu za wagombea wao wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata, wamefuta muhuri wa udhamini wa Chadema uliogongwa katika fomu ya mgombea.
“Wagombea wetu wanaenguliwa kihuni tu katika kijiji cha Mwaliga, Wilaya ya Maswa katika jimbo la Maswa Magharibi mgombea wetu wa nafasi ya uenyekiti wa kijiji ameenguliwa kwa fomu yake aliyowasilisha kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata kufutwa muhuri wakati nakala yake ikiwa na muhuri, mchezo huo unafanywa na hao wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi,” amesema Onesmo.
Amesema kwa sasa hawalali, wanapambana kuhakikisha wagombea wao wote walioondolewa bila kufuata utaratibu wanarejeshwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa aliwataka wagombea ambao hawajateuliwa na wana mapingamizi wayawasilishwe ndani ya siku mbili tangu uteuzi ulipofanyika jana Novemba 8, 2024 ambayo yatatolewa uamuzi ndani ya siku mbili.
Imeandikwa na Saada Amir (Mwanza), Rehema Matowo (Geita), Hellen Mdinda (Shinyanga) na Samuel Mwanga (Simiyu).