Dar/Mtwara. Vyama vya siasa vya upinzani vimemuangukia Rais Samia Suluhu Hassan, vikimuomba kuingilia kati kuhusu kuenguliwa wagombea wake katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu.
Jana Ijumaa Novemba 8, 2024 baada ya Tamisemi kuweka orodha ya wagombea walioteuliwa kuwania nafasi hizo, vyama vya upinzani vililalamika kwamba wagombea wao wameenguliwa kwa sababu walizodai hazina mashiko.
Vyama hivyo, vimemsihi Rais, kuingilia kati ili kunusuru hali kwa kuelekeza wasaidizi wake kuvitendea haki vyama vya upinzani ambavyo kwa asilimia kubwa wagombea wao wameenguliwa tofauti na wale wa chama tawala CCM.
Vyama vya upinzani vimefananisha hali hiyo na ile iliyojitokeza mwaka 2019, licha ya Rais Samia kupitia vikao vya maridhiano kueleza kwa nyakati tofauti kuhusu kutofurahishwa na utaratibu wa kuwaengua wagombea kwa sababu zisizo na uzito na kutaka haki itendeke.
Katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2019, CCM ilishinda zaidi ya asilimia 90, huku baadhi ya vyama vya upinzani vikijitoa na vingine vikiulalamikia mchakato vikidai haukuwa na usawa.
“Tunatoa rai kwa Rais Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo ili wagombea wetu na wa vyama vyote vya upinzani walioenguliwa warejeshwe.
“Wagombea wengi walioenguliwa hawajaenguliwa kwa sababu zenye mashiko kisheria, bali wameondolewa kisiasa, jambo linalopaswa kutatuliwa kisiasa,” amesema Dorothy Semu, ambaye ni Kiongozi wa ACT-Wazalendo alipozungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo Novemba 9, 2024.
Semu amesema wamesikitishwa na hatua ya wagombea wao kuenguliwa kwa sababu ACT-Wazalendo, ilifanya maandalizi makubwa wakitambua kuwa uchaguzi utakuwa bora na kukiweka chama hicho kwenye ramani nzuri ya kisiasa, kutokana na uwekezaji uliofanyika baada ya mwaka 2020.
“Taarifa zilizokusanywa na timu yetu ya uchaguzi zinaonyesha zaidi ya asilimia 60 ya wagombea wetu nchi nzima wameenguliwa,” amesema.
Amewasisitiza wanachama ACT-Wazalendo kuchukua hatua kwa kuandika barua kupinga kuenguliwa.
Semu amesema kupitia mikutano mingi ya maridhiano ACT-Wazalendo iliyoshiriki kwa nyakati tofauti walitarajia mambo yangebadilika lakini imekuwa tofauti, hivyo chama hicho kinatoa rai kwa Rais Samia kuingilia kati.
Katibu Mkuu wa Chama cha DP, Abdul Mluya amesema chama hicho kinamuomba Rais Samia kuingilia kati sintofahamu hiyo na kutoa maelekezo kuhusu suala hilo, ambalo limekuwa kilio kwa vyama vya upinzani.
“Rais Samia amwambie Waziri wa Tamisemi (Mohamed Mchengerwa), kuwa wagombea wasienguliwe kwa sababu zisizo za msingi.
“Mfano leo unaambiwa mgombea ameenguliwa kwa kigezo muhuri wa chama, tunajiuliza hadi achukue fomu si chama husika ndicho kimemdhamini? Haya ndiyo yaliyoyalalamikiwa pia katika kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa,” amesema.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Magdalena Sakaya kupitia taarifa kwa vyombo vya habari amesema kwa hali inavyoendelea kwenye uchaguzi, chama hicho hakioni tofauti baina ya ‘zama za maridhiano’ na hali ilivyokuwa kabla.
“Tunatoa wito kwa Rais kuunusuru uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kwa kuiagiza Tamisemi iwarudishe wagombea wote wa upinzani walioenguliwa kwa hila,” amesema.
Kwa mujibu wa Sakaya, asilimia zaidi ya 70 ya wagombea wa CUF ambao fomu zao zilipokewa kwa ajili ya uteuzi wameenguliwa.
“Wapo walioenguliwa kwa kutobandika picha hali ya kuwa hilo si hitaji la kikanuni kwa uchaguzi wa mwaka huu,” amesema.
Chama cha Mapinduzi (CCM) katika taarifa kwa umma iliyotolewa jana Novemba 8, kiliitaka Tamisemi kutenda haki kwa vyama vyote vilivyosimamisha wagombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.
“Nitume nafasi hii kuwaomba Tamisemi watende haki kwa CCM na vyama vingine vyote. Tunaamini uchaguzi utakuwa huru na haki na atakayeshinda kwa haki, atangazwe,” alisema Amos Makalla, ambaye ni Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM.
Hata hivyo, Waziri Mchengerwa akizungumza na wanahabari jana alivitaka vyama hivyo, kuacha kulalamika pembeni badala yake wafuate utaratibu uliowekwa kuwasilisha malalamiko yao kwenye mamlaka husika ili yafanyiwe kazi.
Mchengerwa alisema hawategemei mtu yeyote kuonewa katika uchaguzi huo kwa sababu misingi yake ni Katiba na kanuni za uchaguzi zilizoeleza nini cha kufanya kwa wagombea wasioridhika na wale walioridhika na uteuzi.
Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi ya Tamisemi, uwasilishaji wa pingamizi kuhusu uteuzi ulianza jana Novemba 8 na unahitimishwa leo Novemba 9, huku uamuzi wa pingamizi hizo utahitimishwa kesho Novemba 10.
Wakati huohuo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitaka Serikali kuwachukulia hatua baadhi ya watendaji wanaodaiwa kufunga ofisi ili kukwepa kupokea barua za pingamizi.
“Jana (Novemba 8) Waziri wa Tamisemi (Mchengerwa) alitangaza wasioridhika wakate rufaa, lakini taarifa tulizozipata baadhi yao wamefunga ofisi za mitaa, vitongoji na vijiji,” amesema John Mrema, ambaye ni Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema.
Katika hatua nyingine, madiwani 10 wa vyama vya upinzani katika Halmashauri ya Mtwara Vijijini wamesusia kikao cha baraza la madiwani kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa uteuzi wa wagombea wa upinzani.
Katika maelezo yao, wamesema hawakubaliani na uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi wa halmashauri hiyo, aliyewaengua baadhi ya wagombea uenyekiti kwa madai ya kujaza fomu vibaya.
Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika Novemba 8, diwani wa Ndumbwe, Abdul Mahupa amesema wamechukua hatua ya kususia kikao kutokana na uteuzi wa wagombea kugubikwa na sintofahamu.
“Mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa haukuwa wa haki tunaondoka na kuacha kikao hiki, tunakwenda kusimama na wananchi na kumfahamisha mwenyekiti (Profesa Ibrahim Lipumba) kwamba hatujaridhishwa.
“Hatuwatendei haki katika uchaguzi huu, licha ya wananchi walijitokeza kujiandikisha lakini haki haijatendeka kwa wagombea ndiyo tumelazimika kujiondoa,” amesema Mahupa.
Diwani wa Nanguruwe (Chadema) Patrick Simwinga amesema: “Watu waliotumia haki yao ya kidemokrasia na nguvu zao za kuwa sehemu ya uchangiaji wa michango ya maendeleo kwenye vijiji vyao ya kuwa wenyeviti na wajumbe lakini wanaenguliwa bila sababu hii si sawa.”
Katibu wa ACT-Wazalendo Mtwara Vijijini, Hamisi Likwenda ameunga mkono madiwani wa upinzani kususia kikao hicho akidai demokrasia hakuna katika mchakato wa uteuzi wa wagombea.
“Kwa hali ilivyo kwa kweli tumefikia pabaya na tutatoa tamko kwa nchi nzima, hii hali si nzuri hatutakubali,” amesema.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mtwara Vijijini, Abdallah Makame amekosoa kitendo cha madiwani hao kutoshiriki kikao, akisema ni utovu wa nidhamu akiwataka warudi kwenye viti vyao.
“Jazba unajua haijengi inabomoa uchaguzi uko nje ya kikao hiki, hatujapata taarifa yoyote inayohusu uchaguzi, ni vema wangetafuta majibu kupitia maswali ya papo kwa hapo walichofanya ni utovu wa nidhamu,” amesema Makame.
Msimamizi Mkuu wa uchaguzi wa serikali za mitaa katika Halmashauri ya Mtwara, Abeid Kafunda amesema bado hajapokea malalamiko yoyote kutoka kwa wagombea walioenguliwa katika vijiji 110.
Kafunda amesema wapo walioondolewa lakini wapo waliofanya vizuri na wakapitishwa kwa ambao wana malalamiko wayafikishe ofisini.
“Niwasihi viongozi wa vyama vya upinzani, wanapokuwa na malalamiko, kuwasiliana na maofisa wa uchaguzi ili kuhakikisha mchakato unafanyika kwa amani na haki,” amesema.