Miongoni mwa wasiwasi ni uwezekano wa utawala wa Trump kupunguza mchango wa Marekani kwa umoja huo na kuiondoa tena Marekani kwenye mkataba wa kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi.
Trump alipoibuka mshindi dhidi ya makamu wa rais Kamala Harris, mwanadiplomasia mmoja wa ngazi ya juu wa Asia alisema kulikuwa na hali ya “hofu fulani” kwenye umoja huo wenye nchi wanachama 193.
Hata hivyo mwanadiplomasia huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema “pia kuna matumaini kuwa utawala ujao utashirikiana na Umoja wa Mataifa kwenye baadhi ya masuala hata kama itaondoa au itapunguza ufadhili akihoji hakuna jukwaa jingine kubwa na bora zaidi kuliko Umoja wa Mataifa.
Kulegea kwa Marekani katika Umoja wa Mataifa kunaweza kufungua mlango kwa China, ambayo imekuwa ikijenga ushawishi wake duniani kidiplomasia.
Je Trump atapunguza ufadhili wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa?
Miongoni mwa wasiwasi mkubwa katika Umoja wa Mataifa ni ikiwa Marekani itaamua kuchangia fedha kidogo kwa umoja huo na ikiwa itajiondoa katika taasisi na mikataba muhimu ya kimataifa, ikiwemo Shirika la Afya Duniani na mkataba wa Paris wa kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi.
Wasiwasi wa moja kwa moja ni ufadhili wa Marekani. Washington ni Mchangiaji mkubwa zaidi wa Umoja wa Mataifa huku Uchina ikichukua nafasi ya pili kwa asilimia 22 ya bajeti kuu ya Umoja wa Mataifa na asilimia 27 ya bajeti ya kulinda amani.
Mara ya kwanza Trump alipoingia madarakani, aliahidi kupunguza theluthi moja ya mchango wa nchi yake kwenye juhudi za kidiplomasia na misaada, hali iliyosababisha upungufu mkubwa wa ufadhili kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa.
Unaweza kusoma pia: Trump amteua Susie Wiles kuwa Mtendaji Mkuu wa Ikulu
Unaweza kusoma pia: Biden awataka Wamarekani “kutuliza joto la kisiasa”
Msemaji wa Umoja wa Mataifa alisema wakati huo kwamba mapendekezo ya kupunguza bajeti yangeathiri pakubwa utekelezaji wa miradi katika umoja huo.
Lakini baraza la wawakilishi ambalo huamua bajeti ya serikali ya shirikisho la Marekani, lililizuia pendekezo hilo la Trump.
Umoja wa Mataifa umejiandaa vipi kukabili hatua ambazo Trump anaweza kuchukua
Kulingana na Richard Gowan, mkurugenzi wa taasisi ya kukabili migogoro, kwa muda sasa, sekretarieti ya Umoja wa Mataifa imekuwa ikitarajia uwezekano wa kurejea kwa Trump madarakani. Kwa hivyo kumekuwa na baadhi ya mipango ya nyuma ya pazia ya jinsi ya kudhibiti uwezekano wa kupunguzwa kwa ufadhili kutoka Marekani, kwa hivyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na timu yake hawajajiandaa vya kutosha, lakini wanafahamu kwamba hali itakuwa ngumu sana mwaka ujao.
Timu ya Trump haikuweza kuyajibu maswali mara moja kuhusu itakayokuwa sera yao kuhusu Umoja wa Mataifa punde itakapochukua Madaraka mwakani.
Katika muhula wake wa kwanza, Trump alilalamikia ukosefu wa usawa, kwamba Marekani imeubeba mzigo mkubwa wa gharama za Umoja wa Mataifa na alishinikiza mageuzi.
Wakati wa muhula huo wa kwanza Trump alitangaza mipango ya kujiondoa katika shirika la Afya DUniani WHO. Aidha aliiondoa Marekani katika Baraza la Haki za Binadamu, katika shirika la utamaduni UNESCO, aliiondoa Washington kwenye mkataba wa Paris kuhusu udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi na pia katika mkataba wa kimataifa kuhusu mipango ya nyuklia ya Iran.
Wakati wa kampeni zake, timu ya Trump iliahidi kuiondoa tena Marekani kwenye mkataba wa mabadiliko ya tabia nchi.
Baada ya uchaguzi wa 2020, Biden alipoingia mamlakani alisitisha uamuzi wa kuitoa Marekani katika Shirika la Afya Duniani na vilevile aliirejesha Washington kwenye mikataba ya Paris na UNESCO.
(Chanzo: RTRE)