Dar es Salaam. Baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tamisemi, wameutaka uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuweka mikakati ya kulipendezesha jiji hilo, ikiwa pamoja na ujenzi wa miundombinu na kuweka taa za barabarani na kwenye majengo.
Wameyasema hayo leo Novemba 9, 2024 walipokuwa wakitembelea miradi inayotekelezwa Kituo cha Ubia wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), jijini hapa.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi amesema licha ya Dar es Salaam kuwa jiji la kibiashara, bado halijapewa kipaumbele.
“Ukiacha Dodoma ambayo ni makao makuu ya nchi yetu, Dar es Salaam ndio mji mkuu wa biashara, hivyo ikifanya vizuri Tanzania tumefanya vizuri.
“Ukienda Burundi au Malawi, wao wanaona Kariakoo tu, sasa kwa nini tusiipendezeshe? Unapotoka nchi za watu unaingia Dar es Slaam, unajisikia vibaya,” amesema.
Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba ameshauri Kamishna wa PPP, David Kafulila ayatangaze baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuvutia uwekezaji.
“Kule Kinondoni kuna maeneo mazuri, pale kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya, Magomeni Kota sasa limejengwa nyumba za watu kuishi, hebu kamati hii ipendekeze eneo lile lifanye shughuli ya kusaidia uchumi wa Tanzania, sio kukaa tu, linaweza kuwa na mall (maduka makubwa),” amesema na kuongeza;
Mbunge wa Mlimba, Godwin Kunambi amesema licha ya Dar es Salaam kuwa jiji muhimu la biashara, bado halijapewa kipaumbele kwa miundombinu.
“Mkoa wa Dar es Salaam ndio muhimu, lakini kwenye miundombinu bado kuna changamoto. Hatutarajii leo barabara inajengwa kesho, Dawasa (Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira) wanachimba, umeme unapita wapi, gesi inapita wapi? Jiji letu linakuja kuwa na treni za abiria, hayo ni mambo ambayo wataalamu wetu wanapaswa kushauri,” alisema.
Kunambi pia alishauri Sheria ya PPP kutumika katika halmashauri zote ili kuiwezesha miradi ya maendeleo kuwa na uratibu wa pamoja.
Mbunge wa Hai, Saasisha Mafue ametaka mikakati iliyowekwa kwa Jiji la Kigali nchini Rwanda itumike kupendezesha Dar es Salaam.
“Hivi kinachofanyika Kigali hakiwezi kufanyika hapa?” amehoji.
Akijibu maoni ya wabunge, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar e Salaam, Elihuruma Mabelya amesema wameweka mkakati wa kuhakikisha asilimia 10 ya mapato ya mkoa huo yanakwenda katika ununuzi wa taa za barabarani.
“Mpango wa kununua taa tumeshaupitisha kwenye vikao vilivyopita na kwa kuanzia tutanunua taa 281
Amesema pia wanakusudia kufunga kamera za usalama hasa katika maeneo ya biashara.
Awali akizungumza wakati wa kutembelea jengo la biashara unaotekelezwa kwa Sheria ya PPP na Shirika la Maendeleo la Dar es Salaam (DDC), Kamishna Kafulila alisema;
“Huu ni mradi wa kwanza kufuata Sheria ya Ubia Na.103 hatua kwa hatua mpaka kusainiwa kwa mkataba na kwa uchambuzi wangu, mkataba huu una ubora kuliko mikataba mingi.
“Nafikiri mtakuwa mmeona kwenye taarifa, kwenye ujenzi, huyu mwekezaji analipa Sh2 bilioni kila mwaka na utekelezaji utakavyoanza atalipa Sh2.5 bilioni kila mwaka, kwa sababu Kituo cha Ubia kilifika hatua moja hadi nyingine kupitia mfumo wa fedha na taratibu nyingine,” amesema.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Justin Nyamoga amesema ameshauri kuongezwa kwa uwekezaji ili kukuza biashara.
“Katika siku za karibuni tumeshuhudia ukuaji wa biashara eneo la Kariakoo si tu kwa Watanzania, bali hata kwa watu wengine kutoka nchi za jirani, hivyo tunahitaji wawekezaji kama hawa,” amesema.
Ziara hiyo pia ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tamisemi, Dk Festo Dugange.