Wabunge watoa kauli hujuma SGR

Dar es Salaam. Wabunge wameliagiza Shirika la Reli Tanzania (TRC), kufunga kamera za ulinzi mara moja maeneo yote ya reli ili kukabiliana na watu wanaohujumu miundombinu ya treni ya kisasa ya umeme (SGR).

Agizo hilo limetolewa leo Novemba 9, 2024 jijini Dar es Salaam na wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge za Miundombinu na Bajeti waliotembelea na kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa SGR.

Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Selemani Kakoso amesema kufungwa kwa kamera za ulinzi (CCTV) kutawezesha kukabiliana na hujuma kwa mradi huo.

Kauli ya wabunge imetolewa ikiwa zimepita siku nne tangu TRC kupitia Mkurugenzi Mkuu wake, Masanja Kadogosa kueleza kuna njama zinazofanywa kuhujumu mradi huo ili kuonyesha haufai.

Treni ya SGR kwa nyakati tofauti safari zake zimekuwa zikipata hitilafu za mara kwa mara jambo linalosabisha watu kukwama wakiwa katikati au kuchelewa kuanza safari wanapokuwa stesheni.

Akizungumza na Mwananchi Novemba 5, Kadogosa alisema treni ya SGR ambayo inafanya safiri kati ya Dar es Salaam, Morogoro hadi Dodoma imekuwa na changamoto za hitilafu ya umeme inayoathiri ratiba za wasafiri.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa akizungumza na Mwananchi Novemba 5, alisema kuna njama zinazofanywa kwa lengo la kuhujumu mradi huo.

Amesema hujuma hizo si za hivi karibuni, bali zimeanza muda mrefu akieleza baadhi ya wahusika wamekamatwa ambao wako mbioni kuchukuliwa hatua.

“Hatua dhidi yao zinaendelea, watakapohukumiwa wananchi watawafahamu,” alisema.

Safari ya kwanza ya treni ya umeme ilianza Juni 14, 2024 kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro ikiwa na mabehewa 14 yaliyojaa. Julai 25, 2024 treni hiyo ilianza safari za Dar es Salaam hadi Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan ndiye aliyeizindua.

Kadogosa alisema kumekuwa na sintofahamu ikiendelea, wengine wakihisi kuna mgawo wa umeme kwenye SGR.

“Kuna nyaya zilikatwa kwenye eneo la kati ya Soga na Pugu na waliofanya hivyo si vibaka, ni watu wenye nia ya kuhujumu mradi huu na wanajua walichokuwa wanakifanya.

“Kuna ambao tumeshawakamata na ushahidi upo, na hii si mara ya kwanza, hatukutaka kuwatangaza kwa sababu tulihitaji ‘tu-dili’ nao kimyakimya, hatua dhidi yao zinaendelea na watakapohukumiwa wananchi watawafahamu,” alisema akieleza hujuma ndizo zimekuwa zikiathiri safari za treni hiyo.

Kakoso amesema mbali ya kamera, uwekwe ulinzi wa mfumo wa umeme ambao wote wanaotaka kuihujumu reli hiyo wanaswe na mifumo ya umeme.

“Hii itasaidia sana kwa sababu sisi Watanzania kuna watu ambao bado hawaoni umuhimu wa kutunza hii miundombinu, ndiyo maana watu wanashuhudia mradi mkubwa unaweza kujengwa kwenye barabara, eneo lote ambalo wameweka vibao ambavyo vinawasidia hata wenyewe, wanakuja kutoa na kwenda kuuza kama chuma chakavu.

“Vitu hivi havitusaidii kwa sababu Serikali imewekeza fedha nyingi ikiwemo kuahirisha kufanya mambo mengine ili kumalisha mradi huu. Hivyo, watu wanapaswa kuelewa mradi tulionao ni wa kwetu sote Watanzania na si wa TRC peke yao,” amesema.

Kuhusu miradi ya SGR inayoendelea amesema ni vyema kujenga itakayounganisha Tanzania na nchi jirani itakayofanya sekta ya usafirishaji kupitia eneo la bandari kufanya kazi kwa ufanisi.

“Reli tunayoijenga si tu kwa ajili ya kubeba abiria, bali tunaitegemea ibebebe mzigo mkubwa kutoka nchi ya Burundi ambako kuna uchimbaji mkubwa wa madini ya nikeli.

“Tunataka iunganishwe na nchi jirani ya DR Congo ambako kuna mzigo mkubwa. Maendeleo ya reli yanategemea sana mizigo, kwa hiyo tunaiomba Serikali iunganishe katika maeneo ambayo faida itakuja kuonekana,” amesema.

TRC pia imetakiwa kuja na mpango kabambe wa kibiashara ili shirika liendelee, akieleza ilishawahi kushuhudiwa shirika lilifikia katika hali mbaya.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Oran Njeza amesema kuna haja ya kuendelea kumalizia kujenga vipande vilivyobaki kwa kutumia kile kitakachopatikana, badala ya kusubiri bajeti kutokana na umuhimu wake katika uchumi.

“Hata hivyo, wakati tunaendelea na ujenzi wa reli hii tusisahau na ile reli ya MGR (reli ya kawaida) na kujenga viunganishi muhimu vya kwenda bandarini, kwa kuwa nayo ina umuhimu wake katika kupeleka uchumi wetu kwa kasi,” amesema.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Ludovick Nduhiye kwa niaba ya waziri wake, Profesa Makame Mbarawa ameahidi watafanyia kazi maelekezo na ushauri uliotolewa na kamati hizo.

Related Posts