KATIKA misimu 13 iliyopita kuanzia 2011/12 hadi 2023/24, Yanga imejipatia historia ya kuwa klabu yenye mafanikio makubwa Ligi Kuu Bara. Hata hivyo, historia hiyo pia inaonyesha bingwa huyo mtetezi huwa katika hatari ya kupoteza ubingwa endapo atapoteza michezo miwili mfululizo.
Kitendo cha kupoteza dhidi ya Azam FC kwa bao 1-0 na Tabora United kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, kimeibua hofu kwamba historia inaweza kujirudia msimu huu wa 2024/25, kama ilivyotokea awali kwenye misimu mingine mitatu kati ya minne ndani ya kipindi cha misimu 13 iliyopita.
Yanga imewahi kupoteza ubingwa mara tatu katika miaka ya hivi karibuni baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo. Hii inatoa taswira kwamba hali kama hiyo inaweza kurejea msimu huu ikiwa hawatabadilisha mwenendo wao. Kabla ya hiki ambacho kimetokea msimu huu wa 2024/25 ambapo Yanga wamejikuta wakidondosha pointi sita kwenye michezo miwili iliyopita, Wananchi walikumbana na mazingira ya namna hii msimu wa 2019/20. Yanga ilipoteza mechi mbili mfululizo, dhidi ya Kagera Sugar kwa mabao 3-0 ambayo yalifungwa na Yussuf Mhilu, Ally Ramadhn na Peter Mwalyanzi huku wakiwa pungufu kutokana na Mohamed Issa ‘Banka’ kuonyeshwa kadi nyekundi kwenye Uwanja wa Uhuru. Katika mchezo mwingine, pia Yanga ilimaliza ikiwa pungufu dhidi ya Azam FC ambapo walipoteza kwa bao la kujifunga Ally Mtoni ambaye pia alionyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 80. Ndani ya msimu huo, Yanga iliyokuwa na pointi 72 ilishika nafasi ya pili nyuma ya Simba ambao walitwaa ubingwa wakiwa na pointi 88.
Msimu wa 2017/18, Yanga ilikumbwa na majenga mengine ya kupoteza mechi mbili mfululizo katika ligi dhidi ya Mtibwa Sugar kwa bao 1-0 kisha dhidi ya Tanzania Prisons. Bingwa alikuwa Simba, alitwaa akiwa na pointi 69, Yanga ilishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 52, Azam ilishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 58. Katika msimu wa 2014/15, Yanga ilipoteza dhidi ya Ndanda kwa bao 1-0 na Azam FC kwa mabao 2-1. Yanga ilichukua ubingwa licha ya kupoteza mara mbili mfululizo katika ligi ikiwa na pointi 55.
Msimu wa 2011/12, Yanga ilifungwa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar na Toto Africans kwa mabao 3-2. Simba ilichukua ubingwa ikiwa na pointi 62, Azam ikishika nafasi ya pili na pointi 56, Yanga ilishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 49.
Kwa upande mwingine, Yanga inakabiliwa na changamoto ya kuimarisha kikosi chake ili kurejesha kasi ya ushindani. Hii inahitaji wachezaji kujituma zaidi na benchi la ufundi kuboresha mbinu za uchezaji. Mbinu hizi ni muhimu ili kuhakikisha timu haijikuti kwenye hatari ya kupoteza nafasi ya ubingwa msimu huu.
Maandalizi ya kimkakati ni muhimu sana kwa Yanga ili kuweza kurejea katika kasi ya ushindi. Kocha na wachezaji wanahitaji kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha hawarudii makosa yaliyowahi kuwagharimu katika misimu ya nyuma. Pia, nidhamu ya uchezaji na umoja ndani ya timu ni mambo ya msingi yatakayoweza kuisaidia Yanga kurudi katika mbio za ubingwa.
Ni wazi kuwa kipigo mfululizo kinapunguza morali ya wachezaji na huongeza shinikizo kwa benchi la ufundi. Hali hii hupelekea mashabiki kupoteza matumaini na kuleta mvurugano ndani ya klabu. Hivyo, ni jukumu la uongozi kuhakikisha kuwa wanawapa wachezaji na benchi la ufundi mazingira bora ya kushinda michezo yote iliyobaki.
Kocha wa zamani wa Yanga, Luc Eymael alisema: “Yanga inahitaji kujiamini na kucheza kwa utulivu hata inapoanguka. Kocha na wachezaji wanatakiwa kufahamu ligi ni ngumu na mechi inaweza kugeuka kuwa changamoto, hasa unapokuwa mtetezi. Mara nyingi timu zinajituma zaidi na hii inahitaji maandalizi ya hali ya juu na mbinu.
“Kupoteza mara mbili mfululizo kwa timu kubwa kama Yanga kunapaswa kuchukuliwa kama kengele ya tahadhari.”