Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, imemhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa Lameck Mpembe, mkazi wa kijiji cha Namansi, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya mtoto wake wa kambo, Maria Thomas aliyekuwa na umri wa miezi 11.
Mpembe alishtakiwa kwa kosa la mauaji, kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu na alidaiwa kumuua Maria Julai 6, 2022, katika kijiji hicho.
Hukumu hiyo ilitolewa Novemba 8, 2024 na Jaji Thadeo Mwenempazi na nakala yake imewekwa kwenye tovuti ya mahakama.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Mwenempazi alisema kutokana na ushahidi wa mazingira pamoja na kukiri kwa mshtakiwa, Mahakama hiyo imemkuta na hatia na imemhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Jaji alieleza kuwa hakuna mtu aliyeshuhudia tukio hilo moja kwa moja, lakini mashahidi wa pili na wa tano walimsikia mshtakiwa akikiri kutenda kosa hilo wakati anahojiwa.
Jaji alisema ushahidi wa shahidi wa pili, wa nne na wa tano wakiwa eneo la tukio, walisema mshtakiwa alikiri kwa mdomo wake kumuua mtoto huyo kwa kumnyonga shingoni na kuonyesha nguo ya ndani aliyokuwa amevaa ambayo ilikuwa na haja kubwa.
Akitoa hukumu hiyo, Jaji alisema amezingatia hoja za pande zote mbili na kimsingi, kesi hiyo kwa kiasi fulani inategemea mazingira ya ushahidi wa kimazingira na kukiri kwa mshtakiwa mwenyewe mbele ya shahidi wa pili, wa nne na wa tano wakiwa eneo la tukio na pia wakati akiandika maelezo ya onyo.
Huku akinukuu kesi ya rufaa ya jinai namba 281 ya mwaka 2020 ya Halfan Mohamed dhidi ya Jamhuri iliyoeleza ushahidi bora zaidi katika kesi yoyote ya jinai, ni mshtakiwa ambaye anakiri hatia yake kwa uhuru.
“Kwa mazingira na sababu zilizoonyeshwa katika hukumu hii hapa juu, bila shaka yoyote nina imani kuwa mshtakiwa anahusika kumuua Maria,” alisema jaji huyo.
Kuhusu iwapo mshtakiwa alikuwa na ubaya kabla ya kumnyonga Maria, Jaji Mwenempazi alisema mtuhumiwa alisimulia kilichojiri kwa maneno yake mwenyewe, kwanza alihakikisha mama wa mtoto yuko mbali na mtoto, kisha akamnyonga.
Jaji Mwenempazi alisema mshtakiwa alidai katika mchakato huo, mtoto alijisaidia, kisha akachukua nguo zilizochafuliwa akazitundika
ukutani na ili kuficha kilichotokea, alimlaza mtoto kitandani, “Hatua zote hizi zinathibitisha mshtakiwa alidhamiria kuua.
“Hivyo, kwa maoni yangu, ni wazi mshtakiwa alikuwa na nia mbaya kabla ya kutimiza mauaji ya Maria, kwa sababu hizo naona ushahidi uliotolewa unamhusisha mshtakiwa na mauaji ya Maria moja kwa moja, hivyo amekutwa na hatia na atahukumiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu,” alisema jaji huyo.
Akisoma hukumu, Jaji alisema chini ya kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu, kuna sentensi moja tu, “mtu anayepatikana na hatia ya mauaji atahukumiwa kifo, hivyo mtuhumiwa naye anahukumiwa kifo kwa kunyongwa hadi kufa,”alieleza Jaji huyo.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watano na vielezo viwili na uliwakilishwa na mawakili wawili wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Xaveria Makombe, huku mshtakiwa huyo akitetewa na Wakili Samwel Kipesha.
Shahidi wa kwanza, Reginaldo John alieleza kuwa yeye ni mkazi wa kijiji hicho na alikuwa akifanya kazi katika moja ya mashamba yanayomilikiwa na Editha Fredrick ambako mshtakiwa na mkewe (Rozalia) walikuwa wakifanya kazi pia.
Alidai siku ya tukio wakiwa katika moja ya kambi zilizopo shambani hapo mbali kidogo na alipokuwa akiishi mkewe, Mpembe alikuwa akimpeleka mkewe hospitali saa sita mchana na gari.
Shahidi alidai walipopita kambini, mshtakiwa aliomba msaada wa kumpeleka mkewe hospitalini. Walipouliza kuhusu mtoto (marehemu), hawakupata jibu.
Baada ya mshtakiwa kuondoka, shahidi aliwaomba wenzake wawili waliokuwa naye eneo hilo waende kumchukua mtoto huyo mdogo.
Alisema wenzake walipokataa, alikwenda kambini peke yake na alimkuta mtoto amelala kwenye mkeka chumbani. Alipofunua shuka, aliona mchwa wakiingia mdomoni na puani mwa mtoto, akabaini alikuwa amefariki dunia.
Alisema alirudi kuwajulisha wenzake na kumkamata mshtakiwa, kisha kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kijiji. Wakati huo, mkewe alikuwa akipelekwa hospitalini kwa bodaboda.
Shahidi wa pili, Editha Fredrick alidai siku ya tukio akiwa njiani kuelekea shambani aliiona bodaboda ikiwa imembeba Rozalia na Reginaldo, na walipomkaribia walimweleza kuwa shambani kuna tatizo, mtoto wa Rozalia amekufa na Mpembe anashukiwa kuhusika.
Alidai kuwa alirudi kijijini akatoa taarifa kwa polisi nao wakafuatana naye hadi eneo la tukio wakauchukua mwili wa mtoto na kuupeleka kituo cha afya Kirando.
Alidai Julai 7, 2022, mshtakiwa alikiri kumuua mtoto huyo kwa kumkaba koo na alijisaidia haja kubwa wakati wa tukio hilo.
Alidai mshtakiwa alikuwa amemuacha mke wake eneo lingine nje ya nyumbani kwao ili atekeleze mpango wa kumuua mtoto huyo.
Shahidi wa tatu ambaye ni daktari aliyeufanyia mwili wa marehemu uchunguzi, Catherine Kimaro alisema alibaini kuwepo na dalili za baridi na ukakamavu wa misuli na kifo hicho kinaweza kuwa kilitokea kati ya saa 28 hadi 32 zilizopita.
Alisema pia uchunguzi ulibaini nguo za mtoto zilikuwa na haja kubwa, shingo yake ilikuwa imelegea na alifariki kwa kukosa hewa baada ya kunyongwa.
Shahidi wa nne ambaye ni mama wa mtoto, alisema Mpembe ni mumewe na walikuwa wakiishi na kufanya kazi katika shamba la Editha, siku ya tukio alikuwa anaumwa akamuomba mshtakiwa ampikie uji.
Alidai baada ya kuona anazidiwa alimuomba ampeleke hospitali ila amsaidie kumbeba mtoto, lakini mumewe (Mpembe) alikataa.
Rozalia alidai wakati wanaelekea hospitali, walifika sehemu mshtakiwa alimlaza chini na kumwambia amsubiri hapo, anaenda kumfuata mtoto ila alirudi bila mtoto na kumjulisha kuwa ameahirisha na atawaomba majirani warudi kumchukua.
Alidai mahakamani hapo kuwa walipokaribia kambi aliyokuwa akiishi Reginaldo na watu wengine, waliomba msaada wa kupelekwa hospitali na shahidi huyo wa kwanza alisisitiza kumchukua mtoto huyo na kwa bahati mbaya alipokwenda akakuta mtoto amekufa.
Shahidi wa tano ambaye ni askari polisi, Koplo Masunga aliandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa ambayo yalieleza mshtakiwa akiwa njiani kumpeleka mkewe hospitalini, alimuacha barabarani na kurejea kambini kumchukua mtoto.
Katika maelezo hayo, mshtakiwa alidai alipofika nyumbani alimkuta mtoto sebuleni, akamchukua na kumpeleka chumbani alikokwenda kumnyonga.
Baada ya kuthibitisha kuwa mtoto ameshakufa, alimlaza chini na kumfunika kwa shuka la kimasai, kisha akaondoka kumfuata mkewe aliyemuacha njiani.
Mshtakiwa alidai alipoulizwa na mkewe kuhusu alipo mtoto, alimjibu kuwa amemuacha ndani.
Hata hivyo, alipokuwa akijitetea mahakamani, Mpembe alikana maelezo hayo na kudai alipelekwa eneo la tukio na kulazimishwa kukiri kosa hilo kwa kupigwa.