Basi la abiria lagonga treni Kigoma, 14 wajeruhiwa

Dar es Salaam. Abiria 14 wamejeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Classic linalofanya safari zake kati ya Kigoma na Dodoma kugonga treni ya mizigo.

Ajali hiyo imetokea usiku wa Novemba 09, 2024 katika makutano ya reli na barabara kati ya Malagarasi na Nguruka, mkoani Kigoma ikihusisha treni ya mizigo Y611 iliyokuwa ikitoka Kigoma kwenda Tabora na basi hilo.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Jumapili na Shirika la Reli Tanzania (TRC), chanzo cha ajali ni dereva wa basi kulipita kwa kasi basi lingine lililokuwa limesimama kupisha treni, hivyo kusababisha ajali hiyo.

“Ajali hii ilisababisha mabehewa matano kati ya 30 kuanguka, pia abiria 14 kati yao wanawake nane na wanaume sita waliokuwa wakisafiri na basi hilo wamepata majeraha madogo na hakuna abiria aliyepoteza maisha,” imeeleza taarifa hiyo.

Kutokana na tukio hilo, TRC imewataka madereva na watumiaji wa barabara kufuata sheria na kuheshimu vivuko vya reli vilivyowekwa, ili kuhakikisha ajali zinazoweza kuepukika zinazuiwa.

“Shirika la Reli Tanzania linawapa pole kwa majeruhi na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano, Fredy Mwanjala.

Ajali hiyo imetokea ikiwa zimepita siku 73 tangu ajali nyingine ya treni kuripotiwa kutokea Agosti 28, 2024.

Ajali hiyo ilihusisha treni ya abiria iliyokuwa ikitokea mkoani Kigoma kuelekea mikoa ya Tabora, Dodoma, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam ambayo ilijeruhi watu 70 kati ya 571 waliokuwa wakisafiri kwa treni hiyo.

Taarifa iliyotolewa na aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TRC, Jamila Mbarouk ilieleza, “ajali imetokea baada ya mabehewa sita ya treni kuacha njia na kusababisha majeruhi 70, wanawake 26 na wanaume 44. Treni ilikuwa na jumla ya abiria 571 wakisafiri kutoka Kigoma kuelekea mikoa ya Tabora, Dodoma, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.”

Related Posts