Dar/Mikoani. Uanzishaji wa viwanda vya kurejeleza vyuma na kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwamo nondo, umeongeza mahitaji ya chuma chakavu mitaani.
Hali hiyo imewafanya watafutaji wa bidhaa za vyuma kutumia mbinu mbalimbali zikiwemo za kihalifu –wizi wa miundombinu barabarani, vifaa vya majumbani na uvunjaji wa misalaba makaburini.
Si ajabu kupita maeneo ya barabarani na kuona vyuma vya madaraja, kingo za barabara, alama au mifuniko ya chemba vikiwa vimeng’olewa.
Hata kwenye majumba, nondo na vitu vingine vyenye asili ya chuma vinabwebwa na kuuzwa kama chuma chakavu.
Uhalifu unaohusisha biashara hiyo, unaelezwa na Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), kuwa unasababisha hasara kubwa kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa.
Kutokana na hali hiyo, mara kadhaa viongozi na makanda wa Jeshi la Polisi wamesikika wakiwaonya wanaojihusisha na uhalifu huo, kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Katikati ya wizi huo, wanunuzi wa vyuma chakavu na taka ngumu wameeleza ugumu wa kutambua kama bidhaa wanazouziwa ni za wizi au la, hali waliyosema inawaweka mtegoni katika biashara hiyo kubwa nchini na duniani.
Baadhi ya metali zinazouzwa na bei zake rejareja ni pamoja na shaba ambayo kilo moja huuzwa kwa Sh15,000, chuma Sh900, chuma ‘cast’ Sh2,500, aluminiamu Sh3,000, brass Sh8,000, chuma aina ya fufu Sh700, zinki Sh1,500, rejeta Sh4,000, chuma kisichopata kutu (stainless) Sh7,000.
Mbali na vyuma chakavu, biashara ya vitu vyenye asili ya plastiki nayo imekuwa kero kwani nayo inasababisha wizi wa vifaa vya majumbani kama mabeseni, ndoo, madumu na wakati mwingine hadi matenki, ambavyo huuzwa kwa viwanda vya urejelezaji wa bidhaa za plastiki.
Tukio la karibuni la uhalifu wa aina hiyo ni la kuvunja misalaba iliyowekwa kwenye makaburi ya Kola, mkoani Morogoro. Zaidi ya makaburi 50 yaliharibiwa.
Hatua hiyo imesababisha ndugu wa marehemu waliozikwa kwenye makaburi hayo kushindwa kuyatambua, huku wengine wakiingia hasara ya kuweka misalaba mingine.
Hii ni mara ya pili kutokea kwa matukio hayo ya kuibwa misalaba katika eneo hilo, ikidaiwa wahusika wanakwenda kuuza nondo na kingo za aluminiamu kama chuma chakavu.
Hili si tukio la Morogoro pekee, limewahi kutokea katika mingine kadhaa, hasa Tabora, Shinyanga, Dodoma, Mwanza, Mbeya na maeneo mengine.
Licha ya kuwa maficho ya wahalifu, biashara ya vyuma chakavu kwa upande mwingine, inatajwa kusaidia katika usafi wa mazingira kwa kufanya urejelezaji wa taka hatarishi na kuingiza fedha za kigeni baada ya kuuzwa nje ya nchi.
Utafiti uliofanywa na wanazuoni Clashon Onesmo, Edmund Mabhuye na Patrick Ndaki wenye kichwa cha habari, Uhusiano kati ya usimamizi endelevu wa taka ngumu na hali ya uchumi katika miji ya Tanzania: Biashara ya vyuma chakavu Arusha wa mwaka 2023, umebainisha hilo.
Suala hilo halijazungumziwa tu na wanazuoni hao, hata ripoti ya Benki ya Dunia (WB) ya mwaka 2021, inaonyesha Tanzania ilisafirisha nje ya nchi kilo milioni 8.01 za vyuma chakavu na kuingiza fedha za kigeni sawa na Sh4.6 bilioni.
Nchi zinazoongoza kununua bidhaa hizo hapa nchini ni India, ikifuatiwa na Kenya na Ujerumani.
Licha ya changamoto zake, biashara ya chuma chakavu inasimamiwa na kanuni za ufanyaji wa biashara ya chuma chakavu za mwaka 2019, kama anavyoeleza Hamadi Taimuru, mkurugenzi wa utekelezaji na uzingatiaji wa sheria katika Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
“Kanuni zinawataka wafanyabiashara wa chuma chakavu kuwa na vibali ambavyo hutolewa na NEMC baada ya kujiridhisha, atakayekiuka kanuni na taratibu anachuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutaifishwa mzigo wake,” anasema.
Akifafanunua kuhusu utaratibu huo, Taimuru anasema vibali vya kukusanya chuma chakavu vinatolewa kwa gharama ya Sh50,000 na tozo zake kwa mwaka ni kati ya Sh1.5 milioni kwa wafanyabisahara wadogo na Sh5 milioni kwa wakubwa.
“Kama mtu anaiba miundombinu na hajakamatwa inakuwa ni ngumu kujua kama ameiba wenye kibali au asiye na kibali na wakiiba wanaficha, hata ukienda katika ofisi zao huwezi kuvikuta,” amesema.
Suala hilo lilipohojiwa bungeni na Fakharia Shomar, mbunge wa Viti Maalumu, Khamis mwaka 2021, akitaka kujua Serikali imejipangaje kupambana na wizi na uharibifu huo uliokithiri, Serikali ilisema imeandaa rasimu ya muswada wa sheria ili kuweka utaratibu na mfumo wa usimamizi na udhibiti wa biashara hiyo.
Aliyekuwa Waziri wa viwanda, Biashara na Uwezakaji wa wakati huo, Charles Mwijage alisema “ili kupata suluhisho la kudumu, wizara imeandaa rasimu ya muswada huo unaodhibiti kuanzia uzalishaji, ukusanyaji, usambazaji, uuzaji na uyeyushaji wake kwa kuzingatia hifadhi na usimamizi wa mazingira kwa manufaa ya Taifa.”
Alisema miundombinu iliyoathirika ni mifumo ya kusafirisha umeme, reli, barabara na maji.
Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads), ukiwa miongoni mwa waathirika wa wizi uhalifu huo, umeeleza hasara unayoipata na njia za kuiepuka.
Mtendaji mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta amesema biashara hiyo inaathiri zaidi vyuma wanavyotumia kutengeneza nguzo za taa.
“Baada ya kuona malighafi hizo zinaibiwa zaidi, tumeamua kuja na mfumo mwingine tunatumia nguzo za zege kuweka alama za usalama barabarani na kuweka taa,” amesema.
Amesema wizi wa malighafi hizo umekithiri zaidi katika maeneo ambayo hayana watu wengi, zaidi maeneo ya mikoani, na wanashirikiana na viongozi wa serikali za mitaa kukabiliana nalo.
Anatoa mfano wa Mkoa wa Iringa kuwa waliweka taa za kurukia na kushukia ndege kwenye uwanja wa ndege lakini baada ya muda ziling’olewa.
“Hatuelewi waliong’oa walikwenda kuuza wapi. Tunapata hasara kubwa kutokana na wizi huo si wa fedha tu, hasara kubwa ni kutokea ajali kwa sababu hakuna alama zinazoonyesha alama za usalama barabarani au uwanja wa ndege,” amesema.
Ameitaja mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Morogoro na Pwani kuwa ndiyo imekithiri kwa wizi wa nguzo hicho,” amesema.
Kwa upande Meneja Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) Wilaya ya Nyamagana, Danstan Kishaka pia amesema biashara hiyo imechochea wizi wa alama za barabarani, vyuma kwenye madaraja na taa za barabarani.
“Kwa hapa Mwanza wanaiba sana vyuma vya madaraja, alama za barabarani ambazo ni vyuma na pia taa za barabarani. Mfano ukienda pale Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekouture, waraibu wa dawa za kulevya usiku hupanda kwenye taa na kuzing’oa,” anasema.
Akizungumza na Mwananchi, Mkazi wa Ilala jijini Dar es Salaam, Sadiki Khamis ameishauri Serikali kabla ya kutoa vibali vya biashara yoyote itazame kwa upana ni madhara gani yanaweza kutokea kwa kuwa biashara ya vyuma chakavu na plastiki imekuwa kero majumbani.
“Mimi kwangu hapa wameshaniibia ndoo nane, mbili nilikuwa naweka takataka na sita zilikuwa zina maua. Nimekuta wamemwaga taka na maua chini na kwenda kuuza.
“Tukitaka kupata mwarobaini wa hili jambo, ni kuwabana na kuwashughulikia wanaonunua hivi vitu, wao ndio wanachochea huu uhalifu ambao unatupa hasara uendelee. Na hata Serikali kuna miundombinu yake pia inafanyiwa hujuma,” anasema Khamis.
Mkazi wa Mbopo, Mabwepande nje ya Jiji la Dar es Salaam, Subira Nuru anaeleza namna alivyoibiwa mifuniko sita ya chemba za majitaka nyumbani kwake.
“Kuna siku niliamka na kukuta kila chemba haina mfuniko, katika kufutilia na kuwabana vijana wa jirani zangu na nilipowahoji walikubali na kuonyesha walikoenda kuiuza.
“Nikamuuliza muuzaji, wakati unanunua hukuwa na shaka na mifuniko hii imeibwa kwa kuwa ni mipya? Alinijibu alijua vijana hao wameokota na kuja kuuza kama siku zote,” alidai.
Anasema mifuniko hiyo ambayo alinunua kwa Sh60, 000 kila mmoja, ilikuwa imeuzwa kwa Sh2,000 kila mfuniko.
Mkazi wa Tabata Bima, Dar es Salaam, Theodora Sahani amesimulia namna alivyoibiwa taa na nyaya za umeme.
“Nyumba yangu ujenzi ulikuwa unaendelea na nilikuwa sijazungushia uzio. Siku moja niliamka asubuhi nikakuta taa, nyaya za umeme zimechukuliwa,” amesema.
Biashara hiyo imekuwa ikiwahusisha watoto hadi wenye umri kati ya miaka saba hadi 11 na vifaa vinavyoibiwa zaidi ni dira za maji, koki, mabati, vijiko na masufuria.
Rachel Fredy anayeishi Mtaa wa Forest, jijini Mbeya amesema awali kuliibuka wizi wa mabati, vijiko na sefuria na vitu vyenye hasiri ya chuma lakini sasa wamegeukia rasilimali za Serikali kama alama za barabarani, vivuko na dira za maji.
“Kwenye mtaa ninaoishi dira za maji zaidi ya tano zimeibwa kwa Oktoba na Novemba na uhalifu huo ufanyika usiku na kuacha maji yakimwagika,” amesema.
Akizungumza kuhusu wizi wa dira za maji, Ofisa Uhusiano na Mawasiliano Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya -UWSA), Neema Stanton amekiri kupokea malalamiko kutoka kwa wateja wanaowasambazia huduma.
“Ni kweli matukio ya wizi wa dira za maji yameripotiwa, ingawa tumeanza kuchukua hatua za ufuatiliaji kwa sasa sina takwimu sahihi za dira zilizoibiwa,” amesema.
Wanunuzi wa vyuma chakavu
Mnunuzi wa vyuma chakavu eneo la Ubungo, Dar es Salaam, Yohana Mchana ameliambia Mwananchi kuna wakati wanauziwa malighafi za wizi na hujikuta kwenye mikono ya Jeshi la Polisi.
“Mnunuzi wa bidhaa hizo kulala vituo vya polisi ni jambo la kawaida kwa sababu kuna wakati tunauziwa vitu vya wizi, kwa mfano mwenyewe nimewahi kulala polisi mara mbili niliuziwa mali ya wizi,” amesema.
Anasema ingawa masharti ya leseni zinawaelekeza kuwa mtoto haruhusiwi kupima chuma lakini mara kadhaa suala hilo hawalizingatii isipokuwa kukusanya mzigo.
Mnunuzi mwingine katika eneo la Nata jijini Mwanza, Peter Robert anasema kutokana na kazi hiyo kuwa na changamoto ya baadhi ya vyuma kuwa vya wizi, ameamua kuchagua aina ya vyuma vya kununua.
“Mimi hapa nanunua vyuma vidogo vidogo, siwezi kupokea vyuma vikubwa kwa sababu najua vinakuwa na shida na mara nyingi huwa vinatokana na wizi, ukinunua unakamatwa na mwisho wa siku unapelekwa jela,” anasema.
Anasimulia alivyonusurika kukamatwa baada ya kusingiziwa na mtoto kuwa amemuuzia chuma, hali anayosema ilimfanya kuwa makini zaidi na aina ya vyuma anavyoletewa.
“Miezi miwili iliyopita watoto walikuja na chuma kipya, mimi sikununua na niliwafukuza nikawaambia hivi vyuma mimi sinunui, wakatoka wakaenda kuuza sehemu nyingine, lakini yule mtoto alipokamatwa, nikaitwa nikaanza kuulizwa na yule mtoto akidai ameniuzia mimi wakati si kweli,” anasema.
Lakini Juma Jongo, mmoja wa wauza vyuma mjini Morogoro, anasema wao wanaletewa vyuma na vijana kutoka maeneo tofauti na hawawezi kujua vilikototwa au vimeibwa.
“Mimi nipo hapa kwenye eneo langu la biashara, vijana wanatoka huko watokako na vyuma vyao, siwezi kujua kama wameiba au la.
“Kuna wakati wanaleta vyuma ambavyo vimeshakatwakatwa, siwezi kujua kama huu ni msalaba au chuma cha daraja,” anasema Jongo.
Kauli ya Jongo za za wenzake, hazipishaji sana na ya Mawazo Sokoni, mfanyabiashara wa vyuma chakavu, mtaa wa madukani, mjini Mpanda, Mkoa wa Katavi anayeongeza kuwa changamoto nyingi kwenye biashara hiyo zinawafanya kushindwa kupata maendeleo.
Amesema mara nyingi amekuwa anakamatwa kwa makosa ya kubambikiziwa na kutozwa faini kubwa ambayo haiendani na kipato cha biashara husika.
“Tumekuwa tunapata changamoto nyingi sana sisi wauzaji wa vyuma chakavu hasa ambao mitaji yetu ni midogo, kumekuwa na ubambikizwaji wa kesi na kutozwa faini kubwa tofauti na kipato, jambo ambalo linafanya tushindwe kunufaika na biashara hii ya vyuma chakavu,” amesema.
Wakati Sokoni akisema hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani anasema katika kuhakikisha uhalifu unapungua wamekuwa na utaratibu wa kufanya misako maeneo ambayo wanakusanya vyuma chakavu na wakibaini tatizo wanawachukulia hatua za kisheria.
“Kipindi cha nyuma kulikuwa na wizi wa vyuma katika miradi ya shule, maji na ujenzi wa madaraja, tulifuatilia na baadhi ya wafanyabiashara tuliwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria, kwa sasa hali imetulia na wanafanyabiashara kwa kufuata sheria na taratibu za leseni zao,” amesema na kuongeza:
Alipotafutwa jana Kamanda wa Kanda Maalumu wa Dar es Salaam, Jumanne Muliro kuhusu suala hilo amesema suala hilo atalizungumzia kesho Jumatatu na hivyo mwandishi aende ofisini kwake.
Juni 17, 2023, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbroad Mutafungwa alitangaza kukamatwa kwa watu sita wanaojihusisha na ununuzi wa vyuma chakavu wakiwa na nyaya zinazofanana na za Shirika la Umeme (Tanesco).
Aliwaonya wanaonunua vyuma vya wizi akisema watu hao walikamatwa wakati jeshi hilo likifanya uchunguzi kubaini wahusika wa wizi wa transfoma ya umeme eneo la Sagani wilayani Magu.
Imeandikwa na Tuzo Mapunda (Dar) Anania Kajuni na Daniel Mkaka (Mwanza), Hamida Sharif (Morogoro), Hawa Mathias (Mbeya), Idd Mumba (Katavi).