Fadlu aanza kupitia faili la Waangola

KIKOSI cha Simba kinaingia kambini kuendelea na mazoezi kujiandaa na mechi za kimataifa kwa wachezaji ambao hawakuitwa katika timu za taifa, huku kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids akiweka wazi maandalizi ya kimkakati ya kikosi hicho akisema ameanza kupitia mafaili ya timu pinzani CAF wakiwamo Waangola.

Simba inajiandaa kwa mchezo wa kwanza wa makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola, utakaochezwa Novemba 28, 2024, huku kocha Davids akichukua hatua za kuhakikisha timu yake iko katika kiwango bora kabla ya mchezo huo na mingine ya Kundi A lenye CS Constantine ya Algeria na CS Sfaxien ya Tunisia.

Katika kipindi kama hiki, Fadlu amekuwa akifanya mabadiliko katika mbinu za uchezaji na kujikita katika sehemu ambazo zimekuwa na udhaifu msimu huu, ikiwamo muunganiko wa viungo na washambuliaji.

Maandalizi ya mchezo dhidi ya Bravos do Maquis ni ya kipekee kwa sababu ni mechi muhimu ya michuano ya kimataifa na inaweza kuathiri safari ya Simba katika michuano ya CAF. Davids anajua kuwa kila hatua ya mazoezi inahitajika kufanyiwa kazi kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kuwa wachezaji wapo tayari kwa changamoto kubwa inayowakabili.

Fadlu amekuwa akifanya mazoezi ya makusudi ili kuboresha ufanisi wa safu ya ulinzi, ambapo amekuwa akifanyia kazi mabeki wake katika kuhakikisha wanakuwa imara dhidi ya mashambulizi ya wapinzani wao. Kocha huyo pia amekuwa akijitahidi kuongeza umakini katika mipira ya juu na mbinu za kukabiliana na mashambulizi ya haraka.

“Niko kwenye juhudi kubwa kuhakikisha kuwa timu yangu iko tayari kwa changamoto yoyote inayokuja. Maandalizi yetu tunazingatia kila kipengele cha mchezo, kuanzia ulinzi, viungo, na mashambulizi,” alisema kocha huyo na kuongeza;

“Tunajua kuwa mchezo dhidi ya Bravos do Maquis ni muhimu sana, hivyo tunajitahidi kujenga kikosi chenye nguvu kinachoweza kupambana na wao kwa usahihi. Hata hivyo, tunazingatia hali ya wachezaji wetu, kuwarudisha wakiwa na hali nzuri, na kuhakikisha kuwa kila mmoja anajua jukumu lake.”

Katika hatua nyingine, kocha Fadlu pia aliitakia kila la kheri Taifa Stars kwa michezo ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 ambapo itaanza ugenini dhidi ya Ethiopia Novemba 16 kisha kumalizana na Guinea nyumbani Novemba, ili kuungana na DR Congo iliyofuzu katika kundi hilo la H.

Kocha huyo wa Simba amesema kuwa Taifa Stars wanahitaji umoja na mshikamano ili waweze kutimiza malengo yao ya kufuzu kwa michuano hiyo mikubwa ya Afrika. Davids amekiri kuwa timu ya taifa ina wachezaji wenye uwezo mkubwa, na kwamba mchezo dhidi ya Ethiopia na Guinea ni nafasi nzuri ya kuonyesha kwamba Tanzania inastahili kuwa kwenye jukwaa kubwa la soka la Afrika.

Kocha huyo alisisitiza kuwa mechi hizi zitakuwa na ushindani lakini Stars inaweza kufuzu.

Related Posts