Songwe. Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Itumba wilayani Ileje, Mkoa wa Songwe, Huruma Ally amevamiwa na watu wasiojulikana na kumvunja miguu yote miwili.
Akizungumzia tukio hilo leo Jumapili, Novemba 10, 2024 mjini Ileje, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM wilayani hapa, Maoni Mbuba amesema uvamizi huo umetokea usiku wa kuamkia jana Jumamosi, Novemba 9,2024, huku chanzo kikiwa bado hakijafahamika.
Mbuba amesema katibu huyo amevamiwa saa nne usiku, eneo la Shule ya Msingi Itumba na aliokotwa na wasamaria wema akiwa katika hali mbaya, baada ya kuvunjwa miguu na kupoteza fahamu.
Amesema alipelekwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matibabu, huku akisema kitendo hicho hakikubaliki na kimezua taharuki hususani katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Mbuba amesema CCM Wilaya ya Ileje inalaani kitendo hicho, huku akiwataka wanasiasa na watu wa kada zote kuacha kujichukulia sheria mkononi.
“Tukio hili hatuwezi kulihusisha na siasa moja kwa moja… vyombo vya dola vinaendelea kufuatilia ili kubaini chanzo chake na ninaombea wahusika wapatikane na kukamatwa, ili sheria ichukue mkondo wake,” amesema Mbuba.
Amewataka wanasiasa wa vyama vyote wilayani Ileje katika kipindi hiki kuelekea kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa, wazifanye kwa ustaarabu na wajiepushe na matukio yanayohatarisha usalama wa raia na mali zao.
Akizungumza kwa simu na Mwananchi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea.
“Ni kweli katibu wa CCM kata ya Itumba amevamiwa na kuvunjwa miguu yote miwili na sasa amelazwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, watu waliohusika wamekimbia lakini tupo kazini kufuatilia wote waliohusika kusudi tuwafikishwe kwenye vyombo vya sheria,” amesema Kamanda Senga.