Kilichomponza Beimbaya hiki hapa | Mwanaspoti

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Kiluvya United ya mkoani Pwani, Twaha Beimbaya amesema sababu kubwa ya kutimuliwa ndani ya timu hiyo ni kutokana na uongozi mpya ulioingia madarakani, ila sio kwamba alishindwa kutimiza malengo aliyopewa mwanzoni.

Kocha huyo wa zamani wa Pan Africans, ametimuliwa ndani ya kikosi hicho baada ya kukiongoza katika michezo saba msimu huu ambapo kati ya hiyo ametoka sare mmoja na kupoteza sita, akikiacha nafasi ya 15, kwenye msimamo na pointi moja tu.

“Wakati naingia makubaliano na viongozi wa timu waliniambia wanataka ibaki tu Championship kwa sababu uwezo wa kupanda Ligi Kuu Bara isingewezekana kutokana na aina ya wachezaji waliopo, ila ghafla nikaona mipango imebadilika,” alisema.

Beimbaya aliongeza, mipango hiyo ilianza baada ya waliokuwa viongozi wa zamani alioingia nao makubaliano kuondoka ndani ya kikosi hicho wakiongozwa na Mwenyekiti, mweka hazina na meneja jambo ambalo limemsababishia kuondolewa na walioingia.

Timu hiyo ambayo inashiriki Ligi ya Championship msimu huu, imepanda daraja baada ya kuonyesha uwezo mkubwa na kumaliza nafasi ya pili msimu uliopita katika Ligi ya ‘First League’ nyuma ya mabingwa wa michuano hiyo African Sports ya Tanga.

Related Posts