Lina Tour yatibua kambi ya timu ya taifa

TIMU ya Taifa ya Wanawake ya Gofu, inaendelea na mazoezi kujiandaa na  Mashindano ya Ubingwa wa Gofu Afrika, yatakayofanyika mjini Agadir Morocco, Novemba 28 hadi 30 mwaka huu.

Wacheza gofu wa timu hiyo wanaendelea na mazoezi yao katika viwanja vya Arusha na Dar es Salaam gymkhana baada ya kuahirishwa kwa michuano ya Lina PG Tour  yaliyokuwa yaanze  Alhamisi hii jijini Dar es Salaam.

Akiongea  na Mwanaspoti, katibu wa mashindano kutoka chama cha gofu ya wanawake nchini(TLGU), Rehema Athumani alisema kuharishwa kwa raundi ya tano ya michuano hiyo, kumewafanya Madina Iddi na Neema Olomi kuendelea na mazoezi yao jijini Arusha, wakati mchezaji wa tatu, Hawa Wanyeche akiendelea na mazoezi katika viwanja vya TPDF Lugalo, jijini Dar es Salaam.

“Hapo awali ilipangwa wachezaji wote watatu wacheze katika michuano ya Lina Nkya kama mchezo wa mwisho wa kujinoa kabla ya kwenda mjini Agadir Morocco  kwa ajili ya mashindano ya ubingwa wa Afrika nzima,” alitanabaisha katibu wa mashindano wa TLGU.

Hata hivyo, Rehema Athumani hakutaja tarehe mpya ya mashindano ya Lina PG Tour na kusema umma utatangaziwa tarehe mpya wakati wowote juma hili.

Chama cha gofu ya wanawake nchini kiliwachagua Madina, Neema  na Hawa kuunda timu ya taifa kwa ajili ya mashindano ya gofu Afrika, baada ya wachezaji hao kufanya vizuri katika mashindano makubwa ya gofu nchini Ghana, Zambia, Kenya na Uganda.

Yakienda kwa jina la All Africa Golf Challenge Trophy, mashindano ya mwaka huu yatafanyika mjini Agadir, Morocco kutoka Novemba 28 hadi 30 mwaka huu.

Raundi ya tano ya michuano ya Lina PG Tour ilitakiwa kuanza  Novemba 14 mwaka huu na kumaliza Novemba 17 katika viwanja vya Dar Gymkhana, kabla ya kusogezwa mbele hadi Disemba mwaka huu.

Related Posts