NYOTA wa kimataifa wa Tanzania, Aisha Masaka anayekipiga Brighton ya Ligi kuu ya Wanawake England, amepata majeraha ya bega yaliyomlazimu kutolewa uwanjani kwenye mchezo dhidi ya Arsenal wa kichapo cha mabao 5-0.
Mchezo huo ni wa pili kupoteza kwa timu hiyo na wa pili kwa Masaka kucheza akiingia akitokea benchi baada ya awali kuingia dhidi ya Birmingham akitumika kwa dakika saba.
Masaka aliingia dakika ya 87 baada ya kutolewa Seike Kiko na dakika tatu alizocheza alionyesha kiwango kizuri hadi alipochezewa faulo na mchezaji wa Arsenal.
Pasi yake ya kwanza alichukua mpira na kupeleka mashambulizi lango la Arsenal kabla ya kuchezewa vibaya nje kidogo ya 18 na kushindwa kuendelea na mchezo akilazimika kutolewa kwa machela.
Kocha wa timu hiyo, Dario Vidosic alisema licha ya kupoteza mchezo huo lakini nyota wake walitengeneza nafasi nyingi ikiwemo ya Masaka.
“Hatujashinda lakini timu yetu ilitengeneza nafasi nyingi ikiwemo Masaka aliyepokea pasi na kupiga shuti, bahati mbaya akachezewa vibaya. Hatutakata tamaa na badala yake tutaendelea kupambana na kuhakikisha haturudii makosa,” alisema kocha huyo aliyewahi kuichezea Man City.