MBEYA Kwanza inayoshiriki Ligi ya Championship, inatyarajiwa kutest mitambo kwa kuvaana na Namungo iliyopo Ligi Kuu Bara, huku ikielezwa benchi la ufundi linauchukulia mchezo huo kwa uzito mkubwa kwani ni kipimo kizuri kwa wachezaji kabla ya kukutana na Polisi Tanzania katika ligi Novemba 16.
Meneja wa Mbeya Kwanza, iliyowahi kucheza Ligi Kuu kabla ya kushuka daraja, Salum Telela kiungo nyota wa zamani wa Yanga na Moro United, amesema mchezo huo dhidi ya Namungo utakuwa kipimo kizuri kwa timu hiyo, kujua kiwango cha wachezaji ili kurekebisha makosa mapema, kwani malengo yao wanahitaji kukaa nafasi tatu za juu katika msimamo wa ligi hiyo.
Kwa sasa timu hiyo, ipo nafasi ya tano, imevuna pointi 14 kwa mechi nane iliyocheza, hivyo mchezo ujao dhidi ya Polisi Tanzania inajipanga kuhakikisha inashinda, ili izidi kupanda nafasi ya juu zaidi.
“Tunacheza na Namungo kesho Jumatatu saa 10:00 jioni, Uwanja Nagwanda Sijaona, mchezo huo ni kipimo kizuri kwa upande wetu, kwani itatuonyesha kipi kinatakiwa kwa wachezaji. Ligi ya Championship ni ngumu inahitaji wachezaji wawe fiti na kiwango cha juu, ili kupata matokeo ya ushindi ili kuyafikia malengo ya kukaa nafasi tatu za juu katika msimamo wa ligi hiyo,” alisema Telela.
Mbali na hilo, Telela amesema kwa sasa ametofautisha presha ya uwanjani na kukaa benchi, tofauti na kipindi alichokuona anacheza alichukulia wachezaji ndio wanaobeba mzigo mzito, kuliko viongozi.
“Kuna wakati wanaocheza nafasi yangu wakikosea natamani niingie nicheze,ila ndio mpira kila kitu kinatakiwa kiendelee mbele,” amesisitiza staa huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kukilopiga Ndanda FC ya Mtwara ambaye kitaaluma ni Mhasibu wa Chama cha Soka cha Mkoa huo wa Mtwara.
Telela akiizungumzia Ligi Kuu Bara, amesema kati ya wachezaji wanaomkosha katika nafasi aliyokuwa anaicheza, ni kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutokana na mikimbio yake, anajua kufunga na kutoa pasi za mwisho.
“Feisal ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, anafanya kazi nyingi uwanjani, namuona mbali na atafanya vitu vingi katika soka,” amesema Telelsa.