Mh.Mwinjuma amtembelea mzee Zorro atoa msaada wa vifaa vya mazoezi

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, amemtembelea msanii mkongwe nchini Zahir Ally Zorro (Mzee Zorro) nyumbani kwake Kigamboni Dar es salaam jioni ya Novemba 9 2024, na kumpatia msaada wa vifaa vya mazoezi ikiwa ni sehemu ya ahadi yake kwa Mzee Zorro aliyotoa siku chache zilizopita akiwa kwenye uzinduzi wa vionjo vya album ya Fid Q na Lord Eyes iitwayo ‘Neno’.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo, Mzee Zorro amesema, “Namshukuru Mungu sana, namshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Mhe. Naibu Waziri, Hamis Mwinjuma amekuwa na mwitiko wa haraka kwenye suala langu, Mungu ambariki sana, Nitaendelea kumuombea. Mimi siumwi chochote, ni kwa sababu ya hii miaka sabini. Nitavitumia vifaa hivi, nitaanza kidogo kidogo kwa mikono, baadaye nitaanza kuitumia baiskeli, Naamini nitakaa sawa.”

Kwa upande wake Mh. Mwinjuma baada ya kukabidhi vifaa hivyo, ameahidi kuendelea kumfuatilia Mzee Zoro kwa ukaribu hadi atakaporejea kwenye hali yake ya kawaida, aidha amesema msaada huo unadhihirisha dhamira ya Serikali katika kutambua mchango wa wasanii wa sanaa zote na kuwasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika maisha yao.

Mhe. Mwinjuma, kwenye safari ya kwenda nyumbani kwa Mzee Zorro aliambatana na msanii maarufu Nchini, Ambwene Yesaya (AY).

Related Posts