Mtengwa aeleza ushindani Uganda | Mwanaspoti

KINDA la zamani la Yanga U-20, Isack Mtengwa amesema licha ya kucheza kwa mkopo Wakiso Giants ya Uganda lakini wanapata uzoefu wa kimataifa.

Akizungumza na Nje ya Bongo, Mtengwa alisema licha ya ligi ya nchi hiyo bado ndogo, lakini vijana wanaochipukia wanapata uzoefu.

“Uganda ligi yao bado haijakuwa, hata wachezaji wanaocheza wengi ni vijana, kwa hiyo uwepo wetu sisi tunajifunza vitu vingi tofauti na Tanzania hadi upewe nafasi ya kucheza kwenye timu angalau umepita timu mbalimbali au wamekukuza wenyewe,” alisema Mtengwa.

Aliongeza wanapoaminiwa na kocha wanapambana kuhakikisha wanaisaidia timu, kwani timu hiyo ina wachezaji wengi wazuri wanaowapa ushindani kikosini.

“Unapopata nafasi unashukuru Mungu kwa sababu kwanza kwenye timu wachezaji wengi wazuri, hivyo kocha anavyotuamini na sisi tunarudisha imani yake kupitia muda anaotupa kucheza.”

Wakiso imecheza mechi nane lakini kinda huyo akipata nafasi ya kucheza na kuanza kwenye baadhi ya mechi ambazo timu hiyo imeshiriki.

Related Posts